Namna bora ya kurekebisha taa za mbele za gari lako

Taa ni moja kati ya vifaa muhimu kwenye gari kwa sababu husaidia kutoa mwanga. Vifaa hivi hutumika wakati wa giza au kikwazo cho­chote kinachosababisha kukoseka­na kwa mwanga, kama vile ukungu wa mvua na moshi.

Mfumo wa taa za gari umega­wanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni upande wa mbele na upande wa nyuma. Taa za upande wa mbele wa gari ambazo kimsingi zipo za aina tatu ambazo ni, taa kubwa za mbele ambazo hutumika kuanzia giza linapoingia mpaka lin­apoisha asubuhi pamoja na sehemu zenye handaki (tunnel) na nyakati za ukungu au mvua.

Taa hizi ni muhimu zaidi kwa sababu zinamsaidia dereva kuona vyema mbele katika sehemu ambazo zina vikwazo tajwa hapo juu hivyo ni muhimu kuwa katika hali nzuri wakati wote.

Ikiwa wewe ni mmiliki wa gari na ushawahi kukutana na tatizo la taa za mbele za gari lako kupishana uelekeo wa kumulika, ama moja inamulika kwa juu na nyingine chini au zote kumulika kwenda juu zaidi au chini zaidi ya eneo sehemu iliyopaswa, basi fahamu kwamba hili ni tatizo kubwa ambalo linahi­taji ufumbuzi wa haraka.

Hivyo kama ulikuwa hufahamu namna ya kuziweka/kuzirudisha kwenye sehemu yake mpaka umu­one fundi, kwenye makala haya nitakupa mbinu rahisi ambazo unaweza kuzitumia ili kuhakikisha unashughulikia tatizo hili bila kuin­gia gharama ya kupeleka gari kwa fundi.


Vifaa vinavyohitajika

Zoezi la kurekebisha taa za mbele za gari lako ili ziwe kwenye uwiano sawa unaweza kulifanya mwenyewe ukiwa na vifaa kama; ubao au unaweza kutumia ukuta, bisibisi, tape measure, kipima upepo tairi (siyo lazima sana) na uwe na sehemu salama ya kuegesha gari lako. Ili kazi yako iwe na ura­hisi ni muhimu kuwa na hivi vifaa na sehemu nzuri na salama nzuri ya kuegesha gari lako.


Utaratibu za kufuata kurekebisha taa

Ili utekeleze zoezi hili unatakiwa kungalia kiasi cha upepo wa tairi zote na hakikisha upepo usipun­gue 30 tairi za mbele na 35 tairi za nyuma, egesha gari lako mita 7.5 kutoka ulipo ubao au ukuta unaotumia kurekebishia taa zako, hakikisha mahali ulipoegesha pako usawa (level moja), isiwe na mui­nuko au bonde.

Safisha taa zako vizuri, ziba taa moja kwa kitambaa au hata boksi, washa taa za gari lako kuelekezea ubao au ukuta ulioutenga kwa kazi hiyo, weka alama kwenye mchoro wa ubao wako, rudia tena zoezi kwa taa nyingine (fanya zoezi hili kwa taa zote mbili). Kama taa zako zinamulika eneo sahihi unaweza kukaza nati zako na utakuwa umemaliza kazi.