Unafahamu muda sahihi wa kubadilisha oili ya gari?

Kwa kawaida gari haliwezi kutembea bila oili. Oili inawezesha injini kufanya kazi vizuri bila kujali ni changamoto gani zinatokea ndani ya chombo hicho.

Ili kufahamu umuhimu wa oili kwenye gari lako, ungana na mimi kwenye makala haya ili ufahamu namna kimiminika hicho kinafanya kazi.

Oili ya gari ni kimiminika kilichotengenezwa ili kulainisha sehemu za ndani ya injini na kusa­babisha ifanye kazi kama bila msuguano wa vifaa vyenye asili ya chuma ambao huweza kuzalisha joto lisilo la kawaida.

Oili pia husaidia kusafi­sha injini na kupunguza joto kwa sababu bila kimiminika hiki muhimu, sehemu za injini ya gari zingekuwa chafu na ingepata joto lisilo la kawaida, vyuma kulika na hata kuharibika.

Oili nyingi ya kisasa yanayo­tumika kwenye magari zimeten­genezwa kwa aina mbili ambazo ni; oili safi yasiyochanganywa na kemikali (refined oils) na ile iliyochanganywa (additives).

Oili safi inatokana na mafuta yasiyosafishwa (crude oili) ambayo huzalishwa na ‘haidrokaboni’ kuto­ka kwenye matabaka ya miamba.

Aina ya pili ya oili (additives) hupendelewa sana na watengene­zaji wengi wa magari. Wakati mwingine, aina hii ya oili inadaiwa kuwa na viambata sabuni, wengine wakidai kwamba inaongeza ulinzi wa vifaa vya ndani ya injini.


Namna ya kuangalia kiwango cha oili kwenye injini

Unaweza kuangalia kiwango cha oili kwenye injini ya gari lako kwa kutumia kijiti maalumu (dipstick) ambayo hutumbukizwa kwenye tanki.

Gari likiwa limezimwa, unataki­wa kuitoa dip-stick, kuifuta, kisha kuirudisha tena kwenye tanki ili kuweza kufahamu kiwango cha oili kilichopo kwa wakati huo.

Ukishaitoa unatakiwa kuisoma ili ujue ni kiasi gani kilichopo kwa sababu dipstick ina alama ambazo zinaonyesha viwango tofauti vya kiasi cha oili kilichopo kwenye tanki kwa wakati huo.


Muda sahihi wa kubadilisha oil

Suala la muda wa kubadili oili kwenye gari limekuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa watumiaji wa vyombo vya usafiri.

Kwa sheria za magari ya zamani zilikuwa zinaelekeza kubadili oili kila gari linapotembea maili 3,000 lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia katika utengenezaji wa injini za magari wengi wanaona kwamba kiwango hicho kinapoteza muda na fedha, hivyo huweka oili inayoduni umbali mrefu zaidi.