Namna chakula kinavyoweza kugeuka sumu 

Muktasari:

  • Vyakula huzalisha sumu hasa vinavyopikwa na kukaa muda mrefu bila kuhifadhiwa vizuri.

Dodoma/Dar. Matukio ya familia kula chakula na baadaye kuathirika ikielezwa kilikuwa na sumu yamekuwa yakiripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari mara kadhaa.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kimaabara imebainika kwa baadhi ya matukio hayo hayakuhusika na sumu kutoka nje ya chakula kwa maana ya kuwekwa na mtu.

Kutokana na hilo, Mwananchi Digital imefanya mahojiano na wataalamu wa afya na lishe kuzungumzia suala hilo. 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wenye shida ya kula chakula chenye sumu.

Amesema wakati mwingine sumu hiyo si inayotoka nje ya chakula bali inayozalishwa na chakula chenyewe (food poison) ambayo husababishwa na mambo kadhaa wakiwamo wadudu.

Dk Ibenzi amesema kuna baadhi ya vyakula vikipikwa au vikikaa muda mrefu husababisha bakteria ambao wakiingia tumboni mwa mtu humletea madhara ya kiafya, hivyo huonekana kama amekula chakula chenye sumu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili na ajali kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguju amesema kuna baadhi ya vyakula ambavyo vyenyewe ni sumu, hivyo mtu anapokula ni lazima apate madhara ya afya.

Dk Ubuguju amesema pia kuna kemikali ambazo zikiingia kwenye mimea si rahisi kutoka, hivyo mwanadamu akitumia mimea hiyo kama chakula anapata madhara ya kiafya na kuonekana kama amekula sumu.

“Kwa mfano kuna aina ya uyoga ambao ni sumu, hivyo mtu akila ni lazima atapata madhara ya kiafya. Pia kuna vyakula vingine vya kienyeji ambayo vina utaalamu wake katika kuandaa, ambavyo vikiandaliwa vibaya vinaweza kuleta madhara kwa walaji kama vile kisamvu kisipopikwa kikaiva vizuri,” amesema Dk Ubuguju.

Desemba mwaka 2023 wanafunzi wawili mkoani Mwanza walifariki dunia kwa kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu, huku watu wengine saba kutoka familia mbili walilazwa kwa ajili ya matibabu.

Mkurugenzi msaidizi wa huduma za lishe kutoka Wizara ya Afya, Neema Joshua amesema hakuna chakula ambacho ni sumu moja kwa moja kwa kuwa si rahisi kitu kiwe sumu halafu kiwe chakula.

Amesema watu wanaopata madhara baada ya kula aina fulani ya chakula inaweza kuwa inasababishwa na muingiliano wa maambukizi kutokana na chakula chenyewe au hata kutoka nje ya chakula.

“Kwa mfano chakula kinaweza kuwa kimeandaliwa vizuri wakati wa kukipika lakini kumbe uhifadhi wake ulikuwa mbaya, hasa kwa mazao ya karanga na mahindi hivyo kusababisha kupata sumu kuvu ambayo huathiri afya za walaji, lakini ukiangalia ugali si sumu,” amesema Neema na kuongeza:

“Hivyo hata uyoga si sumu lakini kuna aina ambazo mtu akila inamletea madhara. Hata hivyo, hailiwi kwa sababu si chakula, kitu chochote ambacho kina madhara kwa binadamu si chakula.”

Ameitaka jamii kuhakikisha chakula kinaandaliwa kwenye usafi wa hali ya juu ikiwamo vyakula ambavyo vinaweza kuathiriwa na sumu kuvu kama vile unga wa mahindi, wa muhogo na karanga kwa kuwa sumu hiyo inasababisha madhara makubwa kwenye mwili wa binadamu, ikiwamo kifo.

Ofisa lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, Wilbert Mgeni, amesema vipo baadhi ya vyakula ambavyo visipoandaliwa vizuri vinaweza kugeuka sumu na wakati mwingine kuingilia matumizi ya virutubisho vingine mwilini.

Mgeni amesema kati ya hivyo, vipo vyenye asili ya mizizi ikiwamo mihogo na majani yake.

“Mihogo mingine inakuwa na asili ya uchungu, ndani yake kunakuwa na madini ya sianidi ‘cyanide’ ambayo ni sumu na inakuwa zaidi kwenye mihogo michungu,” amesema.

Amesema miaka ya nyuma wakazi wa Kilimanjaro waliripotiwa kufariki dunia baada ya kula mihogo michungu ambayo unga wake waliupikia ugali na majani yake wakayapika kisamvu na kujikuta wakipoteza maisha.

Hata hivyo, amesema ili kuondoa sumu hiyo kwenye mihogo, kabla ya kupikwa au kutengenezwa unga inapaswa kulowekwa kwenye maji kwa muda mrefu, ikiwezekana kwa siku mbili ili sumu hiyo itoke katika hali ya usalama.

“Vilevile watu wanaweza kuepuka sumu hii kwa kuacha kula mihogo kipindi cha jua kali (kiangazi), kwa kuwa katika kipindi hiki   sumu hiyo huzalishwa kwa kiasi kikubwa kuliko wakati wa mvua,” ameshauri.

Kwa vyakula vya asili ya mikunde, amesema kuna soya ambayo shida yake inaingiliana na madini ya chuma.

“Hivyo soya isipotengenezwa vizuri husababisha upungufu wa damu kwa kuwa inaingilia ufonzwaji wa madini ya chuma,” amesema

Katika kuondoa tatizo hilo, Mgeni amesema soya inapaswa kuchemshwa kwa dakika zisizopungua 40 na baada ya hapo inapaswa kutolewa maganda ya juu na kuanikwa, ndipo huwa salama zaidi kwa matumizi.

Vyakula vingine vya kunde anavyovitaja kuwa na asili ya sumu ni maharage yanayopendwa katika mikoa ya Kusini, yanayojulikana kwa jina la upupu au maharage pori.

“Huo upupu usipoandaliwa vizuri mtu akila anaweza kufa, hivyo ili kuondoa sumu watu wa huko Kusini huwa wanayachemsha usiku kucha na kunapokucha humwaga maji yake. Usipofanya hivyo mtu akila anapoteza maisha,” amesema.

Vyakula vingine ambavyo maandalizi yake yasipofanyika vizuri yanaweza kuwa na sumu, amesema ni mahindi, ngano, ulezi na karanga ambavyo huwa na sumu kuvu.

Amesema sumu kuvu hutokana na uhifadhi wa nafaka usipofanyika vizuri ikiwamo kupata unyevunyevu, huwa na kama ukungu ambao ndiyo huitwa sumu kuvu.

“Sumu hii ni hatari kwa afya ya binadamu kwa kuwa huenda kuathiri ini, matokeo yake mtu anayekula hupata saratani ya ini na mwisho wa siku hupoteza maisha,” amesema.

“Hivyo ili kuepukana na sumu wakulima, wauzaji na walaji wahakikishe nafaka hizo zinakauka vizuri kabla ya kuhifadhiwa au kuhifadhi eneo salama ambalo halitasababisha kupatikana kwa sumu kuvu,” amesema.

Vyakula vingine vinavyoweza kugeuka sumu kama havitaandaliwa vizuri ametaja kuwa chai ya rangi au kahawa, ambayo mtu akiinywa huenda kuingilia mfumo wa madini chuma na mwisho wa siku mtu kujikuta akiwa na upungufu wa damu.

“Ndiyo maana tunawashauri wajawazito, kama wanataka kunywa chai ya rangi au kahawa, anywe saa moja kabla au baada ya kula chakula kwa kuwa huingilia mfumo wa madini ya chuma, hivyo kupata upungufu wa damu,” amesema.

Katika kusaidia madini haya yasichukuliwe mwilini na vinywaji hivyo, mtaalamu huyo ameshauri ni vema vikachanganywa na maziwa ili kupunguza nguvu ya sumu inayopatikana ndani yake.

Inaelezwa na wataalamu wa lishe kupitia machapisho mbalimbali kwamba, chakula kinaweza kuwa sumu mwilini kama kina viungo au kemikali hatari kwa afya ya binadamu.

Kuna aina kadhaa za chakula au vichocheo vinavyoweza kuwa sumu kama vile:

Sumu ya Kemikali

Zipo kemikali zinazopatikana kwenye chakula zinaelezwa zinaweza kuwa sumu. Hii inaweza kutokea kwa mfano kupitia matumizi ya viuatilifu au dawa za wadudu katika kilimo na pia kutokana na mchakato wa usindikaji wa chakula.


Sumu ya kiasili

Kuna baadhi ya mimea na wanyama inaelezwa wanaweza kuwa na sehemu zinazosababisha madhara kwa afya. Kuna mimea inayojulikana kama sumu, na pia wanyama wengine ambao wanaweza kuwa na sumu, kama vile nyoka au buibui.

Sumu ya kuvu

Baadhi ya vyakula vinaweza kushambuliwa na kuvu zenye sumu. Kuvu hizi zinaweza kutoa kemikali zinazoweza kuwa hatari kwa afya ya binadamu, na hii inaweza kutokea katika nafasi zenye unyevu au chakula kilichoharibika.

Sumu ya metali nzito

Vyakula vinaweza kuwa na kiwango kikubwa cha metali nzito kama vile risasi na zebaki ambavyo vinaweza kuwa na madhara kwa afya ya binadamu.

Sumu ya kupikwa vibaya

Wakati mwingine chakula kinaweza kuwa sumu ikiwa kimepikwa vibaya au kisichopikwa vizuri.

Hii inaweza kusababisha maambukizo ya bakteria au virusi vinavyoweza kusababisha magonjwa.

Mbali ya hayo, sumu ya chakula (food Poisoning) ambayo ni hali inayotokea baada ya kula au kunywa kitu ambacho kina vimelea vya bakteria, virusi, kuvu, au sumu nyingine ambazo zinasababisha madhara kwa afya imekuwa ikiwasumbua wengi.

Dalili za sumu ya chakula zinaelezwa zinaweza kujitokeza haraka baada ya ama kula chakula kilichoharibiwa au kunywa maji yenye vimelea, pia zinaweza kuonekana baadaye kulingana na aina ya vimelea na kiasi kilichoharibu mwili.

Inaelezwa dalili zake ni kichefuchefu, kutapika, kuharisha, tumbo kuhisi vibaya na homa.

Kutokana na hayo, inashauriwa kwamba ni muhimu kuchukua tahadhari wakati wa kuandaa, kuhifadhi na kula chakula kwa kuhakikisha kinapikwa vizuri, kuhifadhiwa katika joto sahihi, na kuepuka kula kilichoharibika.

Imeandikwa na Rachel Chibwete (Dodoma na Nasra Abdallah (Dar).