Namna ya kubadili balaa la mafuriko kuwa neema

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Abdulrahman Kinana akiwa kwenye boti alipoenda kuangalia maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika Kijiji Cha Muhoro, leo Aprili 9, 2024 na kuwapa pole wakazi wa Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani waliokumbwa na mafuriko hayo. Picha na CCM
Uwekezaji wa teknolojia ya kisasa na miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ni mambo yanayopendekezwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, wakisema yanaweza kubadili changamoto ya wingi wa maji yatokanayo na mvua zinazoendelea kuwa fursa.
Mapendekezo mengine ni kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kufanya uwekezaji, kujenga makazi kwa kuzingatia sheria ya mipango miji, matumizi bora ya ardhi, kutengeneza sera na sheria zinazoelewana na sekta zote muhimu.
Wadau mbalimbali wanaamini kwamba kuwa na mipango thabiti, laana itokanayo na mvua kubwa zinazonyesha inaweza kugeuka kuwa neema, hususani wakati wa kiangazi na msimu wenye mvua kidogo.
Pia wanaamini kuwa jambo hilo likisimamiwa vizuri litasaidia hata kupunguza gharama za ujenzi kwa miradi mikubwa, lakini pia kupunguza gharama ya ukarabati wa miundombinu katika maeneo tofauti.
Mpaka sasa mvua zinazoendelea zimesababisha kuharibika kwa miundombinu, mali za watu lakini kubwa zaidi maisha ya watu yamepotea, huku vijiji kadhaa vikisombwa na maji katika mikoa tofauti, hususan mkoani Pwani katika Wilaya za Rufiki na Bibiti.
"Nilipokuja huku nilipata shamba nimelima, mazao ya kwanza yalizama, ya pili yamezama na nyumba," anasema Bahati Msura, mkazi wa Kijiji cha Mohoro wilayani Rufiji aliyehamia hapo mwaka mmoja uliopita.
Wakati wengi wakilia na changamoto ya mafuriko wanayokutana nayo hivi sasa katika maeneo yao, wengine wanakumbuka namna walivyokutana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya misimu, hali iliyosababisha mgawo, kukosekana kwa umeme, mifugo kufa na mazao yao kuharibika.
“Sasa hivi tunasikia mafuriko katika maeneo tofauti, lakini kesho utasikia tuna shida ya maji kwa sababu mvua hazijanyesha, wenzetu walishatoka huko. Maji yanavunwa yanatumika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi mvua zikiisha, wengine wanaanzisha mabwawa, mifereji na mengine ili kuhifadhi maji,” anasema Ayub Tarimo, mkazi wa Dar es Salaam.
Ofisa kutoka taasisi ya Door of Hope, inayojihusisha na Mabadiliko ya Tabianchi, Shamim Nyanda anasema aliunga mkono hoja ya Tarimu, akisema nchi inahitaji kuhamasisha na kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa na kujenga miundombinu ya kuwezesha kuvuna na kuyahifadhi maji ya mvua na kuyatumia kipindi cha ukame.
“Kuna nchi nyingi zilizoendelea zinafanya hivyo, teknolojia hiyo inawezesha kuyavuna hayo maji yanayoweza kusababisha mafuriko na baadaye yanatumika kwenye shughuli za kilimo cha umwagiliaji pamoja na viwandani,” anasema.
Japo katika maelezo yake Shamim anaonesha wasiwasi wake, akisema kutozingatia sheria ya mipango miji mathalani katika Jiji la Dar es Salaam inaweza kuwa kikwazo kuvuna kwa sababu nyumba nyingi zimejengwa hadi kwenye mikondo iliyotakiwa kupitisha maji.
“Yapo maeneo nchi hii hayana maji ya uhakika na kwa kawaida wanasubiri mifumo ya mabomba. Lakini ingewezekana kukajengwa mifumo imara ya kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya watu, mifugo na mimea, hasa katika maeneo yasiyo na maji ya uhakika,” anasema Ofisa Programu Mkuu wa Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi (Forumcc), Msololo Onditi.
Anasema jitihada hizo zikifanyika zitasaidia kupunguza gharama kubwa za kulaza mitandao ya mabomba na kutumia nishati kufikisha maji kwa wananchi na kuondoa utegemezi wa kilimo kinachotegemea mvua ili kuwa na uhakika na usalama wa chakula.
“Badala ya kuweka miundombinu ya kuhimili mafuriko, ni vema ile ya kuvuna maji. Mfano kama tutajenga mifereji ya kukusanya maji mijini, basi mifereji hiyo ielekezwe katika matenki ambayo yatahifadhi sehemu ya maji hayo badala ya kuyaachia yote yaelekee mitoni, ziwani au baharini,” alisema.
Onditi anaongeza kuwa Serikali inaweza kupunguza gharama za ujenzi katika miradi yake, hususan upatikanaji wa maji kwa kuandaa mifumo ya uvunaji wa maji katika maeneo ya miradi .
“Tunaamini Serikali ina mipango ya muda mrefu, hivyo inawezekana kukawa na mipango ya namna hii na kutumia mafuriko au mvua nyingi kuvuna maji ya mvua na kurahisisha shughuli za ujenzi.”
Anasema mafuriko pia yanaweza kutumiwa kuzalisha umeme. Katika ulimwengu wa sasa, ni vema wakati wa mvua nyingi na mafuriko kukawa na miundombinu ya kuzalisha umeme na kuuhifadhi ili yatumike wakati wa ukame,” anasema.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Ponsian Ntui anasema kabla ya kufikiria kujenga miundombinu hiyo au uwekezaji, ni lazima utafiti wa kutosha ufanyike kwa kuzingatia historia ya eneo na aina ya dongo ili kuepuka hasara ya matumizi ya fedha za umma.
“Ukifuatilia miundombinu mingi iliyojengwa hapa nchini, ukiangalia unakosa majibu kujua kama kweli utafiti ulifanyika au waliamua kujenga tu baada ya kupata fedha. Kuna maeneo mengi kama jangwani wamejenga vituo vya Mwendokasi au vituo vya kupaki magari,” nasema
Alisema changamoto kubwa inayojitokeza wakati mwingine inasababishwa na mbinu za kihandisi kiasi cha kuzikosesha kampuni za kizawa tenda za kazi zinazohitaji kujifunza zaidi.
“Jambo la pili mafuriko yanatokana na maji na yana mikondo yake, inatakiwa turejee kwenye ujenzi wetu kama unazingatia historia ya mikondo ya maji na tunatakiwa kuyapeleka sehemu gani kwa shughuli za uchumi,” anasema.
Anasema Serikali inatakiwa kujipanga kuhakikisha wananchi wanachimbiwa mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji, kuhamasisha dhana ya uchumi jumuishi kwa kufanya shughuli za kilimo kwa wakati wote badala ya kutegemea kulima kwa msimu.
“Hasa kwa maeneo ya Kanda ya Kati yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, wachimbiwe mabwawa ya kuhifadhi maji ili wafanye shughuli za kiuchumi kwa muda wote, ikiwemo ufugaji wa mifugo na samaki,” anasema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja naye anasema ni muhimu wahusika kutoka sekta zote kutambua mabadiliko hayo ya ndani na nje kutumia changamoto hiyo kuwa fursa.
“Nchi yetu ina ardhi kubwa ya aina nyingi kuna sehemu za milima, mabonde na tambarare. Ni muhimu kujua maji yanatoka kwa wingi sehemu zipi na uelekeo wake, ni suala la wizara zote; Maji, Teknolojia na Ardhi kushirikiana kupanga pamoja kwa kuwa na sera na sheria zinazoelewana,” anasema.
Mchumi huyo mwandamizi anasema Tanzania inategemewa na Afrika kutokana na ukubwa wake wa ardhi inayoweza kutumiwa kuzalisha mazao ya chakula ya kujitosheleza na kusaidia wengine.
“Wizara za ndani ni lazima zishirikiane pamoja na taasisi za nje na kuzitumia taarifa zinazotolewa na mataifa makubwa, na kingine ni kuja na miradi ya ujenzi wa mabwawa ili kulinda ujazo wa maji kwenye mito, hasa kipindi cha mvua,” anasema Profesa Semboja.
Kuhusu upangaji bora wa matumizi ya ardhi, mwanaharakati wa mazingira, Clay Mwaifwani anasema kukosekana kwa mipango hiyo kunasababisha watu kuingilia miundombinu ya maji kufanya shughuli za kilimo na kujenga kwa kila mtu kuamua cha kufanya.
“Kama matumizi yatapangwa huduma za kijamii zitafanyika sehemu yake na njia za maji zisiingiliwe na ikaheshimiwa, ndiyo maana watu wengi hawana hati hata za kimila, hawana kwa sababu maeneo hayajapimwa,” anasema.
Anaongeza: “Tunatakiwa kuheshimu uoto wa asili, pembezoni mwa mito kunakuwa na mikoko na miti mingine, tuache kuvamia, lakini tunapaswa kutengeneza sheria ya mabadiliko ya tabianchi inayozungumza kwa upana wake ili kila mmoja atimize wajibu wake”.