Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nanauka: Serikali imeanza utekelezaji ahadi kwa vijana

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo ya pikipiki kwa vikundi vya vijana wa Bodaboda wilayani Kyela mkoani Mbeya kupitia program ya bilioni 200 chini ya mfuko wa maendeleo ya vijana. Picha na Sadam Sadick

Muktasari:

  • Katika hafla hiyo, jumla ya pikipiki 22 zenye thamani zaidi ya Sh87 milioni zimetolewa kwa vikundi viwili vya vijana kwa lengo la kuwainua kiuchumi kupitia program ya Sh200 bilioni chini ya mfuko wa maendeleo ya vijana.

Mbeya. Serikali imesema itahakikisha inasimamia na kutekeleza ahadi na kuwafikishia fursa vijana kwa usawa na kuwainua kiuchumi kwa kutatua changamoto zao na kuondoa kero zinazokwamisha.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Julai 13, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka wakati wa hafla ya utoaji mikopo kupitia programu ya Sh200 bilioni chini ya mfuko wa maendeleo ya vijana iliyofanyika wilayani Kyela, mkoani Mbeya.

Nanauka amesema Serikali imejipanga kusimamia na kutekeleza maelekezo ya Rais Suluhu Hassan, katika kutatua changamoto za vijana na kuwafikishia fursa kwa usawa.

Amesema mbali na kutatua changamoto, wataondoa na kurekebisha masuala yanayowakwamisha vijana kustawi kiuchumi na kwamba yapo mambo mawili yaliyopitishwa na bunge kuwa sheria.

"Moja ni kuongeza mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kufikia asilimia 15. Hiyo tano ni kuboresha miundombinu, sheria ya pili ni marekebisho ya kodi, ambapo eneo hili lilikuwa na changamoto kwa vijana lakini imefanyiwa marekebisho," amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka (aliyevaa tisheti nyeusi) akikabidhi mikopo ya pikipiki kwa vikundi vya vijana wa Bodaboda wilayani Kyela mkoani Mbeya kupitia program ya bilioni 200 chini ya mfuko wa maendeleo ya vijana. Picha na Sadam Sadick

Amesema kijana anapoanzisha biashara hatadaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) badala yake atasubiriwa kwa kipindi cha miezi 12  lengo ni kumpa muda kujipanga.

Waziri huyo amesema uwezeshaji huo unaofanywa na Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na kwamba lengo ni kujenga uchumi shindani na jumuishi.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Celina Mtenya amesema jukumu la Serikali ni kuwaunganisha vijana na fursa zinazotokea na kwamba kwa mwaka wa fedha wa 2025/26, Sh4.6 bilioni zimetolewa kwa vikundi vya vijana 576 sawa na asilimia nne ya mapato ya ndani.

Mikopo hiyo, amesema imewainua vijana kiuchumi, baadhi yao wanamiliki shule za mchepuo wa kiingereza, zahanati na vyombo vya moto.

"Ipo pia mikopo kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa wafanyabiashara wadogo, ambapo tayari Sh630 milioni zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya 268 kwa Mkoa wa Mbeya," amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Frolah Luhala, amesema kupitia programu hiyo, jumla ya pikipiki 24 zenye thamani ya zaidi ya Sh87 milioni zimetolewa kwa vikundi viwili vya vijana wilayani humo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka (aliyevaa tisheti nyeusi) akikabidhi mikopo ya pikipiki kwa vikundi vya vijana wa Bodaboda wilayani Kyela mkoani Mbeya kupitia program ya bilioni 200 chini ya mfuko wa maendeleo ya vijana. Picha na Sadam Sadick

Amesema mikopo hiyo itawasaidia vijana kuwa na uhakika wa kazi zinazowaingizia kipato na kuendesha maisha yao kwakuwa haina riba.

"Lakini kwa mwaka wa fedha wa 2025/26, Halmahauri kupitia zile asilimia 10, tumetoa Sh1.8 bilioni, kati ya hizo Sh902 milioni ni kwa vijana pekee, hivyo wahakikishe wanarejesha ili wengine wapate,” amesema.

Mmoja wa wanufaika kundi la Bodaboda Matema, Daud Mwaisuna, amesema mkopo huo unaenda kuwabadilisha uchumi na kutengeneza ajira nyingine kwa walio chini yao.

"Tunaishukuru Serikali na tunaahidi kurejesha mikopo hii ili tuweze kukopa tena lakini kufungua fursa nyingine kwa makundi mengine," amesema.