Sh200 bilioni za vijana zaanza kutolewa Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka,akikabidhi hundi ya mfano wa kikundi cha Umalita Arusha, wakati wa uzinduzi wa Programu ya Sh200 bilioni chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, leo Alhamisi Julai 9, 2026 mkoani Arusha.
Muktasari:
- Mafanikio ya programu hii hayatapimwa kwa kiwango cha fedha kilichotolewa, bali kwa matokeo yatakayopatikana. Tunataka kuona biashara zenye tija, ongezeko la ajira, mapato ya wananchi na ukuaji wa kampuni zinazoendeshwa na vijana
Arusha. Serikali imeanza rasmi utoaji wa mikopo kupitia Programu ya Sh200 bilioni ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, huku Mkoa wa Arusha ukiwa wa kwanza kunufaika baada ya kupokea Sh730 milioni kwa ajili ya kufadhili miradi ya vijana.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo Alhamisi, Julai 9, 2026 jijini Arusha, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema Serikali imepokea maombi 30,384 ya mikopo kutoka kwa vijana wa maeneo mbalimbali nchini.
Amesema baada ya kukamilika kwa tathmini ya maombi hayo, Serikali imeidhinisha utoaji wa Sh8 bilioni katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hiyo, inayolenga kuwawezesha vijana kuanzisha na kupanua shughuli za uzalishaji mali.
"Leo tunazindua rasmi utoaji wa mikopo hii, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuondoa vikwazo vinavyowakabili vijana katika kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali," amesema Nanauka.
Amesema uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa kuwawezesha vijana kujitegemea, kuzalisha ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika awamu hiyo, Mkoa wa Arusha umepokea Sh730 milioni kwa ajili ya miradi mitatu ya vijana. Kati ya fedha hizo, Sh500 milioni zimetengwa kwa mradi wa utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu, Sh130 milioni kwa kiwanda cha kuzalisha chaki zisizotoa vumbi, huku Sh100 milioni zikitolewa kwa vikundi vya Mama na Baba Lishe ili kuongeza uwezo wao wa uzalishaji na biashara.
Nanauka amesema maombi yaliyowasilishwa yanahusisha sekta mbalimbali zikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda vidogo, biashara, ubunifu, teknolojia na huduma, jambo linaloonyesha mahitaji makubwa ya mitaji kwa vijana wenye mawazo ya biashara na uzalishaji.
"Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa vijana wa Tanzania si wavivu kama ambavyo wakati mwingine imekuwa ikidaiwa, bali wanahitaji mazingira yanayowawezesha kuonyesha uwezo wao," amesema.
Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 34.5 ya Watanzania wana umri kati ya miaka 15 na 35, kundi ambalo lina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa uchumi iwapo litapata elimu, ujuzi, teknolojia, mitaji na mazingira rafiki ya kufanya biashara.
Aidha, amewataka wanufaika kutambua kuwa mikopo hiyo si zawadi, bali ni uwekezaji wa Serikali unaolenga kuongeza uzalishaji, kupanua biashara, kuanzisha viwanda vidogo na kuzalisha ajira.
"Mafanikio ya programu hii hayatapimwa kwa kiwango cha fedha kilichotolewa, bali kwa matokeo yatakayopatikana. Tunataka kuona biashara zenye tija, ongezeko la ajira, mapato ya wananchi na ukuaji wa kampuni zinazoendeshwa na vijana," amesema.
Amewasisitiza wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, kuimarisha usimamizi wa biashara, kutunza kumbukumbu na kurejesha mikopo kwa wakati ili vijana wengi zaidi wanufaike na programu hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Meru, Haika Mawalla amesema benki hiyo imejipanga kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji.
Amesema pamoja na kutoa mikopo, CRDB itaendelea kuwajengea vijana uwezo kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, uendeshaji wa biashara na matumizi sahihi ya mikopo.
"Tunaamini mchanganyiko wa mtaji, maarifa na nidhamu ya fedha ndiyo msingi wa mafanikio ya biashara na ujasiriamali endelevu. Tunawasihi vijana kuitumia fursa hii kwa ubunifu na uwajibikaji ili mikopo hii iwe chachu ya kuongeza uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi," amesema.
Ameongeza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha programu hiyo inawafikia vijana wengi zaidi na kuchangia ujenzi wa uchumi shindani unaoongozwa na vijana.