Nani anasema uongo?

Thursday November 11 2021
nani anasema uongopic
By Richard Mabala

Juzi niliota ndoto ya ajabu, sijui ni kwa sababu ya muvi niliyoiangalia na wanangu. Ilikuwa hadithi ya yule mtoto ambaye kila aliposema uongo, pua yake iliongezeka.

Baada ya hapo watoto wangu walikuwa wanacheka na kufurahi kupimana urefu wa pua zao. Hata pua za baba na mama na baada ya hapo walitoa hukumu kwamba lazima baba ni mwongo kuliko mama maana pua yake ilizidi kwa milimita mbili. Nilipojaribu kupima ya kwao, waligoma hivyo niliwatania.

“Mnaona sasa. Nyinyi ni waongo kuliko wote.”

Wakakana kabisa.

“Hapana baba, mimi sisemi uongo.”

“Hata mimi. Ni mwiko kabisa.”

Advertisement

Nikawasikilizaaa kisha nikawaambia waende kujiangalia kwenye kioo maana pua zao zimeongezeka sana. Haraka wakaanza kujigusagusa usoni ili waone kama ni kweli. Wacha nicheke.

“Oooooh! Kwamba mmejigusa inaonesha kwamba kweli mnasema uongo siku nyingine. Ndiyo maana Waswahili wanasema njia ya mwongo ni fupi.”

Watoto walishika kichwa kwa aibu ya kupatikana ingawa nilikuwa sina nia ya kuwagombeza tu na mimi mwenyewe sikuwa na uhakika kama ninaamini methali hii moja kwa moja. Maadili mazuri lakini katika hali halisi … Nikakumbuka maneno ya msaidizi wa Hitler, kwamba ukirudia uongo mara nyingi ya kutosha mwisho watu wataamini.

Basi labda kwa kuwa nilikuwa natafakari hayo nikaota. Nikaota niko ndani ya uwanja mkubwa kama vila wa mpira. Huko juu, kulikuwa na bango kubwa.

MASHINDANO YA PINOCCHIO

Katikati ya uwanja walikuwa wamesimama watu watatu, kila mmoja na jukwaa lake. Pembeni alikuwa amesimama mtu ambaye niliamini kwamba ni mshereheshaji. Alikuwa anarukaruka kwa furaha na kutangaza kwa madaha.

“Haya, haya, haya, ndugu watazamaji, sasa mnaona. Wamebaki watatu tu katika mashindano ya nani anaweza kusema uongo zaidi na kuaminika. Nitataja kila mmoja na mtashangilia. Kisha kila mmoja atapewa nafasi ya kujieleza ya dakika tano tu.

Mtu wa kwanzaaaaaaaaa: Mwanasiasaaaaa.

Vifijo na hoihoi kwa mlalahai.

Mtu wa piliiiiiiiiiiii: Mhubiriiiiiiiii au kwa majina mengine, askofu, nabii, mtumishi, mtume, na hata Mungu mwenyeweeeeeeee.

Vigelegele vikarindima wakati watu wakirukaruka kama ndama.

Na mtu wa tatuuuuuuu: Polisiiiiiiiiiiii.

Ghafla kukawa kimya. Nikafikiri labda watu waliogopa uongo wa polisi kuliko uongo wowote. Lakini nilifukuzilia mbali mawazo hayo. Watu wataogopaje mtu mwenye jukumu la kuwalinda si kuwalenga. Mshereheshaji aliendelea.

“Haya tumsikilize kwanza mwanasiasa.”

Mwanasiasa akasimama na kuwaangalia watu wote na kuwapungia mkono. Akatoa tabasamu pana lililoonesha mabaki ya nyama katikati ya meno yake, kisha akawaangalia washindani wake kwa dharau kubwa.

“Nani kama mimi? Nani kama mimi? Si tu naweza kwenda kwenye jimbo langu baada ya miaka mitano ya kutoonekana na kuwaongopea kirahiiiisiiii hadi wanichague tena. Naweza kutoa hotuba kwa hohehahe yenye ahadi za kijinga kabisa lakini watanipigia vigelegele. Au hapa nasema uongo jamani.”

Mshereheshaji akajibu.

“Hapana. Kwa mara ya kwanza umesema ukweli.”

Wacha kadamnasi wacheke na mwanasiasa akawapungia tena.

“Lakini haya ni mambo ya kitoto tu. Ukitaka kuwatawala watoto ujue kudanganya kitoto.”

Hapo niliona umati ulikasirika. Wako tayari kudanganywa kirahisi lakini kuitwa watoto hapana! Mwanasiasa aliendelea haraka.

“Nina maana kwamba, kama atakavyosema askofu hapa. Nyinyi wote ni watoto wangu, nawajali, nawapenda. Lakini nimebobea zaidi maana naweza kwenda kwenye mikutano ya kimataifa na kusema uongo mkavu kabisa. Tena wanajua nasema uongo, lakini ninavyoshupalia uongo ule kwa macho makubwa kabisa, wananywea na kukubali uongo wangu.

“Kwa mfano, hata kama tunawafukuza mabinti mama, naweza kusema kwamba si kweli, bali milango ya shule inawabana hivyo wameshindwa kuingia. Mimi ni mwongo wa kudanganya dunia nzima.”

Akapunga mikono tena, hadi watu walimshangilia.

Kisha akaingia nabii/askofu/mtume/mtumishi. Aliingia juu ya migongo ya watu kuonesha jinsi ambavyo uongo wake unakubalika hadi watu wanakubali kuwa watumwa kwake. Kisha alitubariki sisi sote, na wengi walipiga magoti kama vile kumsujudia pia. Kisha akaanza.

“Niseme nini zaidi? Ona wafuasi wangu. Naweza kuwaambia chochote wataamini. Juzi niliwaambia wakija na ufunguo wowote na kuutingisha wakati nawaombea, pamoja na kuweka sadaka ya kutosha, watapata gari. Na wasipopata nitawaambia kwamba imani yao haikutosha ndiyo maana hawakupata. Tena imani hupimwa kwa ukarimu wa sadaka.

“Naweza kusema kinyume kabisa cha maneno ya msahafu, wakati wanajua msahafu lakini bado wataniamini. Naweza kuwauzia maji ya bomba na kudai ni maji matakatifu na watanunua tu. Na zaidi ya yote, kwa kuwa mimi ni mwanamume rijali, naweza kuwarubuni wake za watu hadi waone kwamba kunipokea katika mapenzi ni kumpokea Roho Mtakatifu.

“Kisha hata wanasiasa wananiogopa eti wakinikamata kwa wizi na utapeli, watakuwa wameingilia imani za watu. Mungu awabariki wote kwa kuniunga mkono na uongo wangu mtakatifu.”

Watu wakapaza sauti.

“AAAAAAAAmeeeeen.”

Lakini, kwa mara nyingine, watu wakakaa kimya aliposimama yule polisi. Akanyanyua rungu lake kama vile kusalimia, lakini wote tukaona kwamba ni ya kutishia tu si ya kusalimia. Kisha akaanza kwa sauti kavu kabisa.

“Uongo bila rungu una nguvu gani? Bila rungu, mwanasiasa ataona uchungu. Bila risasi, muumini atalipa kisasi. Na wote wananiogopa mimi tu maana naweza kutunga mashtaka ya uongo wakati wowote na wapende wasipende watatii. Na watafichwa. Ndiyo maana hakuna atakayethubutu kunipinga mimi. Sina haja ya uongo mwingi, lakini uongo wangu ni komesha.”

Akamgeukia mwanasiasa na kumkunjia uso.

“Tena baada ya mkusanyiko huo, unatakiwa kituoni kujibu maswali kuhusu azma yako ya kuteketeza mbuga ya Serengeti ili uwakamate wanyama wanaokimbia na kuwachuna.”

Mwanasiasa alianza kutetemeka.

“Sio kweli afande ni uongo.”

“Sijali kama ni kweli au ni uongo. Mimi sipingiki.”

Akawageukia kadamnasi.

“Mnaona. Mbele ya uongo wangu, waongo ni udongo.”

Kukawa kimya. Hatimaye mshereheshaji akaweza kusimama.

“Haya mmewasikia. Lakini kipimo si maneno yao. Tuna mashine yetu hapa kinaitwa Pinocchiomita. Wote watatu mje hapa na kuweka mikono yenu kwenye tundu moja. Kadiri mlivyo wakubwa wa kusema uongo, pua zenu zitakua na kukua na kukua.”

Wote watatu wakaenda na kuweka mikono. Loooo! Pua zao zikaanza kurefuka sana hadi zikaanza kuwafukuza watazamaji. Wakasambaratika kila kikundi kikifukuzwa na pua mojawapo. Mshereheshaji akatangaza.

“Hakuna mshindi, hakuna mshindi. Wote waongo wa kubuhu. Lakini angalieni. Pua zao zitawashinda hadi wataanguka puani puuuuu!”

Nilianza kucheka. Uzito wa uongo utawasababisha kuanguka puani puuu!

Lakini ghafla nikasikia rungu la polisi.

“Unacheka nini? Unatakiwa kituo ….”

Jasho likaanza kunitoka huku nikishtuka. Kumbe vidole vya mama mtoto.

“We Bwana unaamka leo au …?” Huna kazi?”

Dah! Pua ikapoa. Lakini lini wataangukia pua na wao? Lini tutaweza kukanyaga pua zao?Advertisement