Nape azindua mwonekano mpya wa tovuti za MCL

Muktasari:

  • Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) imezindua mwonekano mpya wa tovuti zake za Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ambazo sasa zimekuja na njia rahisi kwa mtumiaji kuona habari mpya na zile za zamani anapoperuzi kwa kasi zaidi na matumizi kidogo ya intaneti (data) huku ikiwa na mwonekano mzuri wa matangazo.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amezindua mwonekano mpya wa tovuti za Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).

Nape amezindua mwonekano huo mpya unaokwenda sambamba na kaulimbiu ya “Mwonekano Mpya, Ulio na Ubora Zaidi (New Look, Better Experience)” leo Jumatano Februari 15, 2023 alipotembelea makao makuu ya ofisi hizo zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Nape ameipongeza Kampuni ya Mwananchi kwa ubunifu mkubwa waliokuja nao na kuzidi kuthibisha ubora wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (kulia) akimkaribisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipowasili makao makuu ya MCL jijini Dar es Salaam leo.

Kwa muda mrefu Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kupitia tovuti za Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti imekuwa ikihabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma ndani na nje ya mipaka.

Mhariri Mtendaji wa Maudhui ya Mtandao wa MCL, Zourha Malisa amesema kupitia mwonekano huo wasomaji na wadau watapata fursa ya kufurahia tovuti hizo mpya ambazo zimetengenezwa kuwapa urahisi wa kusoma kupitia simu janja, kompyuta mpakato au vishkwambi.

Amesema pamoja na mwonekano wa kuvutia na mpangilio mzuri, pia kutakuwa na ubora wa habari utakazokutana nazo kwenye tovuti hizi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu (wa tatu kulia) akimfafanulia jambo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (wa pili kushoto) alipotembelea makao makuu ya ofisi hizo zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam. Nape ni mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa mwonekano mpya wa tovuti za Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ambazo sasa zinapatikana kwa njia rahisi kwa mtumiaji kuona habari mpya. Picha na Edwin Mjwahuzi.

“Mwonekano mpya wa tovuti zetu unamrahisishia mtumiaji kuziona habari mpya na za zamani kwa urahisi tofauti na hapo awali. Pia, zinatoa fursa kwa makundi mbalimbali ya habari (Uchumi, Burudani, Siasa na safu mbalimbali) kuwa na mwonekano tofauti.

“Ni rahisi kutumia kwenye simu zenye kasi zaidi na matumizi kidogo ya intaneti (data), lakini pia kwa watangazaji kuna mwonekano mzuri wa matangazo unaompa mtumiaji wa tovuti urahisi wa kuona. Hali hii inarahisisha kwa mtumiaji kupata taarifa sahihi na kufanya maamuzi kwa urahisi. Tunafanya haya yote kwa lengo moja tu la kuliwezesha Taifa kama kaulimbiu yetu ya MCL inavyosema,” amesema Zourha.

Ili uweze kufurahia muonekano mpya wa tovuti zetu unachotakiwa kufanya ni kutembelea tovuti zetu za mwananchi.co.tz kwa upande wa Mwananchi, thecitizen.co.tz kwa upande wa The Citizen au mwanaspoti.co.tz kwa upande wa Mwanaspoti.