Nape: Mwananchi mmethibitisha ubora wenu

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameitaja Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuwa moja ya chombo bora cha habari katika ulimwengu wa sasa.

Dar es Salaam. Wakati Kampuni ya Mwananchi Communications Limited ikizindua mwonekano mpya wa tovuti zake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hilo linathibitisha ukubwa na ubora wa chombo hicho cha habari katika ulimwengu wa sasa.

Nnauye ameyasema hayo leo, Februari 15, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika ofisi za MCL, Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

“Kilichofanyika kinathibitisha kuwa Mwananchi ndiyo chombo bora na kinachoongoza katika taaluma ya habari kwenye ulimwengu wa sasa,” amesema.

Ameitaja hatua hiyo imechangia katika ndoto ya Serikali ya kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kuwafikia watu wengi.

Nnauye amesema takwimu zinaonyesha ongezeko la watumiaji wa Tehama nchini kufikia milioni 61 kati yao milioni 40 wanatumia simu kununua na kulipa bidhaa.

Sambamba na pongezi zake, Nnauye amesema Rais Samia Suluhu Hassan pia anafurahishwa na mchango wa Mwananchi katika kulifanya taifa liwe kitu kimoja.

“Kabla sifika hapa nilipomwambia Rais nakuja, alinituma nifikishe salamu zake kwamba anafurahishwa na mchango wa Mwananchi katika kulifanya taifa liwe kitu kimoja,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kuilinda kampuni hiyo.

Mhariri Mtendaji wa Maudhui Mtandaoni, Zourha Malisa amesema kwa miaka mingi Kampuni ya Mwananchi imekuwa ikichapisha habari zake katika mitandao mbalimbali ya kijamii, kuendana na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia.

"Lengo kubwa ni kuwafikia walaji wa maudhui kwa njia zote yaani magazeti na mitandao ya kijamii. Mwonekano huu utamsaidia msomaji kutumia kiwango kidogo cha data na watangazaji wa matangazo watawafikia watu wengi zaidi," amesema.

Mwonekano mpya wa tovuti hiyo, amesema unamshawishi msomaji kutumia muda mrefu kusoma taarifa mbalimbali na kupata anachokihitaji.

"Tumezingatia mwonekano utakaomfanya msomaji akae muda mrefu mtandaoni, lakini maudhui ndiyo hasa yanavutia," amesema.