NCAA yajipanga kuongeza watalii Ngorongoro

Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Elibariki Bajuta akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo.

ARUSHA. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamejipanga kuongeza idadi ya maeneo ya kupumzikia watalii wakati wa mapumziko ndani ya bonde la Ngorongoro na kuboresha barabara na shughuli za uhifadhi katika eneo la ukanda wote wa Ndutu ili kuweza kuongeza idadi kubwa ya watalii.

Hayo yamesemwa leo Juni Mosi jijini hapa na Naibu Kamishna wa uhifadhi NCAA, Elibariki Bajuta wakati akizungumza kwenye mkutano wa mamlaka hiyo na waongoza watalii mkoa wa Arusha.

Amesema lengo la kuongeza idadi ya maeneo hayo ni ili kuwezesha watalii kufika na kutembelea vivutio mbalimbali na kuweza kupumzika katika mazingira mazuri.

Aidha mbali na kuongeza idadi ya maeneo hayo pia wamejipanga kuongeza idadi kubwa ya faru katika eneo la bonde la hifadhi ya hiyo kwa lengo la kuongeza thamani ya bonde ambapo hadi kufikia Agosti mwaka huu watakuwa wameshafikisha idadi kubwa ya faru hao.

"Tunachoomba jamani ni kuwa na ushirikiano katika kuhakikisha kwa pamoja tunatunza mamlaka yetu pamoja na wanyama waliopo na pia naombeni sana mfuate sheria na taratibu zilizopo ndani ya hifadhi" amesema Bajuta

Aidha amewataka waongoza watalii hao kufuata sheria za mamlaka hizo zilizowekwa ndani ya hifadhi kwa kuzingatia muda wa kuingia hifadhini na kutoka kwa muda uliowekwa ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kutokea na kuwasababishia  wageni matatizo .

"Sisi lengo kubwa tunalotaka ni kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka haijalishi ni msimu wa watalii kuwa juu au  kuwa chini kikubwa tuwe  na lugha  nzuri kwa watalii wetu kwani namna tutakavyowahudumia ndivyo idadi itazidi kuongezeka  zaidi," amesema Bajuta.

Aidha amesema kumekuwepo na changamoto ya ongezeko la mimea vamizi katika hifadhi ya Ngorongoro ambapo amewataka wote kwa pamoja kushirikiana katika kuondoa mimea hiyo kwani ongezeko hilo linaongezeka kutokana na asili ya eneo hilo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Chama cha waongoza watalii Tanzania (TTGA), Robert Marks amesema chama hicho kina zaidi ya waongoza watalii 10,000 nchi nzima ambapo amesema kuwa uwepo wa kikao hicho utasaidia sana kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya mamlaka hiyo.



Marks amesema pamoja na kuwepo kwa mafanikio mbalimbali bado kuna changamoto ya miundombinu katika bonde la hifadhi ya Ngorongoro ambapo ameomba kufanyiwa ukarabati ili kurahisisha kuonekana kwa faru kwa urahisi katika eneo hilo.

Aidha wameomba kuwekwa kwa meza, viti na miamvuli katika eneo la kupumzikia watalii wakati wanapoenda kula ili kuondokana na changamoto ya wageni kupata majeraha kutoka kwa ndege.

Nao baadhi ya waongoza utalii wakieleza changamoto zao katika kikao hicho, wameomba kukarabatiwa kwa barabara katika kipindi hiki ambacho hakuna ubize mkubwa wa watalii kabla ya kipindi cha high season ili kuondokana na changamoto ya watalii kupata usumbufu kipindi cha wageni wengi