Nchagwa: Nilitupwa porini kukataa ukeketaji

Muktasari:

Mwaka 1998 Serikali ilipitisha sheria iliyofanya ukeketaji kwa wanawake kuwa kosa la jinai.

Mwaka 1998 Serikali ilipitisha sheria iliyofanya ukeketaji kwa wanawake kuwa kosa la jinai.

Mbali na hatua hiyo, jambo hilo limeendelea kuwapo huku baadhi ya jamii zikiamini kwamba kufanya hivyo ni sehemu ya kutekeleza mila na desturi.

Nchagwa Sensi (21) ni mmoja wa wasichana waliozaliwa na kukulia katika jamii yenye mila za ukeketaji, ambapo alilazimika kuishi mbali na familia yake kwa zaidi ya miaka minnne baada ya kufukuzwa nyumbani, akidaiwa kuwa ni mkosi kutokana na kubeba mimba akiwa bado hajakeketwa.

Kwa mujibu wa kabila la kama Wakurya, binti anapaswa kukeketwa kwanza ndipo abebe mimba.

Nchagwa alilazimika kuondolewa nyumbani kwao katika kijiji cha Genkuru wilayani Tarime na kutupwa katika pori moja wilayani Serengeti, baada ya familia yake kukubaliana kuwa ni lazima aondolewe nyumbani ili kuepusha mikosi ambayo ingeiandama familia hiyo.

Wakati anatupwa alikuwa na umri wa miaka 16 tu huku akiwa na mimba ya miezi minne, baada ya baba yake mzazi kufariki dunia katika mazingira ambayo anadai yanahusisha ushirikina kutokana na baba yake huyo kuwa kinyume na wana familia wengine.

“Baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017 babu yangu alimwambia baba kuwa nikeketwe ili niweze kuolewa, lakini baba alikataa ndipo yalipoanza malumbano ambapo wana ukoo wote akiwemo mama yangu mzazi walikuwa wakishinikiza nikeketwe lakini baba alikataa hivyo kuwepo na uhasama kati ya wana ukoo na baba yangu,” anasema Nchagwa.

Abakwa

Anasema baadaye msimu wa ukeketaji ulipoisha mwaka uliofuata baba yake alisafiri kwenda Mwanza ndipo siku moja alipokutana na kijana mmoja wa hapo kijijini kwao jioni alipokuwa akitoka kununua mahitaji ya nyumbani kwao na kijana huyo kumshika na kumbaka, na kwamba hata alipopeleka malalamiko kwa familia yake hakuna hatua zizilichokuliwa zaidi ya kumalizana na familia ya kijana huyo.

Anasema kuwa baada ya muda baba yake alirejea kutoka Mwanza ndipo ilipogundulika kuwa ana ujauzito na kwamba kikao cha ukoo kilikaa na kuagiza kuwa atoe mimba yake, ili akaketwe maagizo ambayo baba yake aliyakataa na kusema atamlea hadi atakapojifungua.

“Baada ya baba kuonyesha msimamo wake haikuchukua muda akaugua ghafla na kufariki dunia na siku ya kumaliza matanga babu alisema kuwa mtetezi wangu amefariki lazima nikeketwe la sivyo nitatupwa porini kwa sababu mimi ni mkosi,” anasimulia huku akitokwa machozi.

Anasema siku ambayo familia ilipanga kumuondoa usiku wake walikesha wakimfanyia madawa ya kienyeji ambayo hayajui yalikuwa ni ya nini na ilipofika alfajiri saa 11 waliondoka nyumbani na kuanza safari kuelekea porini.

Anasema saa 9 alasiri walifika porini na kumtoa kwenye gari na kumfunga miguu na mikono kwenye mti kisha kumuacha hapo bila msaada wowote ambapo alikaa kuanzia muda huo hadi kesho yake saa 12 jioni alipokuja kuokolewa na polisi pamoja na maafisa kutoka kituo cha Masanga kilichopo wilayani Tarime.

Anasema baada ya kuokolewa alianza maisha mapya katika kituo hicho hadi alipojifungua salama mtoto wake ambaye hivi sasa ana miaka mitatu na kwamba pamoja na tukio hilo, bado alitamani kurudi nyumbani kwao na kuishi na familia yao akidhani kuwa labda watakuwa wamebadili msimamo wao.

“Mwaka 2019 nilikwenda nyumbani nikijua kuwa nitapokelewa lakini badala yake mama alionyesha msimamo wa kutaka nikeketwe na walijaribu kunikamata lakini nilifanikiwa kutoroka na kukimbilia kituo cha polisi lakini mwaka jana pia nilijaribu kurudi nikakuta msimamo ni ule ule kwa hiyo kwa sasa nimeamua kuishi huku najihesabu kama sina wazazi,” anasema Nchagwa.

Anasema baada ya kujifungua alipata mafunzo ya ushonaji pamoja na kufuma masweta katika kituo cha Masanga na baadaye mwaka jana alitoka kituoni hapo kwa ajili ya kuanza kujitegemea, ambapo kituo hicho kilimlipia chumba cha kuishi kwa muda wa miezi sita sambamba na fedha kidogo kwa ajili ya mtaji.

Hivi sasa binti huyo anaishi kwa kufanya biashara ya kuuza ndizi mbivu shuleni pamoja na barabarani kufuatia kukosa mtaji wa kutosha kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ushonaji na ufumaji wa masweta.

Meneja mradi wa kupinga ukeketaji katika kituo cha Masanga wilayani Tarime, Valerian Mgani anasema Nchagwa ni mfano wa baadhi ya wasichana wadogo wilayani Tarime ambao wamekuwa wakipata kadhia mbalimbali kwa kisingizio cha mila hasa ya ukeketaji.

Anasema pamoja jitihada za wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ukeketaji, vitendo hivyo bado vinaendelea ambapo anatoa wito kwa jamii kuwa umefika muda sasa mila potofu ziachwe ili watoto wa kike wafurahie uhuru, utu na haki zao.

“Tangu kituo chetu kimeanza mwaka 2006 tumefikisha mahakamani zaidi ya kesi 30 za ukatili wa kijinsia zikuhusisha ukeketaji, vipigo, ndoa na mimba za utotoni na kesi nyingi tumeshinda huku watuhumiwa wakihukumiwa vifungo jela kulingana na sheria lakini niseme tu ukweli hali bado hairidhishi,” anasema Mgani.

Mwanasheria wa kituo cha Masanga, Dora Luhimbo anasema changamoto ya ukatili wa kijinsia bado ni kubwa katika eneo hilo na kwamba jitihada zaidi bado zinahitajika ili kutokomeza vitendo hivyo.

Dora anasema licha ya shirika lake kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji, bado wanakumbana na vikwazo ikiwemo sheria ambayo bado haijawapa meno ya kushughulikia vitendo ya ukeketaji kwa uhakika zaidi.


Anasema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya makosa ya kijinsia ya mwaka 1998 (Sospa) Sehemu ya 169 ili mtu atiwe hatiani kwa kosa la kukeketa ni lazima kuwepo na ushahidi usioacha shaka juu ya kufanya tendo hilo jambo ambalo limekuwa ni gumu kwa Wilaya ya Tarime kwani waathirika wengi wa ukeketaji wanashindwa kutoa ushahidi kuthibitisha aliyewakeketa, kutokana na sababu mbalimbali vikiwemo vitisho.

Mkuu wa dawati la jinsi katika Mkoa maalum wa kipolisi Tarime/Rorya, Cloud Mtweve anasema kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau katika kupambana na ukatili, tayari jamii imepata uelewa juu ya madhara ya ukatili hivyo wamekuwa wakitoa taarifa juu ya ukatili.

Hata hivyo Mtweve anasema bado kuna changamoto ya ushiriki wa jamii katika suala zima la ushahidi hivyo kupelekea kesi nyingi kuishia kwenye vituo vya polisi.