Nchi 40 kushiriki maonesho Kilifair

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Maonyesho hayo ya Kimataifa yatakayofanyika kuanzia Juni 7 hadi 9, mwaka huu, yatafanyika kwa mara ya tatu baada ya kusitishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la Uviko-19,yanategemea kuvutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na wanunuzi kutoka masoko ya kimataifa.
Arusha. Wanunuzi zaidi ya 600 wa Utalii kutoka nchi 40 duniani, wanatarajiwa kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair, yatakayofanyika jijini Arusha.
Maonesho hayo ambayo yatafanyika kwa mara ya tatu baada ya kusitishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la Uviko-19,yanategemea kuvutia washiriki kutoka Afrika Mashariki na wanunuaji kutoka masoko ya kimataifa.
Akizungumzia maandalizi ya maonesho hayo, leo Ijumaa Mei 24, 2024, Mkurugenzi wa kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo,ambao ndiyo waandaaji wa maonyesho hayo,amesema maonesho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Magereza,yamelenga kujenga na kukuza biashara ya utalii kimataifa kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Amesema maonesho ya mwaka huu waonyeshaji 468 kutoka nchi 37 watashiriki maonyesho hauo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 7 hadi 9, mwaka huu.
Amesema wadau hao na wanunuzi wa utalii watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ili wakawe mabalozi wa utalii kwenye nchi zao.
"Kutokana na ukuaji mkubwa wa sekta hii ,maonyesho haya yamelenga kuinua mazao mapya na kuuleta ulimwengu kwa pamoja kibiashara na
baadhi ya Mataifa hayo ambayo yatashiriki katika maonesho haya ni pamoja na Ujerumani,Afrika Kusini, Uingereza na Italia na nchi za Afrika Mashariki,"amesema Shoo
Shoo amesema mwaka huu onyesho hilo ni kubwa kuliko la mwaka jana, waonyeshaji wameongezeka na mwamko wa wanunuzi umekuwa na sekta hiyo inazidi kukua.
Mwakilishi wa wadau wa utalii kutoka hoteli ya Serena, Daniel Sambai, ameeleza ongezeko la wanunuzi kutoka nchi 34 mwaka jana hadi kufikia nchi 40 mwaka huu,kunaonyesha kuzidi kukua kwa sekta hiyo muhimu hapa nchini inayoongoza kwa kuchangia kwa asilimia kubwa fedha za kigeni katika pato la taifa hivyo ni muhimu wadau kuendelea kushirikiana na Serikali.
Naye Mkuu wa kitengo cha masoko na mauzo, kutoka kampuni ya Media Works, Noel Petro aliiomba Serikali kuruhusu ujenzi wa mabanda ya maonyesho ya kudumu, ili kuwepo kwa mazingira salama nyakati zote, badala ya kusubiri wakati wa maonesho tu.