Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nchi za EAC zakubaliana bonde la Ziwa Victoria kuwa kipaumbele

Baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye mkutano wa siku tano wa Baraza la Mawaziri wa Sekta kuhusu Bonde la Ziwa Victoria uliofanyika mjini Kisumu kuanzia Mei 12, 2025.

Muktasari:

  • Miji ya Mwanza, Bukoba, Musoma, Kampala na Kisumu zimeshudhudia visa vingi vya uchafuzi wa Ziwa Victoria vinavyopelekea mimea vamizi na kulihatarisha.

Kisumu. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kulipa kipaumbele Ziwa Victoria na bonde lake katika juhudi za uhifadhi na usimamizi wa mazingira, kufuatia ongezeko la uchafuzi ndani ya ziwa hilo linalohatarisha bioanuwai na mfumo mzima wa ikolojia ya bonde hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 17, 2025 baada ya kumalizika mkutano wa siku tano wa Baraza la Mawaziri wa Sekta kuhusu Bonde la Ziwa Victoria uliofanyika mjini Kisumu, Mawaziri na Makatibu Wakuu wakiongozwa na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame (ASALs) na Maendeleo ya Kanda, Beatrice Askul wamesisitiza kuwa jumuiya haipaswi kujikita pekee katika kupunguza uchafuzi wa rasilimali hiyo ya pamoja, bali pia kuhakikisha mchango wa kifedha unatumwa kwa wakati ili kuwezesha shughuli za Tume ya Bonde la Ziwa Victoria.

Viongozi hao pia, wamezitaka nchi zinazoshirikiana katika ziwa hilo kuacha kumwaga majitaka au uchafu kwenye ziwa, na badala yake kushirikiana kuandaa sera na kanuni zitakazosaidia kuongoza mienendo ya kila nchi mshirika katika kulilinda ziwa hilo, huku wakitaka uhifadhi wa bonde hilo usiishie kwenye Ziwa Victoria pekee, bali unapaswa pia kujumuisha maeneo yote ya vyanzo vya maji yanayoelekea katika ziwa hilo.

Katibu Mtendaji wa Bonde la Ziwa Victoria, Dk Masinde Bwire akizungumzia umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria na bonde lake.

Naye, Katibu Mtendaji wa Bonde la Ziwa Victoria, Dk Masinde Bwire amesema taasisi hiyo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inajizatiti kuhifadhi Ziwa Victoria kwa vile ni tegemeo kuu la mamilioni ya wanaoishi katika eneo hilo.

Amesema miji ya Mwanza, Bukoba, Musoma, Kampala na Kisumu zimeshudhudia visa vingi vya uchafuzi wa ziwa hilo vinavyopelekea mimea vamizi na kulihatarisha.

"Bonde linaendelea kukumbwa na shinikizo kubwa za kimazingira, ikiwa ni pamoja na ukataji miti ovyo, uvamizi wa maeneo oevu, uchafuzi wa mazingira kutokana na maji taka yasiyotibiwa, na matumizi yasiyoendelevu ya ardhi,”amesema Dk Bwire.

Amesema shinikizo hizo zimesababisha kupungua kwa ubora wa maji, kupotea kwa bioanuwai, na kuongezeka kwa hatari kutokana na mabadiliko ya tabianchi, huku majitaka ya viwandani, maji yanayotiririka kutoka kwenye mashamba, na taka za mijini vikiendelea kuchafua maji ya ziwa hilo.

“Hali hii haiaathiri tu mifumo ya ikolojia ya majini, bali pia inaleta hatari kubwa za kiafya kwa jamii zinazotegemea ziwa kwa ajili ya maji ya kunywa na riziki, mabadiliko yasiyotabirika ya mvua, mafuriko ya mara kwa mara, na vipindi virefu vya ukame vinaathiri uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula, na upatikanaji wa rasilimali za maji,”ameeleza

Nakuongeza kuwa,“Mabadiliko haya yanahitaji hatua za haraka na za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Changamoto hizi zimeonekana katika miji ya Kisumu, Siaya, na Busia katika Jamhuri ya Kenya; Musoma, Mwanza, na Bukoba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Kisenyi na Bwaise katika Kampala, Jamhuri ya Uganda,”


 Hatua za Bonde la Ziwa

Kupitia juhudi za pamoja za kikanda, Tume ya Bonde la Ziwa Vcktoria (LVBC) inahamasisha maendeleo endelevu na usimamizi wa rasilimali za asili za bonde hilo Ili kukabiliana na changamoto za usafi wa mazingira katika Bonde la Ziwa Viktoria.

Kupitia Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Maji (IWRM), ilipata ufadhili wa ziada wa Euro milioni 30 kutoka Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW Desemba, 2024.

Fedha hizo zitawezesha upanuzi wa Miradi ya Kipaumbele cha Juu (HPIs) katika miji ya Kampala, Kisumu, na Mwanza, zikilenga hatua za kupunguza mtiririko wa majitaka yasiyotibiwa kuelekea Ziwani.

Machi 26, mwaka huu tume na KfW walitia saini mikataba miwili ya utekelezaji ili kuanzisha rasmi matumizi ya ruzuku hiyo, na utekelezaji wa shughuli zinazohusiana utaanza katika mwaka huu wa fedha.