Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tani 441 za gugumaji zaopolewa Ziwa Victoria

Vijana wakitumia boti na tenga kuopoa gugumaji ndani ya Ziwa Victoria katika eneo la Kigongo-Busisi. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • January 2025 ilishuhudiwa ongezeko kubwa la gugumaji jipya (Salvinia spp) na kuanza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi, ufugaji samaki, vyombo vya usafiri hususani vivuko eneo la Kigongo-Busisi na kuzorotesha huduma ya usafiri kati ya Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine yanayozunguka Ziwa Victoria yanayotegemea vivuko hivyo.

Mwanza. Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeopoa  zaidi ya tani 441 za gugumaji aina ya Salvinia spp ndani ya Ziwa Victoria katika eneo la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza, kuanzia Mach 29 hadi Aprili 26, 2025 kwa kutumia mitumbwi na zana za kawaida.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alipotembelea eneo hilo kujionea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kudhibiti gugumaji hilo leo Jumatatu Aprili 28, 2025, Mkurugenzi wa bodi hiyo, Dk Renatus Shinhu amesema wameamua kutumia njia ya kawaida kulidhibiti wakati wakisubiri fedha za dharura kwaajili ya kununua mtambo wa kisasa utakaotumika kuyaondoa.

“Wakati tunaendelea kusubiri fedha za dharura kutoka Serikali kuu, Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imeendelea kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ueneaji wa gugumaji hili kwa njia za kawaida kwa kutumia mitumbwi na zana za kawaida kuopoa ili kupunguza athari za gugumaji hasa kwenye eneo la vivuko (Kigongo – Busisi),”amesema Dk Shinhu.

Amesema bodi hiyo pia imeanza ujenzi wa sehemu nne kwa ajili ya kuhifadhia gugumaji lililoopolewa kutoka ziwani ili kuzuia uchafuzi wa maji na udongo, ambapo kwa sasa tayari sehemu moja imejengwa katika eneo la Kigongo.

Amesema ili kulidhibiti,  Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza iliunda kikosi kazi kilichojumuisha watalaam kutoka ofisi hiyo, LVBWB, Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Vuatilifu Tanzania (TPHPA)  Kanda ya Ziwa, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Halmashauri za Misungwi na Sengerema, Wakala wa Huduma za Uhandisi wa Mitambo na Umeme (TAMESA), Asasi za Kiraia (Blue Victoria) naVikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs).

Amesema kikosi hicho baada ya kupitia taarifa mbalimbali za kitafiti pamoja na kujionea hali halisi ya maeneo yaliyoathiriwa kilibaini kuwa shughuli za Kibinadamu ndani ya bonde la ziwa Victoriaa kama vile Kilimo, ufugaji, Uvuvi na ufugaji samaki, Migodi, biashara, usafirishaji, ujenzi holela, utupaji ovyo wa takamaji na takangumu kutoka majumbani na viwandani, huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la virutubisho katika ziwa na kusababisha kushamiri na kuenea kwa gugu maji.

“Ilibainika kuwa mmea aina ya Savese swan, huzaliana kwa njia ya mbegu hivyo spores (mbegu) husambazwa na ndege. Tafiti zinaeleza kuwa mbegu pia huweza kubebwa kupitia vifaa vya usafiri, uvuvi au husambazwa na upepo kutoka eneo moja mpaka eneo jingine lenye maji. Vilevile vyakula au vifaranga vya samaki wakufugwa wanaosafirishwa kutoka eneo lililoathiriwa kwenda eneo lingine inaweza kubeba mbegu na kuzisambaza,”amesema

Ameongeza kuwa, “Kutokana na hali halisi, kiwango cha uzalianaji, madhara ambayo yameshajitokeza na ukubwa wa eneo lililovamiwa na gugumaji jipya, kikosi kazi kilipendekeza njia mbili zitumike katika kupambana na gugumaji jipya ambazo ni kuopoa kwa kutumia njia mbalimbali kama vile mitambo na mitumbwi pamoja na kutumia njia za kibiolojia yaani wadudu (Salvinia Weevil-Cyrtobagous salviniae),”

Amesema kikosi hicho kilishauri Serikali kutenga fedha ya dharura kwa ajili ya kununua aina bora ya mtambo wa kuopoa gugumaji, Wataalam kupata uzoefu kutoka kwenye nchi jirani zilizowahi kukumbwa na gugumaji hilo (Uganda, Sri Lanka, Zambia, South Africa, Senegal na Mauritania), kutafuta wadudu, kubainisha maeneo kwa ajili ya kuzalisha wadudu aina ya Salvinia weevil na namna ya kuzalisha nchini kwa ajili ya kukabiliana nalo.

Naye, Mtanda akazitaka taasisi zinazohusika moja kwa moja kudhibiti changamoto hiyo kufuata maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwemo kuleta meli itakayotumika kuopoa gugumaji hilo na kurahisisha kazi inayoendelea sasa ya kutumia boti.

“Bado ninatoa wito kwa Wizara ya Uvuvi kuzingatia maelekezo ya Waziri Mkuu lakini pia Wizara ya Ujenzi..najua mawaziri hawa wapo makini kabisa... Ninafrahi jitihada zinaendelea kuchukuliwa na hizi ni jitihada za muda mfupi lakini ili kufanya Ziwa Victoria liendelee kuwa safi lakini pia kuhakikisha ziwa halipungui upana wake ni lazima suala la usafishaji liendelee,”amesema Mtanda

Nakuongeza,“Namshukuru Waziri Mkuu kwa kuelekeza Wizara ya fedha kupitia hazina itoe Sh3.1 bilioni kwaajili ya kuimarisha huduma katika Ziwa Victoria. Madhara haya ya magugu ni mengi na makubwa sana..juzi tulikuwa Ukerewe tumeona kuna dalili za magugu haya kuanza kusogea maana yake yatasogea pia kwenye mradi wa vizimba vya samaki kwahiyo ndiomaana jitihada za makusudi zinachukuliwa na Serikali kufanya usafi Ziwa Victoria,”

Ameipongeza bodi hiyo kwa kufuata maelekezo ya Majaliwa na kueleza kuwa ana imani kuwa fedha hiyo iliyoombwa hazina ikifika, itatumika kununua mtambo bora wa kisasa utakaochakata gugumaji hilo.

Mmoja wa vijana wanaopoa gugumaji hilo, Said Juma amesema changamoto wanayokutana nayo ni kuharibika vitendea kazi kama vile mashine za boti na mitumbwi wakati wa kuyaopoa pamoja na kukutana na nyoka pamoja na mamba wanaotishia usalama wao.