Ndalichako: Ujumuishi wenye ulemavu Serikalini waimarika

Muktasari:

  • Profesa Ndalichako amesema Serikali inazingatia ujumuishi katika nafasi mbalimbali za uongozi ambapo watu wenye ulemavu wanajumuishwa nafasi hizo, pamoja na kwenye ajira zinazotolewa na Serikali.

Dar es Salaam. Hali ya ujumuishi katika uongozi imezidi kuimarika nchini ambapo watu wenye ulemavu wanashirikishwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo kwenye Baraza la Mawaziri, makatibu wakuu na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani.

Vilevile, Serikali imekidhi matakwa ya kisheria kwamba katika ajira zinazotolewa na Serikali, asilimia 3 ya wanaoajiriwa lazima wawe wenye ulemavu lakini Serikali imefikia asilimia 3.6, ikiwa ni zaidi ya matakwa ya kisheria.

Hayo yamebainishwa Desemba 5, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya Siku ya Ujumuishi ikiwa ni sehemu ya maadhamisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu inayoadhimishwa Desemba 3 kila mwaka.

Hafla hiyo ya Siku ya Ujumuishi imeandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania ikienda sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa 75 wa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) lililosainiwa mwaka 1948.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Profesa Ndalichako amesema Serikali inazingatia ujumuishi katika nafasi mbalimbali za uongozi ambapo watu wenye ulemavu wanajumuishwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi wa juu na pia kwenye ajira zinazotolewa na Serikali.

"Hali ya ujumuishi katika uongozi liko vizuri sana, ukiangalia kwenye Baraza la Mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa nafasi kwa wenye ulemavu, ukienda kwa makatibu wakuu wapo wenye ulemavu wa viungo, kwa mabalozi pia wapo na kwa wakurugenzi huko ndiyo wapo wengi," amesema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo amebainisha kwamba watu wenye ulemavu waliopewa dhamana hizo wanafanya kazi vizuri, hivyo ameitaka jamii kuacha unyanyapaa, badala yake wawape nafasi wenye ulemavu kwani wana akili na uwezo wa kufanya kama watu wengine wasio na ulemavu.

Amesisitiza kwamba katika ajira za Serikali, sheria inaelekeza asilimia 3 ya ajira zinatotangazwa ziende kwanwatu wenye ulemavu, nanwamekuwa wakitekeleza hilo na katika ajira zilizotolewa mwaka 2022/23, wameweza kufikia asilimia 3.6.

"Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu, wale wenye imani potofu za kunyanyapaa wenye ulemavu waache kufanya hivyo, ulemavu sio kutokuwa na uwezo, wana uwezo ingawa wanakumbana na vikwazo ndiyo maana tunahimiza ujummuishi ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili," amesema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuzingatia masuala ya ujumuishi, haki za binadamu na haki za wanawake kama nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

"Tunatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuleta ujumuishi na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na kutengeneza mazingira bora kwa watu wenye ulemavu," amesema Balozi Hajlaoui.