NDANI YA BOKSI: ...Gunia mbili za mkaa hadi risasi saba kisa ‘miskoli 42’

Picha ya Swalha Salum aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mmewe, Said Oswayo jijini Mwanza

Muktasari:

Dah! Yale ya Kigamboni na gunia mbili za mkaa yameibukia huko ‘Roku Site’. Pisi kali kiwango cha dunia, kakatishwa pumzi jumla bila chenji kwa risasi. Ni penzi! Yes! Hata kama hatukuwepo, stori kitaa ni kuwa penzi linazunguka tukio zima.

Dah! Yale ya Kigamboni na gunia mbili za mkaa yameibukia huko ‘Roku Site’. Pisi kali kiwango cha dunia, kakatishwa pumzi jumla bila chenji kwa risasi. Ni penzi! Yes! Hata kama hatukuwepo, stori kitaa ni kuwa penzi linazunguka tukio zima.

Kitaa ndoa nyingi zina migogoro kwa ‘ishu’ za kukurupuka. Kufanya papara bila kufahamiana vizuri. Kuna vitu vya msingi watu tunapaswa kufanya lakini tunavipuuza. Ujuaji mwingi na kuishi kimazoea au hisia za kipombe pombe tu.

Huwezi kuanzisha uhusiano bila kuwepo kwa upendo wa dhati. Watu wanaoa au kuolewa baada ya kukutana baa na kupendezwa na kampani tu. Yaani akili na matamanio ya tungi yakupe mume au mke wa kuanzisha familia? Hujachunguza tabia kama ana nidhamu, adabu, hasira, mlevi au kicheche. Bado hamjapeana muda wa kutosha, siyo tu kufahamiana bali hata kujua kama rangi ni yake ya asili au ya China.

Lazima muwe kitu kimoja kwanza kabla ya mwili mmoja. Jichanganyeni maeneo tofauti kama michezoni, baa, sinema na out ambazo zitakuwa uwanja mpana wa kutambua ‘interesti’ za kila mmoja.

Wajue ndugu zake, pata habari juu yao ambazo zitafanya ujue mwenzako yukoje. Kama ana mitabia mibovubovu mpotezee. ‘Ishu’ za eti unategemea atabadilika mbeleni ziliwaponza wengi. Abadilike mkiwa wachumba siyo ndani ya ndoa.

Kuna ‘majentromeni’ wenye upeo ule wa miaka ya tisini na wengi hupata shida sana ‘kusavaivu’ katika mapenzi ya leo kutokana na mabadiliko ya kitamaduni. Kwanza kuna unuhimu tupeane ujanja na miyeyusho ya dunia ya sasa. Dunia sasa inampa mwanamke ‘ova pawa’ hata akiwa kakosea. Malezi ya binti humfanya aamini kuwa kila kosa husababishwa na mwanaume. Chukua hiyo. Hii hupelekea binti wazingue makusudi wakijua jamii itasimama nao na hili litazame kwa jicho la tatu.

Atatetewa na jamii yote kuanzia sisi wanaume wenzako, wanawake pamoja na Serikali yaani hadi mifugo na wadudu ikibidi. Kifupi miaka ya sasa wanaume hatuna chetu, ingawa ukweli unauma, lakini huna jinsi zaidi ya kukubali ili uwe huru.

Ukiwa na misimamo yako binafsi bila kushirikisha yeyote imekula kwako kwani, dunia ya sasa hata ukipeleka kesi kwa wazee au mahakamani utaonekana mezingua. Yaani wife akitoa boko utaonekana tatizo ni wewe

Dunia iko na mwanamke na kidume utaambiwa humridhishi, humtunzi sijui, ama hauko romantiki. Mashitaka yote ni yako kama wewe ndio mkosaji. Wakati huo ‘waifu’ kazi yake ni kuongeza chumvi tu. Na wewe unabaki kama zuzu unatoa macho!

Kumbe ungerahisisha kwa kumfukuzia kwao bila hata kutaka vikao na wazazi. Sijui ushauri wa nani na nani, wale ndezi wanaojifanya wao wako ‘klini’. Achana na hekima za miaka ya tisini, utaishia kujizolea dhihaka, kebehi, aibu na soni kama hizi. Shituka mjomba.

Acha kujibebesha matatizo yasiyo kuhusu, kwa kudhani ndio uwanaume. Kuzaliwa kidume raha sana, tatizo letu kinachotuponza ni sifa za kibwege. Tuna viherehere vya kubeba matatizo yasiyo yetu ili tusifiwe tu. Sisi kiasili ni ‘mapedeshee’ toka tumboni mwa mama zetu.

Chukua kalamu na karatasi, anza kuandika shida zote zinazokusumbua halafu chambua shida zako binafsi. Hapo lazima asilimia 90 kwenda juu sio matatizo yako. Umebebelea matatizo ya wengine tu, kifupi tuna ujinga mwingi.

Fanya vitu unavyopenda, tunga sheria zako za kuendesha familia. Achana na akili za kitumwa kutaka kujua ‘totozi’ inataka au kupendelea nini. Ndio maana kila siku vijana wa kiume hufungua komeo za kuumizwa tu. Yote hii kutaka ‘kushea’ miamala na mwanamke.

Dunia ya sasa hata watoto wako wapo pamoja na ‘waifu’ weka akiba yako mwenyewe, hapa kuwa na ubinafsi kiasi. Kwa hili utanikumbuka siku ukiwa kwenye gofu lako peke yako. Na ‘waifu’ akiwa na watoto wamekutelekeza kiaina. Hii elimu huwezi kuipata popote zaidi ya hapa. Acha kujifanya dhaifu na mnyonge ukidhani utapendwa na kuheshimiwa. Kidume sio dhaifu kwa ‘totozi’ kama wengi wanavyofikiri. Tatizo tunapenda kuvaa udhaifu ili tuziridhishe nyoyo za ‘totozi’. Na huu ni mkwamo na wengi hawakubali kuwa ni mkwamo.

Watu siku hizi hawajali kabisa kuhusu maana ya kupendana, pita mtaani huko utasikia watoto wa kike wanalalamika kuwa, siku hizi hakuna penzi la kweli. Sasa unajiuliza kama siku hizi hakuna penzi la kweli, hilo penzi la zamani walilionea wapi?

Utagundua kuwa wanatoka na vibabu kwa mkavu bila aibu. Ndoa hazidumu siku hizi, kwa sababu moja kubwa sana, watu huzingatia tukio la harusi kuliko maisha ya ndoa baada ya harusi. Bila kujua ndoa inaenda mbali zaidi na kuna maisha ya ndoa na kuna tukio la harusi.

Wengi hupenda zaidi harusi na huwaza ndoa katika taswira ya suti kali, shela toka Thailand, mekapu ya bibi harusi kutoka Zee Masaki. ‘Time’ ya mashosti kuingia ukumbini na wimbo wa Zuchu, ‘Mwambieni’ ili kukomesha wanafiki na ma ex kuwaumiza wengine roho kumbe wapi.

Hawawazi mme au mke akiumwa miaka mitatu mfululizo utavumilia? Wakikosa mtoto kwa miaka mitano ya ndoa, watahimili shombo za ndugu wa mume? Mawifi na maneno ya kujaza choo cha kaka yao na huna kizazi? Hili wanawaza kweli?

Ndoa ni zaidi ya sherehe ya harusi baada ya yale matarumbeta kuzimika, usiku kifuatacho ni majukumu mazito na kiapo kisichovunjika. Acha mizuka ya Kwaito. Nenda mbali kidoogo. Uko tayari kuwa mme au mke wa mtu mmoja? Au unatamani kumkomesha shosti yako?

Mizuka ya ‘eksi’ utaweza kukwepa kweli wewe? Mnawaza hayo au mnawaza zawadi ya kamati kutoa ‘Harrier kalio la nyani’? Kabla ya kukubali kuishi na mtu jiulize, unataka ndoa kweli au unataka mizuka ya sherehe ya harusi? Ndoa siyo kuagiza ‘waini’ bar au kubeba ‘tishu’ na kwenda ‘toileti’.

Bahati mbaya familia zetu na jamii kwa ujumla huchangia yanayoendelea kwa sasa, hatuwaandai vijana wa kiume kuja kuwa vichwa vya familia. Hatuwaandai vijana wetu wa kike kuja kuwa walezi wa familia. Tunaandaa vijana wa kiume tegemezi na wasichana walevi na wapenda starehe.

Zamani vijana wa kiume walilelewa katika misingi ya kujiona baba na wale wa kike walilelewa kujiona wao ni kina mama. Ajabu sasa hivi watoto wa kiume wanajipamba kama mama zao na watoto wa kike nao wanalewa kama baba zao.

Watoto wa kiume hivi sasa hawaoni hatari kulelewa na wanawake. Pia wale wa kike wanaona ni sifa kuwalea vijana wa kiume na vibabu. Kwanini? Kwa sababu dunia inamtenga mtoto wa kiume ikimbeba zaidi mtoto wa kike na hili huhitaji maji ya upako kujua.

Kwanini watoto wa kike wanalindwa au kusimamiwa zaidi? Kwa sababu miaka mingi sana nyuma mpaka katika vitabu. Mtoto wa kike huchukuliwa kama vile ni chombo cha starehe kwa mwanaume. Sasa ni kama tunalipiza kisasi kwa kukomesha.

Kama jamii tukisimama na kuwalea watoto kwa usawa basi matukio meusi kama haya ya kuchomana moto na kupigana risasi kwa sababu ya penzi yatatoweka. Tatizo hata ‘kicheni pati’ za sasa hufundisha kukata nyonga zaidi kuliko kusonga ugali.

Malezi mabaya yanachangia kujaza roho nyeusi kwa watoto wetu na jamii isimamie malezi ya watoto wetu. Hili la risasi za Mwanza huko, chanzo ni ukosefu wa hofu ndani ya mioyo ya vijana wetu. Tunawaza sana utajiri kuliko maisha halisi.