Ndejembi aitaka Pura kuwaandaa Watanzania kunufaika na gesi asili
Waziri wa nishati Deogratius Ndejembi akizungumza na wajumbe wa kikao cha tano cha baraza la pili la wafanyakazi wa mamlaka ya udhibiti mkondo wa juu wa petroli PURA lilifanyika mkoani Morogoro leo Januari 26. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Watanzania wanapaswa kushirikishwa mapema ili wapate uhakika wa kutumia rasilimali yao ya asilia badala ya kuweka kipaumbele kwa kampuni za nje.
Morogoro. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) kuanza mapema kuwaandaa Watanzania kushiriki kikamilifu katika mradi wa gesi asilia kimiminika (LNG), ili wanufaike kabla ya wageni.
Akizungumza leo Februari 26, 2026 mjini Morogoro wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Pura, Ndejembi amesema rasilimali za mafuta na gesi ni mali ya taifa na zinapaswa kuwanufaisha wananchi kwanza. Amesisitiza maandalizi ya mapema ili kuepuka kisingizio cha ukosefu wa ujuzi.
Pia ameitaka Pura kuongeza kasi ya utafiti wa vitalu vipya vya mafuta na gesi ili kuvutia wawekezaji, na kufuatilia ucheleweshaji wa shughuli katika maeneo ya Tanga na Ruvuma.
Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni, amesema uchimbaji una gharama na hatari kubwa, akibainisha kuwa kati ya visima 96 vilivyochimbwa, 44 pekee vimetoa gesi. Ametaja changamoto ya kuchelewa kuidhinishwa kwa Mkataba wa Mfano wa Uzalishaji na Ugawanaji wa Mapato (MPSA) na baadhi ya kanuni muhimu.
Naye Katibu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, James Matarajio, ameitaka Pura kuongeza tafiti na kuandaa takwimu sahihi za maeneo mapya ili kuchochea uwekezaji.