Ndejembi amuonya mkandarasi wa mradi wa umeme Songea–Masasi
Muktasari:
- Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi unatekelezwa na kampuni ya Kalpataru Power ya India.
Songea. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Masasi kupitia Tunduru, akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi ili mradi huo ukamilike ndani ya muda uliopangwa.
Akikagua maendeleo ya mradi huo leo Jumatano, Julai 22, 2026, Ndejembi amesema Serikali haitavumilia ucheleweshaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi bila sababu za msingi.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele katika sekta ya nishati inayotekelezwa na Serikali, ikiwa na lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda wa kusini.
"Maendeleo ya mradi huu hayaridhishi ukilinganisha na muda uliopita tangu utekelezaji wake uanze. Serikali inatarajia kuona kasi kubwa zaidi ya utekelezaji katika kipindi kilichobaki. Nimemuagiza Katibu Mkuu kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo haya na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa iwapo hakutakuwa na maboresho yanayoonekana," amesema Waziri Ndejembi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya umeme kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Boniface Magiri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, amesema uongozi wa mkoa utaendelea kushirikiana na Serikali katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo hadi utakapokamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi unatekelezwa na kampuni ya Kalpataru Power ya India.
Ukikamilika, utaiunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Tunduru pamoja na maeneo ya jirani.