Nderemo na vifijo vyatawala ACT Wazalendo ikitimiza miaka 10

Wanachama na wafuasi wa ACT Wazalendo wakiwa wamekusanyika wakijadili hili na lile, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Picha na Juma Issihaka

Muktasari:

  • ACT-Wazalendo leo Mei 5, 2024 kinatimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.

Kigoma. Tarehe kama ya leo, miaka 10 iliyopita Chama cha ACT-Wazalendo kilizaliwa na sasa kinaadhimisha muongo mmoja wa kuzaliwa kwake.

Chama hicho kilianzishwa Mei 5, 2014. Umri wake hauakisi hadhi au kufanana na nguvu yake, kwani chama hicho ni sehemu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Si hivyo tu, kina wafuasi, mashabiki na wanachama wengi waliojitokeza kufanya shughuli mbalimbali kushajihisha sherehe za miaka 10 ya uzawa wa ACT-Wazalendo.

Mwananchi Digital imeshuhudia makundi ya wafuasi wa chama hicho waliokusanyika katika maeneo mbalimbali mkoani Kigoma kulikoandaliwa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya chama hicho.

Burudani za muziki wenye maudhui ya kusifu na kueleza wasifu wa chama hicho zilisikika, zikihusisha vikundi kadhaa vya washiriki wenye sare za ACT-Wazalendo.

Shangwe zilishuhudiwa zaidi katika ofisi za chama hicho Mkoa wa Kigoma, ambako idadi kubwa ya wafuasi wenye sare za chama hicho walikuwepo kuanza ratiba ya sherehe.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizo.

Kwa mujibu wa ratiba, sherehe itaanza kwa mapokezi ya Othman katika Uwanja wa Ndege Mkoa wa Kigoma na kufuatiwa na maandamano ambayo yataanza uwanjani hapo hadi ofisi za chama hicho za mkoa.

Pamoja na mambo mengine, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hizo, kisha kufuatiwa an maandamano kuelekea  uwanja wa Mwamiluaga mkoani humo ambako hotuba mbalimbali za viongozi zitatolewa.