Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndoa za kaburi zinavyowatesa wanawake na watoto Mara

Muktasari:

Baada ya Esther kukeketwa aliolewa, lakini wakadai wazazi wake walifaidi kupata mahari kubwa kwa binti ambaye ana ulemavu.

“Nimeishi na mume kwa zaidi ya miaka 14, tukazaa watoto saba wa kiume na mmoja akafariki dunia, lakini nikafichwa. Mwisho (mume wangu) akanikataa kuwa yeye si mume wangu, bali niliolewa na kaburi, yeye alitumika kunizalisha ili kuendeleza jina la marehemu ndugu yao.”

Ni kauli ya upole iliyochanganyika na kilio cha chini kutoka kwa Esther Itembe Marwa (45) mkazi wa Kitongoji cha Kyambahi Kata ya Uwanja wa ndege Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, ambaye inadaiwa aliolewa na kaburi.

Esther mwenye ulemavu wa mguu kwa uchungu anasema: “Sijui nilimkosea nini Mungu mimi, nimezaliwa kilema, sikupata elimu, nikakeketwa na kuozwa nikiwa na miaka 15, nimezaa watoto saba mwishoni mimi na wanangu tunakataliwa na huyo mwanaume, ninaambiwa mimi ni mke wa kaburi. Walioshiriki kunifanyia mateso haya dhambi itawatafuna.”

Machozi ya Esther yanatoka wakati dunia ikiwa katika siku 16 za kupinga ukatili wa mwanamke na mtoto na kaulimbiu ya kitaifa ikiwa ni “Funguka ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumuachi mtu salama, chukua hatua.”

Ilikuwaje?

Wakiwa wanaishi katika Kijiji cha Kyoruba Wilaya ya Tarime na wazazi wake mwaka 1986, Esther alikeketwa akiwa na umri wa miaka 14 na mwaka mmoja baadaye aliolewa na Samwel Wang’ete kwa mahari ya ng’ombe 15 kwa shangwe na vigelegele.

Ndoa hiyo ya kimila ilifurahiwa na wazazi ingawa Esther hakuwa anajua mambo ya ndoa kutokana na umri wake mdogo huku akiambiwa na wazazi kuwa ana bahati kijijini kupata mchumba ikiwa ni muda mfupi baada ya kukeketwa.

Sifa nyingi zilielekezwa kwa ngariba aliyewakeketa kwa madai kuwa ana mkono mzuri.

Baada ya Esther kukeketwa aliolewa, lakini wakadai wazazi wake walifaidi kupata mahari kubwa kwa binti ambaye ana ulemavu.

“Niliishi na Wang’ete nikijua ndiye mume wangu, ingawa hakuwa na mapenzi na watoto wetu maana hakuwapeleka shule, nikajua hizo ni tabia za jamii ya Kikurya. Wazazi wangu na wake wakahamia Kyambahi nasi tukahama,” anabainisha.

Siri hiyo ilifichwa na ukoo wake na huenda hata baba yake mzazi aliijua kuwa aliolewa na kaburi ili kuendeleza jina na familia ya Mniko Wang’ete ambaye ni ndugu wa Samwel, lakini wakati wa ndoa alijitokeza kama mume wake.

“Katika historia yao inaonyesha kaka yake Samweli, ambaye ni marehemu, alikufa kwa kung’atwa na nyoka akiwa shambani, alikuwa ameishatahiriwa lakini hajaoa na ndipo ukatengenezwa mkakati wa kumuolea mke ili jina lake lisipotee,” anasema Esther kwa masikitiko.

Mahari ya Esther iliyotolewa kwao ilitokana na dada yake na marehemu Mniko kuolewa, wazazi wake walizitumia fedha hizo kupeleka posa kwao na ndiyo maana wakawatoza ng’ombe wengi na kumweka Samwel mdogo wake kama ndiye anamuoa kumbe alikuwa ni kama ‘dume la mbegu’.

“Mwaka 2001 nikiwa nimeshazaa naye watoto saba alioa mke mwingine, nikiamini kuwa anaongeza mke wa pili, kumbe ndiyo alikuwa anaoa mke wake halisi, kwa kuwa mimi ni mke wa marehemu Mniko ambaye alikufa sijaolewa,” anabainisha.

Aambiwa ukweli

“Siku moja nikiwa nyumbani nahangaika kutafuta mahitaji ya watoto maana walikuwa hawahudumiwi, baba mkwe mdogo akaamua kuniambia ukweli kuwa kijana wao sasa ndiyo ameoa mke wake kwa kuwa mimi nimeolewa na kaburi, sikuamini kwa kuwa alikuwa amelewa,” anadai.

Hata hivyo, siku nyingine alirudia maneno yaleyale na alipomuuliza sababu za kumweleza alimwambia ukweli na kuwa walimficha ili kijana wao aliyekufa kabla hajao apate watoto na jina lisipotee. Alipomuuliza mwanaume aliyezaa naye alijibiwa kwa kipigo kikali kuwa asimfuate fuate yeye si mume wake.

“Niliumia sana na kuamua kwenda kwa baba yangu mzazi kutaka kujua sababu za kunioza kaburi, maana sasa kula na kila kitu nilihangaika mwenyewe ili kutunza watoto, kijana wangu mkubwa akalazimika kuacha shule akiwa darasa la nne kwa kukosa sare na mahitaji mengine,”anasema.

Anamwita shemeji

Anasema baada ya siri kubainika aliamua kumuona mume wake kama shemeji yake na wala hana wivu naye, kwa kuwa naye alishampa msimamo wake kuwa hana msaada kwake wala watoto kwa kuwa kazi yale kiukoo alishamaliza ya kufufua jina la ndugu yake.

Baba yake ajitetea

Itembe Marwa (79) kwa masikitiko anasema: “Binafsi sikujua kama naoza mwanangu kwa kaburi, nisingekubali ingawa ni mila na desturi zetu za Kikurya. Esther ni mlemavu najua shida zake, kumuoza na kaburi unampa mateso,” anabainisha.

Anasema siri hiyo aliambiwa na mwanaye na aliumia sana na kufuatilia kwa aliyedhani ni mkwe wake akasisitiza kuwa mume wake ni kaburi la Mniko.

“Niliamua kuchukua wajukuu wawili nimpunguzie mzigo, nikatoa na ng’ombe wa kumlimia chakula,” anasema Marwa.

Anadai pamoja na kuwa ni mila yao hasa kijana anapofariki dunia kabla hajaoa, lazima wamuolee ili jina lisipotee. Anasema binafsi anatamani mila hiyo ipigwe marufuku kwa kuwa inazalisha watoto watakaoishi kwenye mazingira magumu, inatesa mama na watoto wake hasa kwenye familia ambazo hazina kitu.

Baba mkwe achukiwa kwa kutoboa siri

Mwikwabe Mturi (77) mkazi wa Kitongoji cha Kyambahi ambaye ni baba mkwe mdogo wa Esther anasema hata naye alifichwa mwanzo kwa kuwa walikuwa wanaishi mbali na kaka yake ambaye ni baba mkwe wake na mwanamke huyo.

“Baada ya kuhamia kijijini hapo ndipo nikajua kuwa huyu mama ameolewa na kaburi, niliumia kwa kuwa niliona anavyonyanyasika, kwanza mlemavu na ana mzigo mkubwa wa watoto, nikaamua kumwambia…nilichukiwa sana na ndugu zangu kwanini nimetoboa siri hii,” anasema.

Anasema kama angekuwepo wakati wa maandalizi ya ndoa hiyo asingekubali kwa kuwa ana jua madhara yake, “tunadumisha mila kuwa jina la aliyefariki dunia lisipotee, lakini watoto hupata shida kwa kuwa hukosa mtu wa kuwasaidia, matokeo yake wanajihusisha na mambo ya ajabu kama ujambazi,” anabainisha.

Mama mkwe atoa ya moyoni

Mgosi Mwikwabe (62) ambaye ni mke wa Mwikwabe anadai kuwa, “sisi wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa ndoa kama hizi za kaburi, za mke kuoa mke mwenzake (Nyumbanthobu), mume wangu alipoamua kutoa siri walimchukia lakini mimi niliona amefanya vizuri kusema,”anadai.

Anasema kuwa ndoa hizo huwa na usiri mkubwa na mambo hujulikana iwapo kuna mgogoro ndani ya familia au kijana aliyekuwa amepewa jukumu la kuzalisha anapooa mke wake, mambo hubadilika, ingawa anakiri kuna maeneo hadi mwanamke anazeeka huwa hajui.

Kuhusu watoto

Anasema ingawa wanapozaliwa wanamjua baba yao, lakini hawatakiwi kutumia jina lake kama mzazi wao, watatumia la aliyefariki dunia ama babu yao, pamoja na kuwazaa hana mamlaka nao kwa kuwa mahari iliyotumika kuoa si yake hutolewa na wazazi wao.

“Kwa mila na desturi wenye kutoa mahari ndiyo wanasauti juu ya mwanamke huyo, kijana anatumika kuficha siri, ingawa mwisho wa siku anayebaki na maumivu ni mwanamke na watoto, hili linatakiwa kuangaliwa vizuri ili kupunguza ukatili kwa wanawake,” anabainisha Mgosi.

Kauli ya watoto

Emmanuel Wang’ete (22) kijana wa kwanza wa Esther anasema kuwa hakuwahi kujua kama huyo si baba yake.

“Wala sikujua kama sisi ni watoto wa marehemu Mniko Wang’ete ambaye alikufa mama hajaolewa, baada ya kufahamu hilo niliumia sana,” anasema kisha anatulia kwa muda.

Itaendelea kesho.