Ndugai: Zitto ananipa tabu

Muktasari:

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mbunge anayempa shida pale anapotaka kumwadhibu ni Zitto Kabwe


Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mbunge anayempa shida pale anapotaka kumwadhibu ni Zitto Kabwe.

Ndugai ametoa kauli yake hiyo leo Alhamisi Januari 17, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.

Ndugai amesema amekuwa akichelea kumfukuza bungeni mbunge huyo wa Kigoma Mjini kwa kuwa ndiye pekee anayewakilisha Chama cha ACT-Wazalendo.

"Unajua niseme ukweli, huyu mbunge amekuwa akinipa tabu sana, ananipa tabu sababu ndio mbunge mmoja wa chama chake,” amesema Ndugai.

“Hawa wengine huwa nafukuza sababu wenzao wapo, sasa huyu (Zitto) ni mmoja tu wa chama chake (ACT Wazalendo).”

Ndugai amtoa kauli alipokuwa akijibu swali la mwandishi aliyehoji kwa nini Bunge lisimchukulie hatua Zitto kama anadaiwa anapotosha ukweli kuhusu sakata la Profesa Assad kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.

Msingi wa kauli hiyo ulitokana na ufafanuzi wa Ndugai kuhusu nguvu ya Bunge kumuita CAG, akisema Zitto amekuwa akipotosha ukweli wa jambo hilo.

"Hii nchi ina mihimili mitatu, CAG ni ofisa wa Bunge tu, sasa tukichukua hatua bila kumhoji nyie (waandishi wa habari) mtaanza kulalamika tumechukua hatua, hatukumpatia nafasi ya kumsikiliza, " amesema Ndugai.