Ndugu ataja sababu kifo cha Dk Kamala

Waombolezaji kwenye msiba wa Dk Deosdarus Kamala wakimfariji mke wa marehemu, Adelaida Kamala (mwenye kofia ya kitenge), walipofika nyumbani kwake Mbweni Beach, Jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Dk Diodorus Kamala amefariki dunia jana, Februari 12, 2024 katika Hospitali ya Mzena alipokuwa akipatiwa matibabu.

Dar es Salaam. Maradhi ya tumbo yametajwa kusababisha kifo cha aliyewahi kuwa mbunge wa Nkenge na Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Diodorus Kamala.

Dk Kamala amefariki dunia jana, Februari 12, 2024 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Mzena alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumanne, Februari 13, 2024 nyumbani kwa marehemu Mbweni JKT ulipo msiba, kaka wa marehemu, Dk Francis Rwiza amesema ndugu yake huyo aliugua ghafla tumbo na kukimbizwa hospitali.

“Ilikuwa Ijumaa, ndugu yetu huyu alikuwa akilalamika kuumwa tumbo na kukimbizwa hospitali.

“Hata hivyo, madaktari wakiwa bado wanamfanyia uchunguzi kujua nini hasa kinachomsumbua, ndipo akakutwa na umauti siku ya jana,” amesema kaka huyo.

Akizungumza kuhusu ratiba ya mazishi, Dk Rwiza amesema mwili wa marehemu utaagwa Jumamosi, Februari 17, 2024 katika Kanisa Katoliki Mwenyeheri Isdory Bakanja, Parokia ya Boko.

Amesema mwili huo utasafirishwa Jumapili kuelekea kijijini kwao Bwanjai, Wilaya ya Nkenge na utazikwa Jumanne ijayo, Februari 20, 2024.

Dk Kamala aliyezaliwa Novemba 26, 1968, amewahi kuwa mbunge wa Nkenge (2000 hadi 2010) na mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki na baadaye waziri kamili wa wizara hiyo, mwaka 2008 hadi 2010

Mwaka 2011 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Uholanzi ambako alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2015 aliporejea kuwa mbunge hadi mwaka 2020.

Baadaye Kamala alirudi kufundisha Chuo cha Mzumbe, kazi aliyokuwa akiifanya kabla ya kuingia kwenye siasa. Mwanasiasa huyo ameacha mke na watoto wawili.