Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndugu wagomea kuzika mwili wa aliyedaiwa kuuawa kwa risasi

Lilian Nzota ambae ni mke wa marehemu Nicholaus Nzota akisimulia tukio la kuuwawa kwa mume wake kwa kupigwa risasi na mlinzi wa mashamba ya masista wa kanisa katoliki, wilayani Siha.

Muktasari:

  • Nicholaus Nzota alifariki Oktoba 1,2023 saa 12:15 jioni, baada ya kudaiwa kupigwa risasi na mlinzi wa mashamba ya Masista wa Kanisa Katoliki wilayani humo.

Siha. Zikiwa zimepita siku mbili tangu kutokea kwa tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi kwa mkazi wa kitongoji cha Kilari, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Nicholaus Nzota (35), familia ya marehemu huyo imesema haitazika mwili mpaka pale watakapopata muafaka.

Nicholaus Nzota alifariki Oktoba 1, 2023 saa 12:15 jioni, baada ya kudaiwa kupigwa risasi na mlinzi wa mashamba ya Masista wa Kanisa Katoliki wilayani humo.

Juzi Oktoba 1, 2023 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alinukuliwa na Mwananchi Digital akithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa Mlinzi anayedaiwa kuhusika na tukio hilo anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa na uchunguzi unaendelea.

Akizungumza leo oktoba 3, 2023, mdogo wa marehemu, John Nzota amesema kifo cha kaka yao kimewaumiza sana kama familia na sasa hawawezi kuzika mpaka watakapopata muafaka wa familia yake itakavyoachwa kwa kuwa ndiye alikuwa tegemeo.

"Hili tukio kama familia limetuumiza sana, tunafahamu limefanywa na mlinzi wa mashamba ya  Masista, hatuwezi kuzika mpaka tupate muafaka familia yake itaishije na marehemu atazikwaje, mpaka makubaliano yapatikane, ndipo tuzike, maana yeye ndiye alikuwa tegemezi na ameacha mke na watoto watatu ambao bado ni waadogo"amesema Nzota.

Aidha Nzota aliiomba serikali itazame kwa jicho la karibu watu wanaopewa silaha na kuhakikisha taratibu na sheria zinafuatwa ili kuepusha matukio ya mauaji yasiyo ya lazima.

"Ila naomba serikali iangalie hawa watu wanaopewa silaha, maana mtu analinda mashamba ambayo yanazungukwa na makazi ya watu na hakuna wanyama, anapewa silaha ya moto, maana tulifikiri eneo lile ni suala la walinzi kutembea na marungu na kama kutalazimika kuwepo na mwenye silaha za moto basi kuwepo na msimamizi na si kuachwa kila mlinzi kuzunguka na silaha bila usimamizi" 

Akisimulia tukio hilo Mke wa marehemu, Lilian Nicholaus amesema siku ya tukio ambayo ni jumapili, alishinda na mumewe kutwa nzima na hata jioni alipotoka alimzuia akimtaka asubiri kula lakini aliondoka na ndipo alipofikwa na umauti.

"Jumapili tulishinda na mume wangu vizuri, saa tisa nikatoka nikaenda kikundi na saa 12 kasoro hivi nilirudi  nikaenda kwenye kibanda cha biashara nikamuomba mume wangu aje anipasulie kuni na alifanya hivyo na  alipomaliza akaniambia anasikia njaa nikamwambia asubiri nimtengenezee chipsi akasema anataka awahi kwenda kunichukulia maziwa kwa sababu nateseka na moshi nisije nikapata TB, nikamwambia asiende asubiri, nilimzuia lakini aliondoka bila mimi kujua" amesema Liliani.

Ameongeza kuwa "Nikiwa hapa nikasikia yowe nikaondoka kukimbilia kujua tatizo lakini njiani nilizuiwa na kina mama wakanirudisha wakaniambia Mume wangu amefariki, jamani ameniacha na watoto watatu wadogo, mume wangu ameniacha na madeni, maana tulikopa tujenge nyumba  hii  ambayo hatujamaliza, ameondoka ameniacha" amesema mama huyo huku akiangua kilio.

"Nilikuwa napambana na mume wangu kutafuta maisha, leo ameniacha, inaniuma jamani,  naomba serikali inisaidie sina msaada kwa sasa, na toka tumeoana miaka 11 iliyopita sijawahi kuona amegombana na mtu, inaniuma sana, bora wangemvunja miguu, aje nikae nae nimuuguze kuliko kumuua na kuniacha na maumivu haya"

Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlangoni Ezekiel Mloli amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 1, 2023 saa 12:15 jioni katika eneo la mpakani na mashamba ya Masista, baada kutokea sintofahamu baina ya walinzi na wananchi waliofika kusaidia kina mama waliokuwa wameshikwa na walinzi hao.

Mwenyekiti huyo amesema tukio la Mlinzi huyo kumpiga risasi mwananchi si la kwanza, kwani miezi miwili iliyopita alimpiga kijana mmoja risasi ya mguu.

"Jumapili saa 12:15 nilipigiwa simu kuna mtu amepigwa risasi eneo la mpakani mwa mashamba ya Masista na nilipofika eneo la tukio nilikuta marehemu amepigwa risasi ya kichwani na kwenye bega na alikuwa ameshafariki hivyo nikatoa taarifa polisi na baadae walifika"

Akielezea tukio lilivyokuwa amesema "Kulikuwa na kinamama wanne ambao walikuwa wametoka kuokota kuni kwenye shamba jirani na walikuwa wakipita kwenye njia ambayo iko mpakani kabisa na Masista ndipo waliposimamishwa na Mlinzi huyo na akawa amemkamata mama mmoja akitaka kumuweka chini ya ulinzi na akawa anamvuta asiendelee kwenda abaki na katika ule mvutano baadae na wengine wakaja na walipoona kurupushani wakaamua kupiga yowe kuomba msaada"

"Walipopiga yowe kwa kuwa ni karibu na makazi ya watu, marehemu pamoja na kijana mwingine walifika eneo la tukio na walipouliza mlinzi huyo aliitisha bunduki kutoka kwa mlinzi mwingine na akapiga risasi moja juu na baadae akampiga marehemu".

Amesema ipo haja ya utaratibu wa matumizi ya silaha kutazamwa kwa upya kwa kuwa kwa mlinzi huyo hilo ni tukio la pili kumpiga mtu risasi ndani ya kipundi kifupi na mara ya nne kutishia watu na silaha hiyo jambo ambalo ni hatari.

"Katika eneo la Masista lina walinzi wengi, wapo wanaolinda Hospitali, wapo wanaolinda Chuo, wapo wanaolinda mashamba, wapo walinzi wa Shule ya sekondari na wapo walinzi wa maboma ya Ng'ombe, na tunawafahamu, lakini huyu mlinzi aliyefanya tukio hili ni mgeni na si tukio la kwanza kwani miezi miwili iliyopita alimpiga kijana mmoja risasi ya mguu na alikuwa akipitisha Ng'ombe njiani na tulijiridhisha Ng'ombe walipita njiani sasa baada ya miezi miwili, amepiga nwingine risasi na kumtoa uhai,".

Ameongeza kuwa "lakini ni mara ya nne kutumia silaha kusikozingatia utaratibu kwani kuna siku aligombana na mtu baa na alitoka akaenda kuchukua silaha akarudi kutishia nayo, sijui kama taratibu za kumuajiri na kukabidhiwa silaha zilifuatwa lakini tunaomba serikali ifanyie kazi hili".

Mwenyekiti huyo amesema "Hapa jirani kuna shirika lingine mlinzi alipiga mtu risasi na kumuua, lakini ukifuatilia unakuta kosa halifanani na nguvu iliyotumika, unakuta mnyana ameingia shambani, sheria zipo lakini unakuta wanaua mtu, tunaomba setikali iangalie jambo hili kwa jicho la karibu kwani huu ni mgogoro tayari umeingia kwenye kijiji"

"Lakini pia tungeomba mashirika haya yanyang'anywe silaha na taratibu za kumilikishwa silaha zianze upya  ili matukio kama haya yasijitokeze tena kwani kuna wakati yatachangia umwagaji damu za watu wasio na hatia na maafa makubwa zaidi".

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha Dk Christopher Timbuka amesema tayari wamefanya mkutano na wananchi na kesho watakutana na watawa hao wa Kanisa Katoliki ili kuweka mambo sawa na kuwezesha marehemu kuzikwa.

"Watawa wako tayari kushirikiana na familia, kesho nitakuwa na kikao na watawa, naamini mambo yatakuwa sawa na mwili utazikwa"