Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 214

Muktasari:

Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 214 katika mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne kwa hutuma za kufanya udanganyifu.

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 214 katika mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne kwa hutuma za kufanya udanganyifu.

Hayo yamebainishwa leo Jumamosa Januari 15, 2022 na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde wakati akitangaza matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne.

Dk Msonde amesema kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, watahiniwa 83 ni wa darasa la nne, watahiniwa 27 ni kidato cha pili, wengine 102 ni kidato cha nne na wawili ni wa mtihani wa maarifa (QT).

"Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 214 waliofanya udanganyifu katika mtihani kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) (i) na (j) Cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na cha 30(2)(b) cha kanuni za mitihani.

Dk Msonde amesema Baraza la Mitihani limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

"Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2022 kwa mujibu wa kifungu vha 32(1) cha kanuni za mitihani," amesema Dk Msonde.