Neema ya mafao kwa wenza wa Rais, Makamu, Waziri Mkuu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi akizungumza bungeni Jumatano Septemba 6, 2023. Picha na Merciful Munuo.

Dodoma. Serikali imepeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 4, 2023 ambayo ndani yake una marekebisho mapya ya mafao kwa ajili ya wenza wa viongozi wastaafu na waliokufa ambao ni Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Muswada huo uliowasilishwa kwa mara ya kwanza jana bungeni, na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameupeleka katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa ajili ya kuchambuliwa.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi, muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria 10 ikiwamo Sheria ya Stahili na Mafao ya Majaji, Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa Kisiasa, Sheria ya Utumishi wa Umma na Sheria ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Biashara Tanzania.

Muswada huo ambao ulitolewa kwa vyombo vya habari jana, unapendekeza kufuta na kufanya mabadiliko ya baadhi ya vifungu vya sheria inayohusu mafao na stahiki za Rais mstaafu, Makamu wa Rais mstaafu na Waziri Mkuu mstaafu na familia zao.


Mwenza wa Rais mstaafu

Muswada unapendekeza marekebisho kwa kuongeza stahiki za mwenza wa Rais mstaafu au aliyekufa, kifungu kinachopendekezwa kinasomeka “Kiongozi aliyeshika nafasi ya Ofisi ya Rais na kustaafu, mwenza wake atapata stahiki ya asilimia 25 ya jumla ya mshahara wa mwenza wake alipokuwa ofisini.”

Kifungu cha 11 (a) kimefutwa na kupendekezwa kingine kinachosomeka: “(a) familia ya Rais mstaafu itapata mafao kila mwezi ambayo ni sawa na asilimia 60 ya mshahara wa Rais aliye madarakani.


Mwenza wa makamu wa Rais

Kifungu kuhusu stahiki za mwenza wa makamu wa Rais kimefanyiwa marekebisho na kupendekezwa:

“Pale kiongozi aliyekuwa kwenye ofisi ya Makamu wa Rais anapokoma kushika nafasi hiyo mwenza wake atapata stahiki kiasi cha asilimia 25 ya jumla ya mshahara wa mwenza wake alipokuwa ofisini.”

Kifungu cha 13 kinapendekezwa marekebisho na mapendekezo ya kifungu kipya kuhusu stahiki za wategemezi wa makamu wa Rais kinasomeka:

“Pale makamu wa Rais anapofariki dunia au kukoma kushika madaraka, lakini kabla mafao yake hajapewa, mamlaka husika itatoa stahiki kwa wategemezi wake ya kiwango kinacholingana na mshahara aliokuwa akipokea alipokuwa ofisini.”


Makamu wa Rais anapokufa

Kifungu kilichopendekezwa kinasomeka: “(a) Wategemezi wake watapewa stahiki ya asilimia 40 ya mshahara wa makamu wa Rais.

Muswada huo pia umependekeza marekebisho ya sheria kwamba waziri mkuu mstaafu kwa kuongeza mapendekezo “Kiongozi aliyeshika ofisi ya Waziri Mkuu atakapokoma kuendelea na wadhifa huo, mwenza wake atapata stahiki ya asilimia 25 ya jumla ya mshahara aliokuwa akipokea mwenza wake alipokuwa ofisini.”

Mapendekezo mengine ni waziri mkuu mstaafu kupewa magari mawili badala ya gari moja, nyumba yenye samani ndani ya si chini ya vyumba vitatu vya kulala ambayo ni ‘self-contained’ na nyumba ndogo ya wahudumu.

Mapendekezo mengine ni kuwa na madereva wawili, mmoja wake na mwingine wa mwenza wake, walinzi na huduma zingine za ulinzi kwake na familia ya karibu.

Mapendekezo mengine ni huduma za matibabu ndani ya Tanzania au nje ya nchi baada ya kutolewa rufaa na Hospitali ya Taifa.


Ilivyo Kenya na Namibia

Nchini Namibia, sheria ya mafao na stahiki za marais wa zamani ya mwaka 2002, inatambua stahiki za wenza wao na watoto.

Sheria ya Namibia inatambua stahiki za watoto wa Rais mstaafu au aliyefariki dunia walio chini ya umri wa miaka 21.

Kwa mujibu wa sheria, mwenza na watoto watalipwa asilimia 75 ya mafao ya mwezi ya mwenza wake.

Pia, sheria inasema ikiwa mwenza ataolewa au kuoa, atakoma kupata stahiki hizo na watoto wakioa au kuolewa watakoma kuzipata.

Kwa upande wa Kenya, sheria ya mafao na stahiki za Rais mstaafu inatambua watoto walio chini ya umri wa miaka 18 au wenye umri wa miaka 24 lakini bado wanasoma vyuoni.

Namibia na Kenya sheria zimeweka wazi mafao na stahiki hazitatolewa kwa wanufaika wa kiongozi aliyeondolewa madarakani kwa jinai au tuhuma yeyote inayokwenda kinyume cha sheria za nchi.


Maendeleo ya biashara

Wakati huohuo, Dk Feleshi alisema muswada huo unafanya marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania.

Kifungu kipya cha 23A kinapendekezwa kuongezwa kwa kuweka masharti ya vibali vya kufanya maonyesho ya kibiashara na kuweka adhabu kwa mtu atakayefanya bila kibali.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana aliwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali 23 zinazotumika katika mfumo wa utoaji wa haki nchini, ikiwamo Sheria ya Ushahidi.

Marekebisho yanalenga kuwezesha ushahidi wa mtoto wa umri mdogo kupokewa bila kujali vigezo vilivyotolewa na sheria au sheria nyingine yoyote kuhusu kupokewa ushahidi huo.

Alisema hali hiyo imesababisha washitakiwa katika kesi nyingi, hususani za ukatili kwa watoto, kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa uthibitisho wa ahadi ya mtoto kusema ukweli au kutosema uongo.

Pendekezo jingine ni kufanya marekebisho katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kwa kifungu cha 131(2) ili kubainisha umri wa mtoto ni chini ya miaka 18.

Alisema lengo la marekebisho hayo ni kuwianisha umri wa mtoto katika sheria hiyo na umri wa mtoto katika sheria nyingine zinazohusu watoto.

Muswada unapendekeza kufanyika marekebisho kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga, kwa kifungu cha 29 kurekebishwa kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mali zinazohusika na kosa ambalo linaweza kutolewa dhamana kuwa Sh300 milioni.

“Lengo la marekebisho haya ni kuondoa mkanganyiko katika masharti yanayoweka viwango vya fedha katika dhamana zinazohusu mashauri ya uhujumu uchumi,” alisema.


Maoni ya wadau

Wakili wa kujitegemea, Elias Machibya alisema kuweka mafao kwa wenza wa viongozi wa juu wastaafu ni vizuri kwa sababu viongozi hao wamekuwa wakitumika pamoja na wenzao wao wanapokuwa madarakani.

Hata hivyo, alitaka pia Serikali kuboresha masilahi ya watumishi wengine ili waweze kupata stahiki zao.

Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ushahidi, Machibya alisema inaweza kusaidia katika upatikanaji wa haki wa mtoto. “Wabunge waaingalie vizuri sheria hii inaweza kutumika kuwabambikia kesi watu kwa sababu mtoto anaweza kufundishwa na kuleta shida katika mashauri,” alisema.

Takribani miezi 16 iliyopita mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete ambaye pia ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliiomba Serikali kutengeneza utaratibu au sheria kuwahakikishia stahiki zao wake na wenza wa viongozi wa juu, akiwemo Rais, baada ya wenza wao kuchaguliwa kushika nafasi hizo.