Bunge lapitisha marekebisho ya sheria za eneo la uwekezaji

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi akizungumza bungeni Jumatano Septemba 6, 2023. Picha na Merciful Munuo.

Muktasari:

  • Bunge limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu ambao unalenga kupeleka utekelezaji wa sheria mbili katika Wizara ya Uwekezaji na Mipango.

Dodoma. Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu wa mwaka 2023, unaolenga kuondoa mapungufu ya utekelezaji katika sheria mbili.

Sheria hizo ni ile ya Kanda Maalumu za Uwekezaji kwa ajili ya mauzo nje ya nchi, na Sheria ya Kanda Maalumu za Kiuchumi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 6, 2023 wakati akiwasilisha marekebisho ya sheria mbalimbali namba tatu za mwaka 2023.

Amesema lengo la kurekebisha sheria hizo ni kuhakikisha kuwa sheria husika zinatekelezwa na waziri mwenye dhamana na masuala husika, kwa mujibu wa hati ya mgawanyo wa majukumu ya mawaziri ambayo inatolewa na Rais.

Amesema kuwa kwa sasa sheria hizo zinamtafsiri waziri mwenye dhamana ni Waziri wa Viwanda ili hali jukumu la usimamizi wa masuala hayo limehamishiwa Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango.

“Hatua hii itaondoa ulazima wa kufanya marekebisho katika sheria kila inapotokea mabadiliko katika wizara,” amesema.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Kyombo, amesema kamati imeridhika na kwamba marekebisho yanayopendekezwa yatasaidia utekelezaji bora wa sheria zinazohusika.

“Kamati imekubaliana na mapendekezo ya muswada yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuwa yanalenga kuhakikisha  sheria zinazorekebishwa zinaendana na muundo wa majukumu, kulingana na hati idhini ya mgawanyo wa majukumu,” amesema.