Ndani ya hukumu ya mkataba wa bandari kati ya Tanzania, Dubai

Mbeya ilijimilikisha umakini wa Watanzania. Bila shaka hata mataifa mengine yalitega 'antena' zao katika Jiji la Kijani. Sakata la Mkataba wa Ushirikiano wa Bandari, baina ya Tanzania na Dubai, taswira yake ilielekezwa Mbeya.

Je, bandari za Tanzania zimeuzwa Dubai? Tanzania imekabidhi majukumu yote ya uendelezaji na uendeshaji wa bandari za bahari na maziwa kwa Dubai? Mamlaka ya nchi sasa yapo mikononi mwa Dubai? Haki ya ardhi na sheria zake vipoje? Dubai ina hadhi ipi kusaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiserikali (IGA) na Tanzania?

Hayo ni baadhi ya maswali yaliyoibuka tangu sakata la IGA ya Tanzania na Dubai kuhusu bandari lilipojitokeza kwenye uso wa jamii. Watanzania walishaogopa kwamba nchi yao inauzwa. Baadhi ya wanasheria, watu mashuhuri na viongozi wa kisiasa, tena wasomi, walizungumza kwa sauti kali. Hofu ilikuwa kubwa!

Wazalendo wanne, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus, walifungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, kupinga utekelezwaji wa mkataba.

Kwa nini wazalendo? Mwandishi bora wa Marekani Karne ya 20, Sydney Harris, kupitia kitabu chake “Pieces of Eight” – “Vipande nane”, alieleza vema tofauti ya mzalendo (patriot) na mzalendo (nationalist).

Patriot ni mzalendo mwenye hisia na nchi yake, anayebeba wajibu wa kuitetea anapoona mambo hayapo sawa. Nationalist ni mzalendo mwenye upofu, anaipenda nchi yake, mambo yapoharibika, hafanyi chochote.

Wazalendo wanne waliofungua kesi Mbeya ni patriots. Ama kwa kuona mkataba haupo sawa au kwa kuguswa na manung'uniko yaliyotanda nchi nzima, walikimbilia mahakamani kupata tafsiri ya kisheria.

Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza kuwa Mahakama ndio chombo cha utoaji haki. Wazalendo Lusako, Chengula, Ngonde na Nyalus, ni Watanzania wanaotambua wajibu wao wa kiraia.

Bandari zimeuzwa?

Julai 3, 2023, kesi ilifunguliwa. Kwa uzito wa kesi, Mahakama iliketi kwa mfumo wa jopo kamili (full bench). Majaji watatu, Dunstan Ndunguru, Mustafa Ismail na Abdi Kagomba, walisikiliza shauri hilo.

Mnyukano wa kisheria ukachukua nafasi kwa mawakili wa serikali, Mark Muluambo, Edson Mwaiyunge, Alice Mkulu, Stanley Kalokola na Edwin Lwebilo dhidi ya walioshitaki, Mpale Mpoki, Boniface Mwabukusi, Philip Mwakilima na Livino Ngalimitumba.

Agosti 10, 2023, majaji wote watatu walitoa hukumu ambayo ilitupilia mbali maombi ya kuubatilisha mkataba wa IGA, baina ya Tanzania na Dubai.

Hukumu ina kurasa 91. Kuanzia ukurasa wa 47, ndio majaji wanaanza kujikita kwenye uamuzi, baada ya uchambuzi kuhusu maeneo ambayo yalikuwa ya kibishaniwa baina ya wawasilisha maombi (walalamikaji) na wajibu maombi (Serikali).

Mambo sita yaliainishwa kama masuala yaliyokuwa yakibishaniwa. Mosi, kama IGA baina ya Tanzania na Dubai inakinzana na vifungu vya Sheria ya Tanzania ya Mamlaka ya Maliasili na Rasilimali (Sheria namba 5, 2017).

Pili, kama umma ulijulishwa na kupewa muda wa kutosha kutoa maoni. Tatu, kama ibara za mkataba wa IGA zinakinzana na Katiba ya Tanzania. Nne, je, IGA ni mkataba?

Tano, kama ibara ya pili na 23 ya IGA zinakinzana na kifungu cha 25 cha Sheria ya Mikataba (LCA). Sita, kama IGA kati ya Tanzania na Dubai, ilifuata mchakato wa kisheria unaoelekezwa katika kifungu cha 64 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA Act).

Majaji wanaanza na ufafanuzi kuhusu mkataba kwa tafsiri iliyopo kwenye kifungu cha 10, Sheria ya Mikataba (LCA), inayosema: “Makubaliano yote ni mikataba kama yamefanywa kwa hiari na pande zenye uhalali wa kusaini, kwa mazingatio ya kisheria na kama hayavunji sheria.”

Mahakama inatambua tafsiri ya mazingatio ya kisheria kwenye mkataba kuwa ni ahadi za kila upande, kama ilivyoandikwa kwenye jarida la kisheria la Sutton and Shannon, Januari Mosi, 1937. Vilevile, inafahamu kuwa kifungu cha 25 cha LCA, kinasema mikataba isiyo na mazingatio ya kisheria haifai tangu mwanzo.

Wawasilisha maombi walitaka Mahakama itamke IGA baina ya Tanzania na Dubai ni batili kwa sababu haikukidhi mazingatio ya kisheria. Hata hivyo, majaji wameeleza kuwa IGA haifungwi na LCA.

Majaji wamekubaliana na mawakili wa wajibu maombi kuwa IGA baina ya Tanzania na Dubai ni mfumo wa kisheria wa makubaliano ambao umeweka misingi ya maeneo ya ushirikiano.

Hili ni swali lililotokana kuenea kwa sehemu kubwa uvumi kuwa bandari zote za bahari na maziwa zimeuzwa kwa kampuni ya Dubai ya DP World.

Wawasilisha maombi walilalamika mahakamani kuwa kupitia IGA baina ya Tanzania na Dubai, bandari, sehemu maalumu za kiuchumi, maegesho ya logistics na korido za biashara, ni maeneo yaliyo kwenye orodha ya kutwaliwa na DP World.

Hoja ya wawasilisha maombi ni kuwa DP World inatwaa maeneo yote hayo Tanzania, pasipo kuonesha na yenyewe inatoa nini. Hapo ndipo wanaona kunakosekana mazingatio ya kisheria kwenye mkataba.

Majaji wameeleza kuwa hoja hiyo ya walalamikaji ni potofu na haijawashawishi. Wamefafanua kuwa maeneo yaliyoorodheshwa yameainishwa kuwa maeneo ya ushirikiano, sio kweli kuwa yametwaliwa na DP World.

Uhalali wa IGA

Wawasilisha maombi walitoa hoja kuwa IGA ni batili kwa vile Dubai haina hadhi ya kufanya makubaliano ya kimataifa. Walibainisha kuwa IGA ya Tanzania na Dubai imekiuka ibara ya 120 ya Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu, mikataba ya kimataifa ya Montevideo na Vienna.

Mtazamo wa mawakili wa wawasilisha maombi ni kuwa Dubai ipo ndani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na masuala ya ushirikiano wa kimataifa, yanatakiwa kufanywa na UAE.

Majaji wanakubaliana na hoja ya wakili Kalokola kuhusu ibara ya 116 ya UAE, inayoelekeza falme kuwa huru kutekeleza mambo ambayo hayatekelezwi na UAE. Biashara na uwekezaji sio masuala ya muungano UAE. Majaji wameona Dubai walikuwa na uhalali kusaini IGA na Tanzania.

Kingine, majaji wamebainisha kuwa masuala ya biashara na uwekezaji yaliyomo kwenye IGA, hayaingilii sera ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, ambavyo ndivyo hasa vinashughulikiwa na UAE upande wa muungano.

Zaidi, Mahakama imesema kuwa mawakili upande wa wawasilisha maombi, walishindwa kuthibitisha kuwa IGA inaingilia mambo ya muungano UAE na hawakuweza kuthibitisha kama Dubai hawakuwa na uhalali wa kusaini IGA.

Je, IGA inakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA), kifungu cha 64? Majaji wamesema kuwa wawasilisha maombi walijiweka mbali mno na hali halisi kuhusu sheria za kimataifa. Kwamba PPA haiwezi kufanya kazi mbele ya IGA.

Majaji wamekubaliana na mawakili wa utetezi, waliojenga hoja kupitia kifungu cha 4 (1) cha PPA, kinachoelekeza kuwa Tanzania inapoingia mkataba au makubaliano ya kimataifa, mkataba husika ndio utatumika, isipokuwa kwenye manunuzi.

Majaji wanafafanua kuwa sharti la manunuzi lililopo kifungu cha 64 cha PPA, halina msingi kwani kwenye IGA hakuna manunuzi. IGA sio aina ya makubaliano yenye kushughulika na masuala madogo ya manunuzi.

Wameeleza kuwa manunuzi ni mambo ambayo yatakuwemo kwenye mikataba ya utekelezaji (HGA) au makubaliano ya miradi ambayo yanangoja majadiliano na makubaliano baina ya DP World na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Ushiriki wa wananchi kutoa maoni ulikuwa mdogo kwa sababu muda ulikuwa finyu. Majaji wamekubaliana na hoja za wawasilisha maombi kuhusu muda, ila wanaamini njia ya kidijitali ingetumika vizuri, ingeongeza ushiriki.

Zaidi, majaji wamebainisha kuwa dirisha la utoaji maoni ni utaratibu wa Bunge, na Mahakama haiwezi kuingilia. Pamoja na ushiriki mdogo wa wananchi, majaji wameona hoja ya ufinyu wa muda uliotolewa kwa ajili ya maoni, haitoshi kubatilisha IGA.