Kicheko kwa wasafirishaji wa Tanzania, Dubai ikiletwa ndege ya mizigo

Muktasari:
- Kampuni ya Xerin Group imeanzisha safari za ndege aina ya B737-800 freighter yenye uwezo wa kubeba hadi tani 20, kwa kuanza safari itakuwa ni moja kwa wiki.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Tanzania sasa wana sababu ya kutabasamu kufuatia uzinduzi wa ndege mpya maalumu ya mizigo inayounganisha Dar es Salaam na Dubai, hatua kubwa katika sekta ya usafirishaji wa anga na biashara nchini.
Huduma hii mpya ya mizigo kwa njia ya anga, inayoendeshwa na kampuni ya Tanzania ya Xerin Group Limited, itatumia ndege aina ya B737-800 freighter yenye uwezo wa kubeba hadi tani 20 kwa safari moja.
Safari itakuwa ikifanyika kwa wiki mara moja katika siku za mwanzoni, ikiondoka Dubai kila Jumatano asubuhi na kutua Dar es Salaam saa 9:00 alasiri, kisha kurudi saa 10:30 jioni.
Wakati wa uzinduzi wa safari hiyo uliofanyika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam jana Julai 2, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa Xerin Group, Hussein Jamal amesema pamoja na kuwa kampuni hiyo itaanza na safari moja kwa wiki lakini kuna uwezekano wa kuongeza zaidi kulingana na mahitaji yatakayokuwepo.
Kwa miaka mingi, wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale wa kati na wadogo wamekuwa wakitegemea ndege za abiria au njia za baharini zinazochukua muda mrefu zenye gharama kubwa kuagiza bidhaa kutoka Dubai, jiji linalojulikana duniani kwa mazingira rafiki ya biashara na masoko ya jumla.
“Tunaanza na safari moja kwa wiki lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza kulingana na mahitaji lakini pia tunafikiria kuanza safari katika mataifa ya Qatar, Saudi Arabia, Oman na Bahrain ,” amesema Jamal.
Jamali amesema masoko mengine yanayoangaziwa ni Afrika Mashariki na kati huku akisisitiza kuwa huduma hii mpya si tu itarahisishwa usafirishaji kati ya Tanzania na nchi za Ghuba ya Kiarabu bali ni kuwezesha wafanyabiashara wa pande zote mbili.
“Tumewasikiliza wafanyabiashara wadogo na wa kati, wazalishaji na wauzaji kutoka Tanzania na UAE. Ujumbe mmoja umekuwa wazi ambao ni hitaji la suluhisho maalum, la wakati na la kuaminika la mizigo,” alisema. “Huu ni uamuzi wa kijasiri kufungua fursa za kibiashara zilizokuwa zikikwamishwa na changamoto za usafirishaji.”
Takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha biashara kati ya Tanzania na UAE imekuwa ikikua kwa kasi, ambapo thamani ya biashara ya pande mbili ilivuka dola bilioni 2.3 (Sh6.6 Trilioni) mwaka 2023.
Kwa upande wake Mamlaka ya Viwanja vya ndege nchini (TAA) imeeleza kuwa safari hizo zilikuwa zikihitajika kwani wafanyabiashara nchini wamekuwa wakipata ugumu wa kusafirisha bidhaa zinazoharibika haraka.
Kwa upande wake mchambuzi wa uchumi Dk Edwin Mrema anasema kwa kuwa na safari ya moja kwa moja katika ya Falme za Kiarabu na Tanzania thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili itaongezeka zaidi.