Mbunge ataka nyongeza kiwango mafao ya wastaafu

Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi wakati akijibu maswali ya wabunge leo.

Muktasari:

  • Serikali imesema inafanya tathimini ya mifuko kwa ajili ya kuongeza kiwango Cha malipo ya mafao kwa kufuata kanuni za.ulioaji mafao.

Dodoma. Serikali imeeleza vipindi vinavyotumika kwa ajili ya kufanya tathimi ya kiuchumi katika kuboresha mafao ya watumishi.

Vipindi vya tathimini ni miaka miwili, mitano na kipindi kirefu ni miaka 10 lakini wakasema kwa tathimini ya maboresho ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2018.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Ijumaa Septemba Mosi, 2023 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Nancy Nyalusi.

Mbunge huyo ametaka kujua ni lini Serikali itaboresha mafao ya wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata mstaafu kwa mwezi.

Naibu Waziri amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu wake na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake.

"Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na tathmini ya kipindi kirefu ni miaka kumi," amesema Katambi.

Kwa mujibu wa Katambi, Kanuni za ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018 zilielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa mfuko kila baada ya miaka mitatu (3).

Amesema hadi sasa wastaafu wote wa Serikali walishaboreshewa pensheni zao za kila mwezi ambapo kiwango cha chini ni Sh100,000 na kuendelea tofauti na hapo awali.