Neema yaja kwa wakulima tangawizi Same

Muktasari:

  • Tani 44 za zao la Tangawizi zitakuwa zikisafirishwa kila wiki kutoka nchini hadi kwenye masoko ya kimataifa kupitia kampuni ya Akida Group Export Company Ltd hatua itakayowanufaisha wakulima wa zao hilo wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine nchini.


Arumeru. Tani 44 za zao la Tangawizi zitakuwa zikisafirishwa kila wiki kutoka nchini hadi kwenye masoko ya kimataifa kupitia kampuni ya Akida Group Export Company Ltd hatua itakayowanufaisha wakulima wa zao hilo wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine nchini.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa mkombozi kwa wakulima wa zao hilo ambao wamekua hawanufaiki na bei ya soko la ndani kuwa chini ukilinganisha na masoko ya kimataifa ambayo bei hutegemea mahitaji ya soko na kununuliwa kwa bei inayowanufaisha wakulima.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Tanzania Horticultural Association (Taha), Jaquelline Mkindi amesema hayo katika kituo cha huduma kwa wakulima eneo la Tengeru kilichofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wakati wa kuandaa zao hilo kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

“Tumekua tukiwahamasisha wakulima kujikita kwenye kilimo biashara ambacho kina tija kubwa na kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo kupitia wataalamu, hii ni hatua muhimu kwa wakulima wa zao la tangawizi eneo la Miamba Miamba wilaya ya Same kuchangamkia fursa ya soko la kimataifa,”alisema Mkindi


Kupitia fursa ya soko la tangawizi nchini Ukraine imewawezesha kutoa ajira kwa wafanyakazi 250 wanawake na vijana ambao wanandaa zao hilo katika hatua za awali hadi kulifungasha kabla ya kusafirishwa kwenye soko la nje hatua itakayowapa manufaa ya kiuchumi ya kuendeleza jamii zao.

Meneja wa Kituo cha Huduma kwa Wakulima kilichopo Tengeru, Joseph Mwita alisema upatikanaji wa soko la uhakika wa zao la tangawizi unatokana na jitihada za taasisi ya Taha inayojihusisha kuhamasisha kilimo cha maua, mbogamboga, matunda na viungo kutafuta masoko sehemu mbalimbali duniani.

Amesema kiasi cha tani saba kitakua kikipokelewa kwaajili ya kuandaliwa na baada ya kuzipanga kwenye madaraja kiasi cha tani tano ndicho kitafungashwa kwaajili ya masoko ya nje huku kinachobaki kitatumika kwenye soko la ndani.

Mmoja wa wafanyakazi waliopata ajira katika kituo hicho, Rahma Maulid amesema itamsaidia kupata kipato cha kumwezesha kuitunza familia yake vizuri na kuomba kampuni hiyo iwe endelevu ili kuwasaidia wanawake na vijana kuitumikia kampuni hiyo.