Ng’ombe 5,000 wafa kwa ukame Mwanga
Muktasari:
Zaidi ya ng’ombe 5,000 wamekufa katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kutokana na kukosekana kwa maji na malisho hali iliyosababishwa na ukame ambao umekumba baadhi ya maeneo mengi hapa nchini.
Mwanga. Zaidi ya ng’ombe 5,000 wamekufa katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kutokana na kukosekana kwa maji na malisho hali iliyosababishwa na ukame ambao umekumba baadhi ya maeneo mengi hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya ofisa mifugo Wilaya ya Mwanga, Bwai Bayo amesema mpaka sasa zaidi ya ng'ombe 5000 wamekufa katika wilaya hiyo kutokana na ukame uliopo kwa sasa huku akiwashauri wafugaji hao kuuza mifugo wanapoelekea kipindi cha kiangazi ili kuepuka kupata hasara wakati ukame.
"Hatua tuliyochukua kutokana na hali ya hewa ilivyo tumeshauri wafugaji angalau wapunguze mifugo kwa kipindi hiki kwasababu ya hali ya hewa maana huu mwaka umekuwa wa tofauti na miaka mingine ambapo mwaka huu njaa ya maji na malisho kwa mifugo imekuwa ni kubwa na hii ndio sababu kubwa ambayo imepelekea wafugaji kupoteza mifugo yao ,"amesema na kuongeza
"Hapa Wilaya ya Mwanga zaidi ya ng'ombe 5000 wamekufa kwasababu ya ukame, tutazidi kuwashauri wafugaji hasa kipindi cha masikia kinapoisha kuelekea kiangazi waweze kupunguza mifugo yao ili wasikutane na madhara makubwa kama haya,"alisema Bayo
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo ambayo yameathirika na ukame huo katika wilaya za Mwanga na Same, Mwenyekiti wa chama cha wafugaji nchini, Jeremiah Wambura amesema atamuandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuona ni namna gani hatua za haraka zinachukuliwa ili kuokoa mifugo hiyo.
"Jumatatu nitamuandikia barua Waziri Mkuu kumweleza hali ilivyo, lazima tuchukue hatua za haraka kuokoa mifugo, nimeambiwa ng'ombe takribani 900 wamekufa kwenye eneo moja tuu hapa kijiji cha Pangaroo na katika hii Wilaya ng'ombe zaidi ya 5,000 wamekufa, Kiteto mifugo 62,000 imekufa kwa hiyo janga hili ni kubwa ,"amesema Wambura
"Hali sio nzuri kabisa ni lazima tuchukue hatua za haraka kunusuru hii mifugo, kama tutakubaliana kwa sheria za hifadhi hata kama tutaunda timu kati ya wafugaji na watu wa hifadhi, maana kwenye hifadhi yeyote kuna eneo linaitwa "buffer zone" watueleze hifadhi ya Mkomazi buffer zone iko wapi, ili tuombe iokoe hii mifugo,"amesema Wambura
"Kama kuna utaratibu utakaotumika wakushirikiana kuweka doria kati ya wahifadhi na wafugaji ili kuona kama hii "buffer zone" inatolewa kuoko mifugo hii,lakini ni lazima hatua za haraka zichukuliwe kuokoa mifugo ,"