NGOs zatakiwa kuweka taarifa zao katika mifumo ya kidijitali

Msajili wa NGOs kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Vickness Mayao akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa DigitalNGO ambao unatarajiwa kuwa kichocheo cha mabadiliko na mapokeo ya kidijitali kwa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.

Muktasari:

Serikali imeyataka mashirika yote yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuona umuhimu wa kuweka taarifa zao katika mifumo ya kidijitali badala ya kwenye vitabu au makaratasi kama wanavyofanya sasa.

Dar es Salaam. Serikali imeyataka mashirika yote yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuona umuhimu wa kuweka taarifa zao katika mifumo ya kidijitali badala ya kwenye vitabu au makaratasi kama wanavyofanya sasa.

Aidha mashirika hayo pia yametakiwa kutumika katika kutoa elimu kuhusu muhimu wa sensa ya watu na makazii ili jamii ishiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Msajili wa NGOs kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Vickness Mayao wakati wa uzinduzi wa mradi wa DigitalNGO ambao unatarajiwa kuwa kichocheo cha mabadiliko na mapokeo ya kidijitali kwa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania. 

Mayao amesema Serikali inataka kuona kila taasisi na mashirika inatoka katika matumizi ya karatasi na kutumia mfumo wa kidijitali lengo ni kuangalia ni kwa namna gani wataweza kuzungumza kupitia mifumo hiyo.

"Tunafahamu kuwa mashirika haya yakiwa na mifumo ambayo wameitengeneza wenyewe itawasaidia kuitumia katika utekelezaji wa majukumu yao, serikali kupata data kwa usahihi na kujua  mchango wa NGOs katika maendeleo ya nchi" amesema

Amesema kuelekea katika zoezi la sensa wanatambua kuwa NGOs zina mchango mkubwa katika jamii hivyo wanazihimiza kutoa elimu nzuri ili watu wengi waone umuhimu wa kushiriki na kujitokeza kuhesabiwa.

Naye Mkurugenzi wa Tehama kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku amesema matumizi ya teknolojia ni muhimu hivyo kama wizara wanalisimamia jambo hilo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kidigitali.

"Maana yake taasisi zote za ndani ya nchi ziwe za Serikali au binafsi ziweze kutumia teknolojia ya Tehama katika kufanya shughuli zao ikiwemo kutoa huduma kwa wateja wao," amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Media Convergency, Asha Abinallah amesema mradi huo wa DigitalNGO utajikita katika maeneo manne ambayo ni kufanya kazi na NGOs 35 ambazo zitaonesha utayari wa kufanyakazi ambapo watazisaidia kuzikuza ili ziweze kwenda na kasi ya kidijitali kwa haraka zaidi.

Amesema pia mradi huo utafanya mafunzo na umelenga kuwafikia watu 1000 kwa kila baada ya wiki mbili au tatu pamoja na kuongea mara kwa mara ili jamii iweze kuelewa kwa upana juu ya umuhimu wa mashirika kuendeshwa kidijitali. 

"Pia tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu kutoa taarifa zinazohusiana na mapungufu yaliyopo katika ujuzi wa kidijitali kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na kuwaambia watu fursa zilizopo pia," amesema