NHC itakavyoibadilisha Kariakoo

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (kulia) akikadilishana hati za makubaliana na wabia wa sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya eneo la Kariakoo Dar es Salaam.

Muktasari:

Mikataba 19 iliyosainiwa leo kati ya NHC na wabia wa sekta binafsi ni utekelezaji wa sera ya ubia ya mwaka 1993 iliyoboreshwa, ukilenga kuongeza mapato kupitia kodi ya pango itakayokusanywa miradi itakapokamilika.

Dar es Salaam. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limesaini mikataba 19 yenye thamani ya Sh253.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya kwa kuvunja yale ya zamani katika eneo la Kariakoo.

Mikataba hiyo iliyotolewa kwa wabia wa sekta binafsi ni utekelezaji wa sera ya ubia ya mwaka 1993 iliyoboreshwa, ukilenga kuongeza mapato kupitia kodi ya pango itakayokusanywa miradi itakapokamilika.

Kutokana na maboresho ya sera hiyo, NHC inaweza kupata ubia wa asilimia hadi 50, tofauti na zamani, ambapo ilikuwa ikipata asilimia 25 tu.

Akizungumza leo Januari 29 katika utiaji saini huo uliofanyika jijini hapa, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema miradi hiyo ni matokeo ya maboresho ya sera ya ubia iliyozinduliwa mwaka 2022, ambayo miradi 87 ilitangazwa, ambapo eneo la Kariakoo lilipata miradi 24.

“Ukiangalia kwenye soko la milki Afrika Mashariki na Kati inaonekana ndilo lenye mvuto zaidi wa kibiashara. Ukiangalia kodi inayolipwa kwa mita moja ya mraba, ni kubwa zaidi kuliko nchi zinazotuzunguka. Ni eneo ambalo leo hii ukijenga maeneo ya biashara, kabla hujamaliza kuna wapangaji kuna wanunuzi," amesema Abdallah.

Hata hivyo, amesema miongoni mwa miradi 24 iliyopitishwa, miradi 21 imepata wabia, huku miwili ikisubiri ukamilishaji wa nyaraka.

Mradi utakavyokuwa

Akizungumzia miradi hiyo itakayokuwa na thamani ya Sh271 bilioni, ambapo thamani ya ardhi katika eneo hilo ni Sh59 bilioni, amesema kwa sasa eneo hilo lina wapangaji 190 na maduka 118 na nyumba za makazi 72.

“Baada ya ujenzi kukamilika tunategemea tutakuwa na wapangaji 2,011 kutoka wapangaji 192 na wapangaji wa maduka watakuwa 1,258… tutakuwa stoo 500 na makazi 253 kutoka 72 ambayo leo hii tunayo,” amesema.

Amesema miradi hiyo itaanza kutekelezwa Februari Mosi na itakuwa ya awamu kwa kutegemea utolewaji wa vibali.

Kuhusu vigezo kwa wabia, amesemani pamoja na mbia kuandika barua na kisha kuweka andiko la mradi.

“Kwetu sisi tutaangalia mradi unaotaka kuufanya, je una tija kwa shirika na Serikali kwa ujumla?”amesema.

Ametaja pia uwezo wa kampuni kushirikiana na NHC, akisema walitumia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na hatua ya mwisho ni kuangalia uwezo wa kifedha, kwa kuangalia taarifa za fedha za benki na kama mbia ana mikopo chechefu.

“Tulikwenda kwenye taasisi inayoitwa Credit Information Reference Bureau, tukawachambua huko, kwa sababu benki X inaweza kusema tunamkopesha, lakini kuna benki nne tano zilishamkopesha na mikopo hiyo ni chechefu. Hatuwezi kuingia ubia na mtu ambaye taarifa zake zina walakini.

“Vilevile tuliangalia je huyo mtu hana kesi? Kwa sababu kuna wengine kila siku wanashinda mahakamani wanashitakiana na wengine,” amesema.

Amesema vigezo hivyo vimewekwa kutokana na uzoefu walioupata tangu mwaka 1993 hadi 2000, ambapo baadhi ya miradi ilikwama kutokana na uwezo mdogo wa wabia.

Kutokana na hilo alisema wameshaanza kuirejesha miradi iliyoshindwa kukamilika katika mikoa ya Dar es Slaam, Morogoro, Arusha na Mwanza ambako wametoa masharti kwa wabia.

Wapangaji waliopo

Kuhusu wapangaji waliopo, Abdallah amesema walishapewa notisi ya miezi saba na baada ya hapo watakuwa wakipewa notisi za mwezi mmoja mmoja mpaka vibali vya ujenzi vitakapokuwa vikitoka.

Amesema alifanya mikutano na wapangaji wao wa eneo hilo na amekuwa akikutana nao kila mwezi.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 tunatakiwa kuwapa notisi ya mwezi mmoja yaani siku 30, lakini kwa mujibu wa mikataba ya NHC tuliweka miezi mitatu.

“Tulipata ombi kutoka kwa wapangaji kwamba miezi mitatu si rahisi kupata aternative accommodation (makazi mbadala) tukakubali na kwa Dar es Salaam, tukatoa miezi saba ambayo imeisha Desemba 31, 2023. Kwa hiyo ziada tunayozungumza ni Januari 31, 2024. Haya yote ni jicho la huruma, sio sheria,” amesema. 

Amewatoa hofu wapangaji hao akisema watakuwa wa kwanza kufikiriwa kurejeshwa kwenye majengo mapya watakayoondolewa.

“Wapangaji ni wale ambao wana rekodi nzuri za shirika, kwa hiyo kama kuna mpangaji yeyote wa Kariakoo na maeneo mengine na ana rekodi ya ulipaji, basi watarejea kwenye yale majengo,” amesema.

Akizungumza katika utiaji saini huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa aliyekuwa mgeni rasmi, amesema ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa miradi hiyo haileti taharuki kwa wananchi.

“Tupunguze taharuki kwa wananchi, lakini tuangalie maeneo ambayo wakati mwingine sheria inasema hivi lakini busara inaweza kukuongoza kufanya jambo ambalo tija yake ni kupunguza taharuki kwa wananchi,” amesema.

Kuhusu wapangaji waliopo, amesema kwa kuwa idadi ya nyumba itaongezeka mara tatu, itakuwa ajabu kuwaacha wapangaji wa awali.

“Tutakuwa ni watu wa ajabu, ulikuwa na mpango wako, halafu ukawekeza, unatafuta mpangaji mwingine. Lakini tunaendelea kusisitiza neno wapangaji wazuri,” amesema.

Akisisitiza usimamizi wa miradi hiyo 21, Silaa aliitaka NHC kuanzisha kitengo mahususi kitakachokuwa na watumishi wenye weledi wa kusimamia.

Akizungumza utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Pinetech, Jeddah Hasabubaba ambaye ni mbia wa mradi huo, alisema wameishauri NHC kutenga baadhi ya majengo kwa ajili ya kupaki magari.

“Kariakoo ni eneo maalum lenye msongamano, sasa ukisema uvunje sakafu ya chini, yale maduka ya pale chini hayatakuwepo. Huyu mbia anayekuja anataka marejesho ya haraka, sasa kama atawekeza kwenye eneo ambalo halirejeshi hataweza.

“Tuliomba NHC itoe majengo kwa ajili ya kupaki magari na wamekubali,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya wapangaji wa Kariakoo, Shafiq Mohamed amesema katika majadiliano yao na NHC walikuwa na mambo mawili.

“Kwanza jinsi ya kuondoka kwenye majengo ili kupisha mradi na pili jinsi gani tunarudi. Kwa hiyo mpaka juzi tumekamilisha mchakato baada ya mkurugenzi kutuhakikishia kwamba tutapata barua na Control number (namba ya malipo) kwa ajili ya makazi mapya,” amesema.