NHIF yazusha taharuki tena

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Muktasari:
Maboresho yanayoendelea kufanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yameibua malalamiko na taharuki kwa wanachama, hasa baada ya baadhi ya wategemezi wakiwamo wazazi, kuanza kuondolewa katika mfumo wa matibabu.
Dar es Salaam. Maboresho yanayoendelea kufanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yameibua malalamiko na taharuki kwa wanachama, hasa baada ya baadhi ya wategemezi wakiwamo wazazi, kuanza kuondolewa katika mfumo wa matibabu.
Taharuki hiyo imeibuka siku moja tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuagiza mfuko huo kusimamisha mfumo mwingine wa mabadiliko ulioanza kuutumia Agosti Mosi.
Malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wanachama nchini ni kuhusu kuondolewa kwa wazazi wao na baada ya kufuatilia, wamekuwa wakiambiwa wapeleke vyeti vyao vya kuzaliwa vya wazazi hao na namba zao za Kitambulisho cha Taifa ( Nida).
Kufuatia hali hiyo baadhi ya wategemezi na wanachama waliozungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, walieleza kusikitishwa na utekelezwaji wa utaratibu huo waliodai hawakupatiwa taarifa awali.
“Baba anaumwa, nilimpeleka hospitali juzi, tukaambiwa kadi yake ya bima imefungiwa, nilipouliza sababu, nikaambiwa eti alisajiliwa kama ‘others’ (wengineo) na si mzazi. Nikawauliza kwa nini! Wakasema wakati mfuko unaanza, walikuwa wakisajili mfanyakazi na wategemezi wake ambao hawakuwa wakianisha ni kina nani.
“Kwa hiyo nikaambiwa kuanzia tarehe moja, mfuko umeanza kuwaondoa baadhi ya wategemezi hao, lakini sisi hatujapatiwa taarifa. Nimejaribu kuwauliza hata wenzangu ofisini wanasema hawajui hilo,” alidai Victor Komba, mkazi wa Dar es Salaam.
Komba alisema utaratibu huo umewaletea usumbufu mkubwa na kuwaingiza kwenye gharama ambazo hawakuzitarajia.
Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Joshua Mmari, alisema:
“Kwenye kadi yangu wameondoa wategemezi wote, lakini nimeshangaa kwa nini sasa wanawaondoa na wazazi wangu wote wawili. Nimelibaini hili leo (jana) mama alipoenda kutibiwa Muhimbili akaambiwa jina lake limeondolewa. Akanipigia simu nikaenda hadi ofisi za NHIF zilizopo pale Muhimbili, nikaambiwa nipeleke nyaraka zinazothibitisha kuwa huyu ni mzazi wangu yaani vyeti vya kuzaliwa, niambatanishe na kadi za Nida.’’
Akizungumza kwa masikitiko, aliongeza kusema; “Wazee hospitalini hapa wanahangaika sana, lakini najiuliza kwa nini wanakuja na huu utaratibu kimya kimya bila kutoa taarifa?
Hali Muhimbili
Baadhi ya wagonjwa waliofika Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI na JKCI hasa wazee walionekana wamekaa kwenye mabenchi nje kwa muda mrefu wakisubiri hatma yao baada ya kadi zao za NHIF kukataa kusoma kwenye mfumo na hivyo kushindwa kupatiwa huduma huku wengine wakilazimika kuchangia baadhi ya gharama za huduma.
“Tulifika hospitalini juzi, kadi ikakataa kusoma kwa kuwa baba ni mgonjwa sana, ilibidi tuingie mfukoni na mpaka leo mchana tulishalipia zaidi ya Sh3 milioni kwa ajili ya matibabu yake ya moyo, kitanda na baadhi ya vipimo,” alisema Lahel Sunday mmoja wa ndugu wa mgonjwa anayetibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
NHIF yafafanua
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray alikiri kuwapo kwa mabadiliko katika baadhi wategemezi na kusema wanafanya hivyo ili kurekebisha baadhi ya mianya ya uvujaji wa fedha za mfuko kwa udanganyifu.
“Mfuko huu zamani ulikuwa na wategemezi wengine kama mashangazi, wajomba yaani ‘others’ na hawa tumekuwa tukiwaondoa taratibu mpaka watakapoisha, lakini mzazi ataendelea kubaki.
“Mzazi anapaswa kusajili kama mzazi, lakini kama hatuna nyaraka zozote hatuwezi kuthibitisha. Ndiyo maana tunaomba tupatiwe nyaraka hizo na ukaguzi huu ulianza muda kabla ya vitambulisho vya Nida kuanza kutoka. Sasa inawezekana hao wazazi waliingizwa bila vithibitisho vinavyoonyesha huyu ni mzazi wa Mwanachama,” alisema Mziray.
Alisema namba ya Nida ina taarifa zote, hivyo inapoingizwa kwenye mfumo, taarifa zote za mhusika zinapatikana.