Ni enzi za Mbappe, Haaland

Ni enzi za Mbappe, Haaland

Muktasari:

  • Mchezo wa aina yake aliouonyesha Erling Braut Haaland wakati Borussia Dortmund iliposhinda kwa mabao 3-2 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Sevilla jana Jumatano, ulitokana na kile alichokiona usiku uliotangulia.

Paris, Ufaransa. Mchezo wa aina yake aliouonyesha Erling Braut Haaland wakati Borussia Dortmund iliposhinda kwa mabao 3-2 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Sevilla jana Jumatano, ulitokana na kile alichokiona usiku uliotangulia.

Usiku huo, Kylian Mbappe alifunga mabao matatu na kuiongoza Paris Saint Germain (PSG) kuichakaza Barcelona kwa mabaop 4-1 katika mechi nyingine ya ligi hiyo kubwa ya soka kwa klabu barani Ulaya.

"Naipenda Ligi ya Mabingwa na wakati nilipoona Mbappe akifunga mabao matatu, nilipata hamasa, so kwa hiyo shukrani kwake. Ilikuwa ni jioni safi," alisema Haaland baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi ya jingine la timu yake katika mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya 16 bora nchini Hispania.

Jumanne, Mbappe alifunga mabao hayo matatu na kumzima Lionel Messi na Barcelona katika mechi iliyofanyika Camp Nou nchini Hispania.

Messi aliifungia Barcelona bao la kuongoza kwa njia ya penati, lakini hadi mwishoni timu yake ilionekana kupotea, na anaonekana dhahiri kuwa anaweza kutotwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa mwaka wa sita mfululizo kwa mchezaji nyota wa aina yake, na inawezekana wa kizazi chake.

Mechi za wiki hii za Ulaya zimethibitisha kwamba kwa Mbappe na Haaland, wachezaji chipukizi wawili wanaoinukia, huu ndio wakati wao.

Huu si wakati wa Messi au Cristiano Ronaldo, ambaye alishindwa kuizuia timu yake kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Porto nchini Ureno.

Wote wanaendelea kuwa wafungaji wazuri duniani, lakini Messi amefikisha miaka 33 na Ronaldo miaka 36. Wawili hao wanaoongoza kwa ufungaji katika historia ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa tofauti kubwa, wako katika mawio ya soka lao.

Mbappe, ambaye katika umri wa miaka 22 ameshatwaa Kombe la Dunia na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, amekuwa mchezaji wa pili kufunga mabao matatu dhidi ya Barcelona katika michuano hiyo na katika uwanja wa Camp Nou.

Wa kwanza alikuwa Andriy Shevchenko wakati akiwa na miaka 21 alipoifungia Dynamo Kiev mwaka 1997.

"Paris Saint-Germain ina mchezaji mkubwa wa baadaye, ambaye atakwenda kufikia kiwango sawa na Leo na Cristiano," alisema mshambuliaji wa Barcelona, Antoine Griezmann, mchezaji mwenzake katika kikosi cha Ufaransa.

Katika kipindi cha kwanza dhidi ya Sevilla, Haaland alionyesha mchezo safi, akionyesha nguvu, kasi na umaliziaji, wakati Dortmund ilipozinduka baada ya kutangulia kufungwa.

Mabao yake mawili yamemfanya afikishe jumla ya mabao 18 katika mechi 13 za Ligi ya Mabingwa alizocheza kuanzia msimu uliopita, huku nane akifunga katika mechi nane wakati akiwa Red Bull Salzburg na sasa kumi katika mechi saba za Dortmund.

Mshambuliaji huyo wa Norway anaelekea kufikia rekodi ya Mbappe ya kufunga mabao 19 ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kufikisha umri wa miaka 21 mwezi Julai.

Messi alifunga mabao nane ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kufikisha miaka 21, wakati Ronaldo hakufunga kabisa hadi alipofikisha miaka 22.

Na kingine, wawili hao-- Messi na Ronaldo-- hawajawahi kutwaa Kombe la Dunia, wakati Mbappe tayari.

Kama miaka kumi iliyopita ilikuwa ni ya Messi na Ronaldo, muongo ujao ni wa Mbappe na Haaland.

Na kwa sasa, bado kuna mchezaji mwenzake Mbappe katika klabu ya PSG, Neymar, ambaye kwa ulinganifu ni veterani, akiwa na miaka 29. Na pia yupo Robert Lewandowski.