Ni madudu yaleyale ripoti ya CAG


Muktasari:

  • Abainisha kasoro mbalimbali, zikiwemo zile ambazo hubainishwa katika ripoti za kila mwaka.

Dodoma. Kuongezeka kwa deni la Serikali hadi Sh64.52 trilioni kutoka Sh56.76 trilioni na kuwepo madai ya bima ya afya yaliyohusisha wanaume 56 waliodaiwa kupata huduma ya upasuaji wa kujifungua na wengine kujifungua kwa njia ya kawaida, ni miongoni mwa mambo yaliyobainika katika ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, 2021.

Mbali na hayo, imegundulika mashine 89 za makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani zinazotumiwa na trafiki hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo wa malipo wa Serikali.

Pia, suala la mishahara hewa limeendelea kuitesa Serikali na fidia ya kaya 1,125 za wananchi wa Kipawa, Kigilagila na Kipunguni mkoani Dar es Salaam waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere imeongezeka hadi Sh22.35 bilioni kutoka Sh7.41 bilioni mwaka 1997.

Ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliyoitoa juzi baada ya kuwasilishwa bungeni, ilieleza hayo pamoja na mengine ambayo hujitokeza kila mwaka na hivyo kuashiria kuwa mambo ni yaleyale katika utendaji wa Serikali.

Ripoti hiyo inahusu ukaguzi wa shughuli za Serikali, mifumo ya udhibiti wa ndani na taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021, kuanzia Julai 1, 2020 hadi Juni 30, 2021.

Jumla ya ripoti 20 ziliwasilishwa bungeni jana kuhusu Serikali kuu, mamlaka ya Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo, ukaguzi wa ufanisi, mifumo ya Tehama na ukaguzi maalumu wa mifumo ya Tehama inayohusu mapato.

Ripoti nyingine ni ufutiliaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za ukaguzi wa ufanisi kwa miaka iliyopita na ripoti 12 za ukaguzi wa ufanisi zinazohusu sekta mbalimbali.


Deni lapaa

Kichere alisema hadi kufikia Juni 30, 2021 deni la Serikali lilifikia Sh64.52 trilioni ikilinganishwa na Sh56.76 trilioni za mwaka 2019/2020. Alisema kuna ongezeko la Sh7.76 trilioni, sawa na asilimia 13.7, ikilinganishwa na ongezeko la Sh3.65 trilioni, sawa na asilimia saba kwa mwaka uliopita.

“Hata hivyo, kipimo cha deni la Serikali kinachotumia pato la Taifa kinaonyesha kuwa deni ni himilivu,” alisema Kichere.


Wanaume 56 na ujauzito

Kichere alisema wamebaini upungufu kwenye udhibiti wa mfumo wa madai wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

“Madai yanayoonyesha wanaume walipata huduma ya upasuaji au huduma za kawaida za kujifungua wakati huduma hizi hutolewa kwa wanawake,” alisema.

Alisema wanachama 444 wa NHIF waliopata huduma ya kuchunguzwa picha kamili ya damu (full blood picture) zaidi ya mara moja kwa siku na wengine hadi mara 30 kwa siku kwenye kituo kimoja.

“Udhaifu huu umesababishwa na kukosekana kwa udhibiti katika mfumo wa madai, hali iliyosababisha hasara ya Sh14.41 milioni kwa mfuko,” alisema.


Mashine za trafiki

Kichere alisema kumekuwepo na usimamizi duni wa mashine za POS (point of sale) kwenye mfumo wa ‘TMS’ wa Jeshi la Polisi Tanzania.

“Mfumo wa TMS hutumia vifaa vya POS (mashine za kukusanyia mapato) katika ukusanyaji wa ada na adhabu za makosa yanayotokana na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

“Nilibaini POS 89 zilizosajiliwa na zinazotumika katika mfumo wa TMS ambazo hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo.

“Ufuatiliaji zaidi wa sampuli nne za vifaa vya POS mkoani Dodoma ulibaini kuwa vifaa hivyo havipo kwenye orodha ya rejista ya POS ya mkoa.

“Hii ina maana kuwa vifaa hivyo havitambuliki ijapokuwa vimesajiliwa kwenye mfumo,” alisema.

Vilevile, Kichere alisema wamebaini udanganyifu katika matumizi ya mashine za POS zilizotumika kukusanya mapato katika Halmashauri ya Manispaa Ilala (Jiji la Dar es Salaam).

“Katika kipindi cha miaka ya fedha 2019/2020 na 2020/2021 katika halmashauri ya Ilala nilibaini mawakala wawili walikusanya kwa kutumia mashine za POS kiasi cha Sh131.07 milioni na Sh289,500 milioni mtawalia. Hata hivyo, mawakala hao walirejesha nyuma muda katika mashine za POS kwa kuonyesha makusanyo hayo yalifanyika kati ya mwaka 2008 na 2017, kipindi ambacho hata namba za utambulisho zilizotumika hazikuwa zimesajiliwa katika mfumo wa makusanyo ya mapato.

“Hii ilisababisha makusanyo kutotambulika na kuwasilishwa benki katika miaka husika. Ninapendekeza Serikali ichukue hatua stahiki kwa watumishi na mawakala waliosababisha hasara hiyo,” alisema.


Mishahara hewa

Kichere alisema katika uchunguzi wake alibaini tatizo la ulipaji wa mishahara kwa watumishi wasiostahili na kusababisha upotevu wa fedha za umma.

“Mamlaka ya Serikali za mitaa 25 zililipa Sh556.84 milioni kwa watumishi waliostaafu, waliofariki, waliotoroka, walioachishwa kazi na watumishi waliokuwa likizo bila malipo,” alisema.


Makusanyo pungufu

Katika mwaka wa fedha2020/2021 CAG alibaini kwamba TRA ilikusanya Sh17.59 trilioni kwa Tanzania Bara ikilinganishwa na makisio ya Sh20.29 trilioni ambayo ni pungufu kwa Sh2.70 trilioni (asilimia 13.3) ya makisio.

Alisema kwa upande wa Zanzibar TRA ilikusanya Sh299.08 bilioni ikilinganishwa na makisio ya Sh383.54 bilioni, ikiwa ni pungufu kwa kiasi cha Sh84.46 bilioni, sawa na asilimia 22 ya makisio.


Katikakatika ya umeme

Ripoti hiyo imeeleza kuwa katikakatika ya umeme katika mradi wa kuzalisha umeme wa Mwalimu Nyerere imesababisha madai ya dola za Marekani 8.53 milioni (sawa na Sh19.51 bilioni).

“Nilibaini tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kwenye eneo la mradi kuanzia tarehe 10 Januari 2020 hadi Oktoba 2020 kumesababisha mkandarasi kudai dola za Marekani 8.53 milioni (sawa na Sh19.51 bilioni),” alisema.

Alisema hali hiyo ilisababishwa na kukosa tathmini inayoainisha mahitaji ya umeme wa kuendesha vifaa vya mkandarasi kwenye eneo la mradi.


Mapato yachepushwa

Kichere alisema ukaguzi wake ulibaini kuwa wakusanya mapato katika mamlaka 147 za Serikali za mitaa hawakuwasilisha benki makusanyo yaliyofikia Sh17 bilioni.

Alisema pia mawakala wa kukusanya mapato katika mamlaka za Serikali za mitaa 12 hawakupeleka benki makusanyo ya Sh3.31 bilioni kinyume na mikataba yao.


Halmashauri na faini

Ukiritimba katika kuwalipa wazabuni kulingana na mkataba umezilazimu halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kulipa faini ya Sh972.568 milioni kwa makandarasi.

Miradi hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na Tamisemi katika Manispa za Temeke, Kinondoni na Ilala haikuwa na mifumo jumuishi ya uidhinishaji malipo na kusababisha ichukue muda mrefu kuhakiki hati za madai ya makandarasi.