Ni uzembe uliosababisha vifo 19

Muktasari:

Wadau waeleza upungufu mkubwa kwenye mfumo wa uokoaji nchini.

Moshi/Dar. Ni uzembe. Maneo haya mawili ndiyo yanaweza kuelezea kilichotokea katika ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air iliyoanguka katika Ziwa Victoria mjini Bukoba na kusababisha vifo vya watu 19.

Ndege hiyo ilianguka takribani mita 100 kutoka ulipo Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ikiwa na watu 43 kati yao 39 walikuwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili wa ndege waliokuwa wakitoa Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:53 asubuhi na shughuli za uokoaji kwa sehemu kubwa zilifanywa na wavuvi wakiongozwa na kijana Jackson Majaliwa ambaye alitumia kasia kuufungua mlango wa ndege na kuwezesha watu 24 kuokolewa.

Kijana alipewa zawadi ya fedha na kuahidiwa ajira katika Jeshi la Uokoaji.

Simulizi za baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili zinaeleza kuwa rubani wa ndege hiyo aliwatangazia kuwapo hali mbaya ya hewa, hivyo kuwataka wachukue tahadhari.

Kabla ya ndege hiyo kuanguka, walieleza kuwa ilijaribu kutua mara mbili lakini ilishindwa na kulazimika kuzunguka hewani na hatimaye kuanguka.

Licha ya kuanguka takriban mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege, mijadala na kauli kutoka kwa watu na makundi mbalimbali imeibuka wamehoji uwezo wa vikosi vya uokoaji nchini wakisema vifo vya watu hao 19 kwa kiwango kikubwa ni uzembe.

Wakosoaji wamesema kulikuwa na haja ya kuwepo vikosi na vifaa vya uokoaji katika ukanda wa Ziwa Victoria ni muhimu hasa ikizingatia kutokana na shughuli za majini na ajali kubwa zilizowahi kutoea eneo hilo badala ya vifaa vya wavuvi kama kamba na mitumbi kwa ajili ya kuivuta ndege hiyo kwa muda mrefu.


Ajali inaibua maswali

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza yeye alisema ajali za ndege, meli na treni duniani kote huibua maswali na kuchochea uchunguzi wa kina.

Alisema ajali hii inashtua na kuumiza kwa sababu, “imeua watu wengi wa kada tunayoitegemea itusaidie kuua kifo (madaktari na watumishi wa sekta ya afya). Kifo cha daktari mmoja ni maandalizi ya vifo vya wengi zaidi.


LEAT: Hawa ni mashujaa

Taasisi ya wanasheria wa mazingira (LEAT), jana ilitoa salamu za rambirambi kupitia taarifa yake kwa umma, ikiwashukuru wavuvi na wananchi wa kawaida waliookoa abiria 26.

“Hao ni mashujaa wa kweli na wanatakiwa kuenziwa kwa kupewa nishani za ushujaa wa Taifa hili na pamoja na kutambuliwa kitaifa.

“Hongereni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya na Mungu azidi kuwabariki, nyie ni lulu ya Taifa letu,” ilisema LEAT katika taarifa iliyosainiwa na Dk Rugemeleza Nshalla

Hata hivyo, taasisi hiyo ilieleza imeshtushwa na kusikitishwa na uwezo na udhaifu wa vyombo vya uokozi vya Tanzania kwamba haikutarajiwa kwa miaka 26 tangu ajali ya MV Bukoba, vyombo vya uokoaji vingekuwa havijaboresha utendaji wake.

“Ukweli ni kuwa vyombo na mamlaka husika zimezembea kwa kiwango cha aibu kwa taifa. Wakuu wavyo wote wawajibike na na wakisita wawajibishwe mara moja,” alisema Dk Nshalaa, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kuongeza:

“Kwa kweli havijui kuokoa wakati wa ajali za ndege na majini zinapotokea. Kwamba mwaka 1996 (wakati wa MV Bukoba) wavuvi ndio waliookoa watu na jana wavuvi tena ndiyo waliofanya kazi ya kutukuka ya kuokoa watu.”


Mbatia asema imetosha

Mwanasiasa na mtaalamu wa majanga, James Mbatia naye alizungumzia hali hiyo akiungana na LEAT, kuwa Taifa halikujifunza kutokana na ajali ya meli ya Mv Bukoba ya Mdei 21, 1996 na kuua zaidi ya watu zaidi 900, kwani mbinu zilezile ndizo zilizotumika katika uokoaji.

Mbali na hilo, Mbatia ameilaumu Serikali kwa kutolipatia umuhimu suala la usimamizi wa majanga, akisema tangu Bunge lipitishe sheria namba 7 ya 2015 ya kuanzisha wakala wa majanga nchini, hadi leo mamlaka hiyo haijaanzishwa.

“Si hivyo tu, yaani ni mbinu hizo hizo za kienyeji za uokoaji ndizo zilitumika wakati wa ajali ya Mv Nyerere ya Ukerewe iliyoua watu wetu wengi tu mwaka 2018 na ni mbinu hizo hizo zilitumika jengo lilipoporomoka jijini Dar es Salaam”

“Unajiuliza huelewi, miaka 26 iliyopita na teknolojia imekua lakini leo hii kitendo walichokifanya jana (juzi) wanavyovuta ndege kwa kamba na imeonyeshwa duniani kote CNN, BBC, Aljazera, ni aibu. Hatuna vifaa wala mbinu za uokoaji.”

“Hii ya jana wala si ajali ni mauaji ya uzembe kwa viwango vyote na kitu gani kifanyike, tunahitaji utashi wa kisiasa) tuone uhai wa mtu una umuhimu kuliko kitu chochote. Turudi tutekeleze ile sheria namba 7 ya 2015”


Serikali kufanyia kazi

Wakati wadau wakisema hayo, jana katika hafla ya kuaga miili hiyo 19 katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Waziri Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa aliahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maoni ya wananchi ya kuboresha vifaa vya uokoaji.

Alisema kutokana na maoni ya wananchi ya kuwepo vifaa vya uokoaji watalifanyia kazi kwa kuongeza bajeti kwenye wizara yake kwani wamejifunza na kutajipanga namna ya kuboresha mifumo ya uokoaji.

Bashungwa aliwapongeza wananchi na wavuvi kwa kazi kubwa waliyofanya akisema “bila wao sasa hivi tungekuwa tunaongea mambo mengine.

“Katika tukio lolote, zuri na baya pia ni fursa ya kujifunza,” aliongeza Bashungwa.

Kauli ya Bashungwa iliungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni aliyesema Serikali inaendelea kufanya kila jitihada “kuhakikisha inaviwezesha vyombo vya usalama ili viweze kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga mbalimbali.”

Alisema katika hilo “ni kuongeza bajeti katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na niwahakikishie, tunaendelea kuboresha na wananchi waendelee kutoa ushirikiano.”


Majaliwa kuajiriwa

Katika kuthibitisha kwamba kazi kubwa ilifanywa na wananchi wa kawaida, Waziri Mkuu Kassima Majaliwa alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kumpa mafunzo na kumwajiri katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kijana Jackson Majaliwa kutokana na ujasiri wake wa kupasua mlango wa ndege kwa ngalawa na kuwezesha kuokoa watu 24.

Kijana huyo ambaye aliondolewa wanjani hapo kwa gari la polisi, pia alikabidhiwa Sh1 milioni na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila aliyezema ameagizwa na waziri mkuu waziri mkuu kufanya hivyo.

Kutikana na tukio hilo, mwandishi na mchambuzi wa habari, Edo Kumwembe katika ukurasa wake Instagram aliandika, “na baada ya dogo kupewa Sh1 milioni, tujiulize. “Tupo tayari kukabiliana na majanga ya usoni? Kwamba boti linaloenda Zanzibar ghafla limepata moto pale katikati, watu watafikiwa kwa muda gani na waokoaji watakuwa na vifaa vipi?

“Kwamba sasa hivi kuna jua kali na ukame sawa, lakini tunajiandaa vipi kukabiliana na mafuriko pindi mvua nyingi zikija? Kwamba soko kuu la Mtwara likiungua tutawafikia watu na mali zao ndani ya dakika ngapi? Kwamba ndege ikipata ajali Ziwa Tanganyika, Kigoma kutakuwa na tofauti gani na hii ya jana? Kwamba watu wakifunikwa na kifusi Chunya tutawafikia ndani ya dakika ngapi?

“Kuna mambo mawili; uzembe na umaskini. Lakini sisi tumechagua vyote. Bajeti zina mabilioni ya magari ya anasa lakini sio vifaa vya uokoaji, au sio? Tunatembea na roho mkononi...”

Katibu Mkuu wa Chama cha Marubani Tanzania (Tapa), Kapteni Khalil Iqbal akizungumza na gazeti hili aliwapongeza wananchi akisema bado Tanzania kuna changamoto ya uwepo wa vifaa vya kisasa vya kukabiliana na tukio kama hilo.

“Jana niliona mitumbwi na boti za makasia, sio vifaa sahihi vya uokozi au vya kutoa huduma ile, nadhani mamlaka imeona mapungufu katika mchakato ule. Kuna watu wanatakiwa kuangalia mbali ile ndege ya abiria 43 je, ingekuwa kubwa,” alihoji.

Kwa mujibu wa Iqbal, ndege ile ilipaswa kutolewa katika maji kwa boti maalumu yenye ‘crane’ zinazonyanyua ndege na si kuiburuza na kamba hadi nchi kavu, jambo ambalo huenda likasababisha ugumu kwa watalaamu watakaofanya tathimini ya kujua kilichotokea.

“Tukifanya kama vile jana (juzi), wakati uchunguzi haujafanyika tunaharibu kila kitu, kwa sababu kuna vitu vinaharibika, ndege ilipaswa kutolewa na watalaamu waliosomea na kuiweka katika mazingira salama. Lakini inaeleweka iliondolewa kwa namna ile ili kuokoa mali au kujua kama kuna abiria wengine wapo hai,” alisema.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Baraka Loshilaa, Bakari Kiango, Aurea Simtoe na Tuzo Mapunda (Dar).