Ni vita ya vigogo uchaguzi wa kanda Chadema

Muktasari:

  • Kuna ushindani mkali kati ya wanasiasa wenye majina, kama vile Msigwa na Sugu, Wenje na Pambalu, Jacob na Kileo, Ntobi na Heche, Lema na Mgonja, na wengine.

Dar es Salaam. Chadema hapatoshi. Ndivyo unavyoweza kusema kwa jinsi vigogo wa chama hicho kikuu cha upinzani wanavyotarajia kupigana vikumbo kuwania uenyeviti wa kanda mwezi ujao.

Uchaguzi wa ndani wa chama hicho kwa sasa upo ngazi ya mkoa na mwezi ujao utaingia ngazi ya kanda, ambayo inatajwa kuwa na ushindani mkali, ikiwakutanisha wanasiasa wenye majina ndani nan je ya chama hicho, wakiwemo waliowahi kuwa wabunge au viongozi na kanda zenyewe.

Chadema ina kanda 10 za kiungozi, kati ya hizo saba zinatajwa kuwa na mchuano mkali katika mchakato huo, ingawa bado haujatangazwa rasmi.

Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, mwenyekiti wa kanda ni mjumbe wa vikao vyote vya juu – kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu na pia anaongoza vikao vyote vya kamati ya utendaji vya kanda husika.

Kanda hizo ni Nyasa, Victoria, Serengeti, Kati, Magharibi, Kaskazini na Zanzibar.

Baadhi ya mikoa inayounda kanda hizo imeshakamilisha safu zake za viongozi na  mingine ikiwa hatua za mwisho kabla ya kuanza ngwe ya kanda ambayo mbio zake zinatarajiwa kjutangazwa hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa chama hichoa, John Mrema amesema siku chache zijazo kamati kuu itaketi na kutoa ratiba ya mchakato huo.


Sugu kumvaa Msigwa

Moja ya kanda zinazotarajiwa kuwa na mchuano mkali ni ya Nyasa ambako wabunge wa zamani wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini) wanatajwa kuwania uenyekiti.

Mchungaji Msigwa anatetea nafasi huku Sugu akiwania mara ya kwanza uongozi wa kanda hiyo. Wawili hao ni wajumbe wa kamati kuu ya Chadema.

Alipotafutwa Sugu kuhusu suala hilo, amesema, “ni kweli nina nia ya kuwania uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumza sana hadi mchakato wa chama utakapoanza, nitaeleza malengo yangu yote.”

Vilevile, Mchungaji Msigwa naye alipoulizwa amejibu kwa ufupi, “ndio”, akimaanisha pia anatetea nafasi hiyo.


Wenje vs Pambalu

Shughuli nyingine pevu itakuwa Kanda ya Victoria ambapo mwenyekiti anayemaliza muda wake, Ezekiah Wenje anawania tena nafasi hiyo, akitarajiwa kuchuana na John Pambalu ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana na Chadema (Bavicha) anayetajwa kuiwinda nafasi hiyo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hilo, Pambalu alionekana kushtuka, kisha akajibu, “muda ukifika nitasema.”

Mwandishi alipomuuliza tena ni lini atasema, alijibu huku akicheka “wakati wowote kuanzia sasa.”

Lakini Wenje aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamagama aliweka wazi kuwa atagombea tena, akidai azma na malengo ya kuiondoa CCM madarakani hayajakamilika.

Amesema hajaridhishwa na mwenendo wa Serikali katika kutatua kero za Watanzania, hivyo bado ana kazi kubwa ya kufanya, ndio maana anawania tena uenyekiti wa kanda.

“Kanda ya Victoria tuna majimbo 25, ili tubadilishe hii nchi na kuongoza Serikali Kuu au kuwa na wabunge wengi, lengo langu kama mwenyekiti wa kanda katika uchaguzi unaokuja nipate wabunge 14, ili tuwe na wawakilishi wengine bungeni.

“Sasa mimi nikipata wawakilishi wengi na kanda nyingine zikifanya hivyo, tutakuwa na uwezo wa kuibadilisha nchi katika sheria na sera, ili ziwepo zitakazolisaidia Taifa. Safari bado ni ndefu, hitaji la moyo wangu ni kuiondoa CCM,” amesema Wenje.


Jacob, Kileo nani zaidi?

Swali unaloweza kujiuliza bil majibu ni Kanda ya Pwani, yenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, nani anaweza kuibuka mshindi kati ya Meya wa zamani wa Kinondoni/Ubungo, Boniface Jacob na Henry Kileo, mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Kinondoni.

Wawili hao wanatajwa kuwania uwenyekiti wa kanda hiyo, nafasi ambayo kwa kipindi kirefu inaongozwa na makamu mwenyekiti, Baraka Mwango.

Jacob amethibitisha anakusudia kuwania nafasi hiyo ili kuhakikisha kanda hiyo inanyakua viti vingi vya udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Ni kweli nataka kugombea wakati ukifika, nimekaa benchi kwa miaka minne, sina cheo katika chama, sasa nataka nipewe majukumu ya chama,” amesema Jacob, diwani wa zamani wa Ubungo.

Kwa upande wake, Kileo yeye amesema wakati ukiwadia atalitolea ufafanuzi jambo hilo.

Serengeti ni shughuli

Katika kanda ya Serengeti nako kutakuwa na kibarua kigumu baada ya majina ya John Heche, mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, Emmanuel Ntobi, Gimbi Masaba na Lucas Ngoto kutajwa kuwania ubosi wa kanda hiyo.

Ntobi ameiambia Mwananchi Digital kuwa ana nia ya kuwania nafasi hiyoili kuleta mabadiliko ndani ya kanda hiyo, iwe ya mfano katika kujitegemea kiuendeshaji badala ya kusubiri fedha za makao makuu.

Wakati Ntobi akieleza hayo, Heche ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema amesema kujatwa ni jambo la kawaida, lakini akitaka kuwania nafasi hiyo ataitisha vyombo vya habari kueleza na hakutakuwa na kificho.

“Ni nafasi kubwa ndani ya chama kwa sababu unakuwa kiongozi wa mikoa mitatu, una sekretarieti yako, sasa kama nikitaka kugombea haitakuwa kimyakimya nitaweka wazi, lakini kwa sasa sijafikiria kama nitawania,” amesema Heche.


Kati napo hapajapoa

Kanda ya kati nayo inatajwa kuwa na ushindani mkali baada ya majina ya David Jumbe, Aisha Luja, Devotha Minja, Celestina Simba na Ezekiel Chisijala kutajwa.

Minja amekiri kutaka nafasi ya uenyekiti wa kanda ya kati, akisema muda ukifika ataweka mambo hadharani, sawa na Jumbe ambaye amesema anaitaka nafasi kwa sababu ya uzoefu wake ndani ya kanda.

“Niligombea mwaka 2016, jina langu halikurudi safari nagombea tena kwa sababu nina uzoefu wa kutosha tangu kanda hizi zinaanzishwa mwaka 2013,” amesema Jumbe.

Lakini Luja licha ya kusema ana nia hiyo, amesema hivi sasa ni mapema kuweka mipango yake akisubiri taratibu za chama hicho.


Lema, Mgonja watajwa kaskazini

Kanda ya Kaskazini hadi sasa majina yanayotajwa ni Godbless Lema atakayetetea kiti hicho na Gervas Mgonja ambaye amesema amesikia jina lake likitajwa.

“Nimesikia kama wewe ambavyo umesikia na wengine wananihamasisha, lakini chama hakijatoa utaratibu, kikitoa nitasema kama nina nia au la?” amesema Mgonja.

Kwa upande wake Lema, mjumbe wa kamati kuu Chadema, amesema kwa sasa yupo katika ujenzi wa chama kuhakikisha kinakuwa imara Kanda ya Kaskazini.

“Muda wa kuchukua fomu ukifika nitafanya uamuzi wa kuendelea kuteteaa nafasi hiyo au kutoendelea,” amesema.


Mawakili nao watajwa

Patashika nyingine inatajwa Kanda ya Magharibi ambako majina ya Jackson Shundo (anayetetea), Ngasa Mboje na mawakili Dickson Matata na Peter Madeleka yanatajwa.

Akizungumzia Wakili Matata amesema “Ssijapanga wala kuwaza kama nitagombea, lakini mazingira yakiruhusu nitafanya hivyo kwa sababu naijua vema kanda yangu na nimehudumu kama katibu wa kamati ya sheria haki za binadamu, tusubiri wakati ukifika:”

Alipoulizwa Madeleka amesema “nimemsikia habari hiyo kama ambavyo watu wengine wamesikia. Nitawasikiliza wahusika ambao ni wajumbe wa vikao husika wanataka nini kutoka kwangu, wakiona ninafaa kuwaongoza, itakuwa ni heshima kuwaongoza watu kwa ridhaa yao.”

Baadhi wachambuzi waliozungumza na Mwananchi kuhusu uchaguzi wamewataka watia nia hao kufanya kampeni za kistaharabu zisizochafuana, wakitakiwa kukumbuka kuna maisha baada ya uchaguzi huo.

Mchambuzi wa masuala ya kiasiasa, Buberwa Kaiza amesema mchuano kwenye siasa ni jambo jema hasa wakati wa uchaguzi ambapo wajumbe wanapata fursa ya kufanya uamuzi wa kuchagua kiongozi wanaotaka.

“Kikubwa mtu asilete ubinafsi wake, kwa kutoa maneno ya kumkashifu mwingine badala yake wasimamie chama chao, lakini lazima wajumbe msimamo wa chama chao ili mgombea ajitofautishe na mwenzake katika kuyatekeleza yanayosimamiwa.

Mtazamo wa Kaiza ni sawia na wa Gabriel Mwang’onda ambaye naye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa akisema hatua ni kwa vigogo kujitokeza kuwania uenyekiti katika kanda moja, hali inayoonyesha demokrasia ndani ya chama hicho.

“Sasa Chadema kinatakiwa kionyeshe taswira ya namna viongozi wake wanavyopatikana, je kuna demokrasia au hakuna, lakini huu ndio wakati muafaka kwa chama kujipambanua kuwa ni waumini wa demokrasia,” amesema Mwang’onda.