Uchaguzi Chadema moto, kigogo wa zamani CWT awa mgombea pekee

Muktasari:

  • Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania,  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinaendelea na uchaguzi ngazi mbalimbali huku makada wake wakichuana kuwania nafasi hizo. Rais wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) apitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti mkoa wa Kagera.

Dar es Salaam. Mchuano mkali unatarajiwa kujitokeza katika uchaguzi wa uenyekiti wa mikoa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya vigogo kadhaa kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Chadema kipo katika mchakato wa uchaguzi wa ndani katika ngazi ya mkoa, baada ya kumaliza ngazi za msingi, tawi, kata, jimbo na wilaya kwenye kanda za nane kati ya 10 za chama hicho.

Kanda za Victoria yenye mikoa ya (Mwanza, Kagera na Geita), kanda ya Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu), kanda ya Nyasa (Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa), kanda ya Kusini na (Mtwara, Lindi na Ruvuma), zipo kwenye mchakato wa uchaguzi.

Nyingine ni kanda za Pwani (Dar es Salaam na Pwani), kanda ya Unguja na Pemba. Wakati kanda ya kati (Singida, Dodoma na Morogoro) na kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Manyara) zipo katika mchakato wa uchaguzi huo ngazi ya chini.

Miongoni mwa vigogo hao waliojitokeza ni pamoja na mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Kenan atachuana na Sadrick Malila kuwania uenyekiti wa Mkoa wa Rukwa, wakati Emmanuel Chengula atakabiliana na William Mungai anayetetea nafasi hiyo kwa Mkoa wa Iringa.

Mchuano mwingine utakuwa katika Rose Mayemba anayetetea uenyekiti wa Mkoa wa Njombe, akikibaliana na Ahadi Mtweve huku shughuli pevu ikiwa katika Mkoa wa Mbeya ambapo makada wanne, Karoli Masaga, Peter Mwashiti, Izack Mwambona na Joseph Mwasote anayetetea nafasi hiyo.

Kwa upande wa mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine, baada ya kuhudumu kwa miaka kadhaa kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo mwaka 2023 kwa makosa ya utovu wa nidhamu.

Safari hii Ntobi atachuana na Thadeo Mwasi na Peter Machanga katika usahili wa mchujo uliofanyika jana kabla ya kukutana katika sanduku la kura Machi 28, mwaka huu endapo watapenya.

Naye aliyewahi kuwa Katibu wa Chadema mkoa wa Mara kati ya mwaka 2014 hadi 2019, Chacha Heche amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho mkoani humo.

Heche amekuwa mgombea wa kwanza kurejesha fomu kati ya wanachama watatu waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti.

Fomu ya Heche imerejeshwa na marafiki zake leo Jumamosi Machi 23,2024 katika ofisi za chama hicho mjini Musoma kufuatia yeye kuwa nchini India tangu Januari kwa ajili ya matibabu ya ndugu yake.

Wakati hayo yakijiri, Rais wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba ameteuliwa kuwa mgombea pekee wa uenyekiti wa Mkoa wa Kagera baada ya kamati ya uchaguzi kumuengua mpinzani wake, Jovatus Basheka katika usahili uliofanyika jana chini ya Mwenyekiti Grace Kiwelu

Katibu wa Chadema kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema jana uchaguzi wa uenyekiti, ukatibu wa Mkoa wa Kagera utafanyika leo. Pia mchakato huo utachagua viongozi wa ngome za mabaraza ya wazee, vijana na wanawake.

“Mkoba atapigiwa kura ya ndio au hapana katika uchaguzi huo na mkoa wa Geita tutafanya usahili leo (jana) kesho kutwa Mwanza. Hata hivyo Basheka amekata rufaa itakayotolewa majibu kabla ya uchaguzi utakaoanza kesho saa tatu asubuhi,” amesema Obadi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Mkoba aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), endapo kesho Jumapili wajumbe wakimpa ridhaa atahakikisha anakuwa sauti ya Kagera itakayopenya katika mikoa mingine jirani, akijivunia uzoefu wake wa uongozi katika taasisi mbalimbali.

“Kagera ni kama vile imetelekezwa ndio maana gharama za bidhaa zipo juu ikiwemo sukari, sasa ngoja nipate nafasi tusukume ajenda hizi. Nakuja kufanya kazi sauti yangu itaanzia Kagera na kupenye maeneo mengine,” amesema Mkoba.

Mkoba amesema atahakikisha anaisukuma kwa nguvu za kutosha ajenda ya upatikanaji wa Katiba Mpya ambayo imekuwa ikisimamiwa kidete na viongozi wakuu wa chama hicho. Pia suala la mishahara inayotofautiana na kikokotoo zitakuwa ajenda zake atakazozibeba baada ya kupata kijiti hicho.