Mbowe atoa maagizo ushiriki uchaguzi serikali za mitaa

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametoa maagizo kwa viongozi wa chama hicho kusimamisha wagombea ngazi zote za vijiji, mitaa na vitongoji katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Dodoma. Joto la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu limeanza kushika kasi na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka viongozi wa chama hicho kusimamisha wagombea ngazi zote za vijiji, mitaa na vitongoji.

Mbowe amesema viongozi ambao watashindwa kusimamia hilo na kuwafanya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa watawaondoa kwa kuwa hawatokuwa na sifa za kuendelea kuwa viongozi.

Maagizo hayo ya Mbowe kwa viongozi wenzake ni sawa na yaliyotolewa hivi karibuni na Kiongozi wa Chama (KC) wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu alipowataka viongozi wake na wanachama kujipanga kwa ajili ya uchaguzi huo.

Semu alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyikia Uwanja wa Las Vegas, Mabibo, Dar es Salaam wa kuwataka washindi wa uchaguzi wa ndani Machi 6 mwaka huu, ikiwa ni siku chake tangu kauli kama hiyo itolewe na mtangulizi wake Zitto Kabwe.

Leo Ijumaa Machi 9, 2024, akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) mkoani Dodoma, Mbowe alitumia fursa hiyo kufikisha ujumbe wake juu ya uchaguzi huo. 

Hii ni kauli ya kwanza kwa Mbowe kuitoa juu ya ushiriki wao kwenye uchaguzi ujao.

Baada ya uchaguzi wa 2019 na 2020 ambao wagombea wengi wa chama hicho walienguliwa, Chadema iliweka msimamo wa kutokushiriki uchaguzi wowote hadi yafanyike mabadiliko ya kimsingi katika Katiba na sheria za uchaguzi.

Katika hotuba yake, Mbowe aliwaagiza wanawake hao warudi nyumbani wakajipange katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, akisisitiza hakuna kitongoji, kijiji wala mtaa ambako mgombea wa CCM atapita bila kupingwa na Chadema kwenye uchaguzi huo.

“Kama wewe ni kiongozi kwenye ngazi yako ya uongozi ukafanya uzembe, ukaacha kuweka mgombea kutetea wananchi, hufai kuwa kiongozi, tutakung’oa. Tunaelewana ndugu zangu, kwenye masuala ya msingi ya kazi tusifanye masihara,” amesema.

Mbowe amesema watachekeana katika makongamano kama hilo la jana, lakini ikifika wakati wa kazi ni lazima ifanyike.

Katika kusisitiza hilo, Mbowe amemwagiza Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika (aliyekuwapo), mabaraza yote ya Bavicha, Bawacha na wazee Bazecha) na “mfumo wote ndani ya Chadema”, kuhakikisha kila nafasi inayogombewa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu inawekewa mgombea.

Amesema si mgombea wa kujaza nafasi, bali mgombea wa ushindani wa kushinda kwenye chaguzi hizo.

“Mnajua macho yote na matumaini yote ya Watanzania yako kwa Chadema, kama sisi hatukuweka wagombea, maana yake ni kwamba tumetoa kibali cha CCM kupita bila kupingwa,” amesema

Mbowe amesema maumivu yao yataisha siku watakayojivika ujasiri wa kusimamia haki yao na kwamba wakiendelea kuilalamikia CCM, wataendelea kuumia.

Amewataka wanachama hao kuamua kwenda kufanya kazi kwa nguvu ili waweze kushinda katika chaguzi.

Machi 5, 2024, akihutubia mkutano mkuu wa ACT- Wazalendo, katia ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamilia kuhakikish mchakato wa uchaguzi ujao unakuwa huru na haki.

“Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia ina dhamira ya dhati kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi ulio huru na haki,” alisema Kinana

Alisema, “kuna sheria na kuna dhamira, unaweza kuwa na sheria nzuri, lakini kama huna dhamira nzuri unaweza kuikanyaga hiyo sheria ukafanya unavyotaka. Unaweza kuwa na dhamira nzuri na sheria mbaya lakini dhamira ikitawala mambo yatakuwa mazuri.”

Katika msisitizo wake huku akishangiliwa, Kinana alisema,"nataka niwahakikishie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua uchaguzi wa mwaku huu na mwaka ujao unakuwa huru na haki.”


Khenan apewa maagizo

Awali, katika mdahalo ulioandaliwa na Bawacha baada ya maandamano, Mnyika alimwagiza Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khanan kujiandaa kupeleka Muswada binafsi wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bungeni.

Alimwagiza kufanya hivyo, iwapo Serikali haitapeleka muswada huo kwenye mkutano wa Bunge la Bajeti linaloanza Aprili 2 mwaka huu.

Mnyika alisema lengo ni kuwezesha uchaguzi huo kuwa huru na kusimamiwa na chombo huru badala ya kusimamiwa na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Alisema kanuni za uchaguzi huo zilizotumika mwaka 2019, bado hazijafutwa lakini kulikuwa na taarifa kuwa Serikali itapeleka jedwali la marekebisho kwenye Bunge lijalo.

“Bado kuna utata juu ya usimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa ni lazima tuendeleze mapambano ya kutaka uchaguzi wa serikali za mitaa usisimamiwe tena na Rais kupitia Tamisemi,” alisema.

Aliwataka pia wanawake hao kuhamasisha wengine kwenye vijiji na mtaa ili waweze kushiriki katika uchaguzi huo.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha, Sharifa Suleiman alisema wamejiandaa vyema kushiriki katika uchaguzi unaokuja na kwamba wapo wanawake wengi ambao wameonyesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali.

“Tunapenda kuwaambia Watanzania kuwa hatutawaangusha. Niwaagize akinamama wote nendeni mkaendelee na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hakuna mwenye hatimiliki ya nchi hii, ni nchi yetu sote,”alisema Sharifa.


Wanawake wahimizwa kugombea

Akizungumza katika mdahalo, Wakili na Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dodoma, Hidaya Haonga alivitaka vyama vya siasa kuweka mazingira wezeshi ya kuwawezesha wanawake wengi kushiriki kwenye uchaguzi.

“Katika suala la rushwa katika uchaguzi, kama chama tunaweka mikakati gani ndani ya vyama vyetu, ili wanawake wengi kushiriki katika chaguzi?” alihoji Hidaya.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Victoria Lihim alisema sheria ya vyama vya siasa iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge haijaweka asilimia ambayo vyama vinalazimishwa kuteua wagombea katika chaguzi mbalimbali.

“Sheria hii inawagusa tu, ndio maana viwango havipandi vya idadi ya wanawake walio kwenye uongozi. Ni vyema ikaweka asilimia kama ni 50 au 30 wateuliwe kuwa wagomebea,” alisema.

Awali, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge alisema jumla ya wanawake 3,009 walishiriki katika maadhimisho hayo kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyotanguliwa na maandamano yaliyoanzia katika Soko la Kisasa la Machinga hadi kwenye ukumbi wa Chuo cha Biblia kilichopo Mipango jijini Dodoma lilipofanyika kongamano.

Akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Samia, katika mkutano huo,

Amesema wakati anazungumza hivyo ana uhakika wako ambao wana mashaka na kauli hii, “na hao wenye mashaka wanazo sababu na sababu zao zinatokana na 2019 na 2020 huo ndio ukweli.”

Amesema sheria tulizokuwa nazo za uchaguzi ambazo zilitupeleka kwenye uchaguzi 2015 ziliwezesha wanachama kutoka wa upinzani 117 kuingia bungeni. Sheria hiyohiyo iliwezesha karibu madiwani asilimia 40 kuingia katika nafasi za halmashauri.

“Tulipokuja 2020 kusema kweli lazima tuseme ukweli hofu ya Watanzania, hofu ya wenzangu vyama vya siasa, asasi za kiraia, baadhi ya viongozi wa dini, msingi wa hofu yao ni yale yaliyotokea 2019.

Niwahakikishie Rais Samia Suluhu Hassan ameamua uchaguzi wa mwaka huu na ujao utaachwa ili wapiga kura uamuzi wao ndio utoe tafasiri kwenye uchaguzi ujao,” amesema Kinana

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka 2019 wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambao chama hicho tawala kilinyakuwa viti vingi vya udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.

Mchakato huo ulilalamikiwa na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia waliodai haukuwa wa haki huku wagombea wao wakienguliwa pasipo sababu za msingi.

Kitendo hicho kilifanya baadhi ya vyama vya upinzani kususia shughuli zinazoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).