Ni wakati wa kuwa makini na teknolojia

Muktasari:

Matukio ya kusambaza picha za faragha, mazungumzo ya siri yamekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania kwa sasa, tena wengine ni wale waliojijengea heshima na umaarufu mkubwa kwenye jamii.

Nikitafakari yanayoendelea huko mitandaoni fikra zangu zinanirudisha nyuma kwenye kauli iliyowahi kutolewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, marehemu Ruge Mutahaba.

Ruge aliwahi kusema ‘ogopa sana Mungu na teknolojia’, najua wengi tunafahamu kuhusu Mungu hilo halina mjadala, shughuli imebaki kwenye teknolojia, hapa naona bado kuna tatizo.

Wataalam kila kukicha wanafanya ubunifu na kuongeza vionjo kwenye teknolojia lengo likiwa ni jema itumike kwa manufaa kubwa ikiwa ni kurahisisha, wanaozingatia hilo hakika matunda wanayaona.

Nasikitika kwamba Watanzania wengi bado hatujajua matumizi sahihi ya hizi teknolojia zinazoibuliwa kila kukicha na matokeo yake imekuwa changamoto mpya kwenye jamii.

Tumeletewa simu ili iturahisishie kwenye mawasiliano na kutokana na teknolojia inayotumika sasa ndani ya simu za mkononi kuna mambo mengi hivyo ikitumika vyema tija yake ni kubwa.

Simu za kisasa zina kamera kwa ajili ya kupigia picha, uwezo wa kurekodi mazungumzo zinapopigwa, kinasa sauti na mbwembwe nyingine nyingi zinazorahisisha kusambaa kwa mawasiliano, wenye nia ovu wanatumia maendelo haya kama silaha.

Kwa yanayoendelea sasa ni dhahiri tumeshindwa kutumia teknolojia kutatua changamoto au kujiletea maendeleo na matokeo yake sasa imekuwa kama mwiba wenye sumu.

Matukio ya kusambaza picha za faragha, mazungumzo ya siri yamekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania kwa sasa, tena wengine ni wale waliojijengea heshima na umaarufu mkubwa kwenye jamii.

Nabaki najiuliza hivi heshima hii ina maana gani kama anayeheshimiwa anashiriki kwenye kurekodi masuala yake ya faragha na hatimaye yanafika kwa hadhira.

Ndio wanashiriki kwa sababu, zingine tunazoziona ni wazi mhusika alipiga mwenyewe au alikuwa anafahamu kama picha zinapigwa, hapa nazungumzia kurekodi bado sijafika kwenye kusambaza maana hilo nalo ni janga lingine.

Wapo ambao wanaamini katika kuweka kumbumbuku ingawa binafsi sioni kama kuna umuhimu wowote wa kuhifadhi kumbukumbu za faragha, kwani athari yake ni kubwa zaidi ya faida.

Wakati unaweka mambo hayo kwenye kifaa cha mawasiliano iwe ni simu au kompyuta ni muhimu kutambua kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia upo uwezekano wa vitu vyako kuwafikia wengine.

Mtu anakubali kujivua ubinadamu na kuvaa ngozi ya mnyama mkali aweze kupata sifa ya kumchafua mwingine, yaani utu imekuwa ni kitu adhimu siku hizi, muhimu ni kunyooshana. Inasikitisha kwa kweli.

Yaani sasa imekuwa hakuna kuaminiana, ukimpigia mtu simu unaweza kukuta anakurekodi na mazungumzo yenu akayasambaza kwa kadiri atakavyoona itamfurahisha.

Najiuliza ni faraja gani unapata unapoamua kutumia teknolojia kuwachapia wengine maana kusambaza picha za faragha za mtu mwingine bila kujali zitamletea athari gani ni adhabu kubwa.

Ifike wakati tubadilike Watanzania, tuachane na ulimbukeni huu, tuitumie teknolojia kwa manufaa ili ilete matokeo chanya na si simanzi kama ambavyo imekuwa sasa.

Ingependeza kama tungeona maendeleo haya ya teknolojia yamekuja kuturahisishia vitu, hivyo tukaitumia kama fursa ya kufanikisha michakato ya kimaisha.

Kama wewe ni mfanyabiashara basi itumie teknolojia kujitangaza na kutengeneza mtandao utakaokupatia wateja na kukuwekea mazingira mazuri ya biashara yako.

Vivyo hivyo kwa mwanafunzi unapaswa kutumia teknolojia kukusaidia kujifunza na kukuongezea mtandao wa watu wanaosoma fani kama yako hivyo ni muhimu kuitumia fursa ya kuongeza ujuzi na maarifa.

Kwa mtu ambaye huna shughuli ya kufanya ni wakati sasa wa kutumia teknolojia kukuunganisha na watu ambao unaweza kushirikiana nao au kupata mawazo yatakayokupeleka kwenye shughuli fulani. Usitumie teknolojia kupunguza machungu yako ya kukosa ajira na kuhakikisha unawaumiza wengine.

Tuishi kwa upendo na kuheshimiana, hayo yote yamekuja lakini tunapaswa kuweka mbele utu wa binadamu.

Tukumbuke pia kuhusu sheria za mtandao na adhabu ambazo zinaweza kutolewa kwa kosa la usambazaji wa maudhui yasiyofaa.

Kubwa kuliko yote tujitahidi kuheshimu mwezi huu ili wenzetu wanaoufunga saum zao zikawe njema. Ramadhan Kareem.

Mchambuzi ni mwandishi wa gazeti hili anapatikana kwa [email protected]