Nini kinakuzuia kurudi nyumbani?

Muktasari:

Jioni tulivu baada ya saa za kazi, unazuka mjadala kusaili msimamo mkali wa injinia wa Dodoma. Ikiwa ulipitwa na safu hii wiki iliyopita, simulizi la injinia lililenga kubainisha kile alichokiita siri ya mafanikio yake.

Na Christian Bwaya

Jioni tulivu baada ya saa za kazi, unazuka mjadala kusaili msimamo mkali wa injinia wa Dodoma. Ikiwa ulipitwa na safu hii wiki iliyopita, simulizi la injinia lililenga kubainisha kile alichokiita siri ya mafanikio yake.

Kwanza, haja ya mipango ya pamoja katika familia. Kumtenga mke na mipango ya familia ni kujichimbia kaburi lako mwenyewe. Pili, injinia alikuwa kinyume na utamaduni wa michepuko. Ukiwa tapeli wa mapenzi na ndoa, mafanikio yako yataishia kusambaratisha familia yako.

Pati alisoma simulizi hilo. “Tuwe wakweli,” anaongea kwa sauti iliyojaa mizaha kidogo, “mwanamume gani anaweza kutulia na mwanamke mmoja? Acheni utani wazee”.

Hivi kweli unaweza kumlaumu mwanamume kwa kutoka nje ya ndoa? Nani kati yetu hapa anaweza?” Wajumbe wanacheka kwa ujasiri wenye aibu kwa mbali. Salu anajiunga mezani. Hakuna anayeitikia salamu yake. Kimya kimya Imma anamsogezea kiti akae. Nami ninachokoza zaidi mawazo kwa msisitizo, “Je, uzinzi ni hulka ya kimaumbile isiyokwepeka?”

Imma anaingilia kati: “Tusichanganye mambo. Kwamba wanaume wengi wameshindwa kuwa waaminifu, hivyo hatuwezi kuhitimisha moja kwa moja kwamba uzinzi ni tabia ya kawaida. Saa nyingine ni dhana tu inajengwa kuhalalisha tabia inayoficha matatizo yetu”. Kama vile anahisi haeleweki msimamo wake wa kiimani unakuwa dhahiri. “Huu utamaduni wa kukosa commitment (kupuuza ahadi ya ndoa) umekuwepo tangu enzi na enzi, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba uzinzi unaharibu sana familia.”

Pati anaona jahazi linapwaya waya bila mwenyewe. Huyu hapa: “Kuchepuka ni suala very complex (tata) sana. Tusilichukulie kijuu juu. Kuna vitu vingi vinachangia. Sawa, lakini tusilitazame suala hili kwa macho hasi. Mimi ndoa yangu ingeshakufa siku nyingi isingekuwa mchepuko.” Tunacheka wote kwa wasiwasi. “Ninapokwenda kule nje napata faraja ya kuendelea na maisha yangu bila kusumbuana na mke wangu tusiyeelewana nyumbani.”

Imma amepaliwa kinywaji kwa kugugumia kicheko: “Kumbe michepuko inasaidia kukabiliana na stress za ndoa eh?” “Sidhani,” Mato anamkatisha. “Unatatua tatizo kwa kuanzisha tatizo kubwa zaidi? Huwezi kusema nyumbani pakiwaka moto basi ukichepuka ndo’ unapata utulivu.” Mato anaturudisha kwenye hoja ya awali ya injinia. Mojawapo ya gharama nyingi za uzinzi ni mtu kukosa huo utulivu unaouzungumzia. Hata kama kwa haraka haraka mtu unaweza kujiaminisha kama kuchepuka kunaleta kautulivu fulani, mwisho wake huwa ni kuharibu zaidi familia.”

Imma anawahi asisahau: “Najua kuna wanawake ni pasua kichwa wala hiyo sio ajabu, lakini sioni namna gani kutoroka nyumbani ndio kuwe jibu.”

“Shida yako siasa. Onyesha sasa inawezekanaje?”

“Uaminifu, kama zilivyo tabia nyinginezo, ni matokeo ya uamuzi. Kila kitu kinaanzia kichwani. Nikupe mfano. Wengi wetu hata tuwe wahuni namna gani hatuwezi hata kupata wazo la kutembea na dada zetu wa damu. Vichwa vyetu vinaelewa uwezekano huo haupo.”

“Iamuru akili yako kwamba hakuna kuchepuka. Futa kabisa folder (dhana) kwamba uzinzi ni tabia ya kawaida. Ondoa hilo wazo kichwani kwako na usione uwezekano wowote wa kuchepuka. Ufahamu wako utapokea hicho unachokiamini na mara moja utaanza kuwachukulia wanawake wengine kama dada zako.”

“Hivi ni rahisi kiasi hicho?” anacheka Pati. “Ujue mnachukulia mambo magumu kirahisi rahisi nyie?” Salu anatuuliza. Haonekani kufanya mzaha. Tunatulia kumsikiliza. “Niwape personal experience wazee. Mindset. Fanya hivi, kila siku tengeneza taswira ya familia yako. Acha kujidanganya na kujipumbaza. Uone uzinzi kama ulivyo. Uzinzi kama tabia ya kujificha udhaifu wa kuyakimbia matatizo nyumbani. Halafu jiambie sitachepuka. Ondoa mazingira yoyote yanayokuweka kwenye mtihani.”

Salu anatema cheche. Hakuna kicheko. Namwangalia Pato akiipapasa pete yake. Huenda, naye kama wengine, anawaza mtihani mzito ulio mbele yake. Jinsi ya kurudi nyumbani.