NMB yawashika mkono waathirika wa mafuriko Kilwa

Muktasari:
- Kaya 920 zimekumbwa na mafuriko wilayani Kilwa mkoani Lindi na kusababisha watu kukosa makazi.
Kilwa. Mvua iliyonyesha Mei 4, 2024, imesababisha kaya 920 zinazokaliwa na watu zaidi ya 4,000 wilayani Kilwa mkoani Lindi kukosa mahali pa kuishi.
Watu hao pia hawana uhakika wa chakula baada ya walivyokuwa wamevihifadhi kwenye nyumba zao kusombwa na maji hayo ya mafuriko.
Akizungumza ofisini kwake leo Ijumaa Mei 17, 2024 wakati akipokea misaada ya chakula kutoka Benki ya NMB, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amesema mbali ya nyumba, mashamba ya wakazi hao pia yamesombwa na mafuriko hayo.
"Wilaya ya Kilwa ina watu zaidi ya 4,000 ambao hivi sasa hawana makazi wala chakula kutokana na mashamba yao kusombwa na maji, niwaombe wadau wengine kujitokeza kutusaidia kama walivyofanya wenzao hawa wa NMB,” amesema Nyundo.
Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng'ingo amesema wametoa msaada huo kwa lengo la kuwashika mkono waathirika wa mafuriko na wana imani msaada huo utasaidia kwa kiasi fulani.
"Tumeleta mchele, unga wa sembe, maharage, mafuta ya kula na sabuni kwa lengo la kuwashika mkono wenzetu waliopata maafa, NMB tunawapa pole na tutaendelea kusaidia kadiri ya siku zinavyoenda,” amesema Ng'ingo.
Amesema NMB wanatambua magumu wanayopitia wananchi wa Kijiji hicho cha Mlalani Pande ndiyo maana wameamua kuchangia kidogo kwa lengo la kutatua baadhi ya changamoto wanazozipitia.
Nae Subira Mkandile mkazi wa Mlalani Pande, ameishukuru benki hiyo huku akisema msaada huo utawapunguzia machungu wanayoendelea kukumbana nayo.
"Hiki walichotuletea Benki ya NMB ni kikubwa sana, kitatusaidia kwa siku mbili tatu, lakini tuwaombe wadau wengine waje na wao kututembelea, kwa sasa tunahitaji sana kusaidiwa hasa chakula, hali zetu ni mbaya sana,” amesema Mkandile.