Nyalandu aleta madaktari bingwa 50 kumuunga mkono Samia

Mratibu wa jopo la madaktari kutoka Marekani wanaokuja kuweka kambi nchini ya upasuaji wa mifupa nchini, Lazaro Nyalandu akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Arusha. Katika kuhakikisha afya za Watanzania hasa wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali, kundi la zaidi ya madaktari bingwa 50 kutoka Jimbo la Califonia nchini Marekani, watakuwa nchini kutoa matibabu na ushauri wa kitaalamu bure.
Madaktari hao ambao wamebobea kwenye tiba za mifupa, nyonga na mishipa ya fahamu wanatarajiwa kuwaona na kuwapatia matibabu wagonjwa zaidi ya 200 wenye uhitaji bure.
Waatalamu hao wanatarajiwa kuwasili nchini Agosti 10, 2023 na watapiga kambi kwa siku saba kwenye Hospitali ya Selia inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, mratibu wa ujio wa madaktari bingwa hao Lazaro Nyalandu amesema huduma hiyo ya bure itahusisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaosumbuliwa na maradhi hayo.
Nyalandu, waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii na mdau wa afya nchini amesema madaktari hao watatoa huduma hiyo ya upasuaji kwa Watanzania bure kwa siku saba.
Amesema ujio wa madaktari hao ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi wake.
Amesema wagonjwa ambao watapewa kipaumbele ni kutoka familia masikini na wasiojiweza kulipia gharama za matibabu ya mifupa ambayo inakadiriwa kuwa kati ya Sh50 hadi Sh60 milioni, lakini kupitia mpango huo matibabu hayo yatatolewa bure.
"Ujio wa madaktari bingwa hawa ni kudumisha ushirikiano na kuunga mkono jitihada za Rais wetu mpendwa (Samia Suluhu Hassan) na kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Marekani. Hawa madaktari siku zote wamekuwa wakiguswa na watu wasiojiweza wanaosumbiliwa na maradhi hasa haya ya mifupa ambayo gharama zake ni kubwa. Kupitia mpango huu huduma hii itapatikana bure,” amesema Nyalandu.
Nyalandu ambaye ana histoa ya kuleta madaktari na wataalamu wa afya kutoka Marekani kuja kutoa huduma bure nchini, amesema Tanzania itafanywa kuwa kambi maalumu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji katika Hospitali ya Seliani, Dk Goodwill Kivuyo amesema ujio wa madaktari hao ni fursa kwa Watanzania kupata huduma hiyo bure.
Amesema mpaka sasa tayari wagonjwa 200 kutoka maeneo mbalimbali wameshajiandikisha kuomba huduma hiyo.
"Wagonjwa hawa waliojisajili watapatiwa huduma ya upasuaji na kuonana na madaktari hao ni wale wenye magonjwa ya magoti na nyonga yaliyoshindana katika katika hospitali zetu nchini hivyo, baada ya kambi hii kukamilika umma wa wananchi Watanzania watanufaika," amesema Dk Kivuyo.
Amesema kwa kuanzia wataanza kufanya uchunguzi wa awali ili kuona mgonjwa atanufaika na hayo matibabu kisha watamuingiza kwenye programu ya kuonana na madaktari hao.
Dk Kivuyo amesema tatizo la mifupa linawakumba wagonjwa wengi na kliniki ya Selian ndiyo inaongoza huku asilimia kubwa wakisumbuliwa na magonjwa ya viungo na migongo hivyo uhitaji ni mkubwa wa watu wanahitaji huduma hiyo.
Mohamed Msangi ni miongoni mwa wagonjwa waliojiandikisha kupata huduma hiyo, amesema ujio wa madaktari hao utakuwa mkombozi kwa Watanzania wengi.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Nyalandu kwa jitihada zake za kusaidia matibabu kwa watu wasio na uwezo pamoja na Rais Samia ambaye amejipambanua kuwa mtetezi wa wanyonge.