Nyerere alivyoliomba Bunge liridhie mkataba Muungano

Jumamosi, Aprili 25, 1964 Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, alilihutubia Baraza la Taifa (Bunge) akiliomba liukubali mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar.

Katika hotuba hiyo alisema: “Kwanza nataka kuwaombeni radhi kwa mambo mawili matatu. Kabla ya kurudi majumbani baada ya mkutano wenu wa mwisho mlikuwa mmekubaliana kuwa mtakutana tena tarehe 28, mwezi huu; na Makamu wa Rais alikuwa amewaambieni kwamba ilikuwa nia yangu kuwatangazieni mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano hapo mtakapokutana.

“Kwa bahati mbaya ilibidi nitumie uwezo mlionipa katika sheria yenu moja ya utaratibu wa kazi zenu, nikaahirisha mkutano wenu kwa majuma mawili; yaani mpaka tarehe 12 mwezi ujao.

“Pia kabla ya tarehe hiyo kufika imenibidi tena kuwaiteni hapa. Natumaini mtakubali kwamba sababu zote mbili, ya kuahirisha mkutano wenu na ya kuwaiteni kwa haraka ni za maana. “Nimewaiteni katika kikao hiki cha haraka, ili kuwaomba mthibitishe mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri yetu na Jamhuri ya Unguja.

“Parliament (Bunge) hii ndiyo Baraza Kuu la wananchi wa Tanganyika. Hapana jambo lolote kubwa linalohusu Katiba, au mikataba au sheria za nchi hii ambalo laweza kupitishwa na mtu au kundi lolote ila baraza hili. Mambo yote ya aina hiyo hayana budi yafikishwe katika baraza hili na ni juu yenu kuyakubali au kuyakataa. Leo naleta mbele yenu mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Unguja kuzifanya ziwe nchi moja.

“Tanganyika na Unguja ni nchi za jirani kwa kila hali. Kwa umbali, kila mmoja wenu anajua jinsi tulivyo karibu. Inasemekana kuwa kwa kweli kutoka Unguja au Pemba hadi Tanganyika ni karibu zaidi kuliko kutoka Unguja hadi Pemba. Kadhalika kwa historia, wakati mmoja Unguja na mwambao wa Tanganyika vilikuwa chini ya Serikali moja, yaani Serikali ya Sultani wa Unguja. Ni ajali ya historia tu iliyofanya tusiendelee kuwa nchi moja.

“Wakati wakoloni wa Kizungu walipoanza kuzigawanya nchi za Afrika Mashariki, walikubaliana kwamba Unguja na Pemba na mwambao wa Kenya viwe chini ya ulinzi wa Mwingereza, bali mwambao wa Tanganyika na bara yake viwe chini ya Ujerumani.

“Hivyo ndivyo tulivyoacha kuwa nchi moja. Na baada ya vita vikuu viwili vya kwanza, sisi tulipowekwa chini ya Waingereza, Unguja na Tanganyika tuliendelea kuwa nchi mbili mbalimbali kwa sababu ya utaratibu wa kutawaliwa na Mwingereza.

“Jambo moja ambalo uhuru wetu unatupa katika Afrika ni nafasi ya kuona kama wale tuliokuwa kitu kimoja bali tukatengwa na mkoloni hatuwezi tukaungana tena kuwa kitu kimoja, madhali sasa tumemwondoa mkoloni …Tanganyika na Unguja ni nchi ndugu. Tunashirikiana ujirani kwa historia, lugha, mila, tabia na siasa. Udugu wa Afro-Shiraz Party na TANU wote mnafahamu.

“Udugu baina ya viongozi wa vyama vyote viwili haukuanza jana. Basi, tuna sababu zote hizo za kutufanya tuungane, tuwe kitu kimoja. Juu ya yote hayo kuna shauku ya Umoja wa Bara la Afrika …Basi, mimi badala yenu na President Karume badala ya ndugu zetu wa Unguja na Pemba, tulikutana Unguja siku ya tarehe 22 mwezi huu tukatia sahihi mkataba wa umoja kati ya nchi zetu mbili.

“...Serikali zetu zimekubaliana kuleta umoja kwa sababu moja tu. Umoja ni nguvu ya nchi zetu na ni nguvu ya Afrika. Hapana sababu nyingine …Bwana Spika na wajumbe (wabunge) waheshimiwa, nawaombeni muukubali umoja huu. Sisemi kuwa hatutakuwa na matatizo.

“Tukifanikiwa, wale wasiopenda umoja wa Afrika watastuka. Watastuka kwa sababu watatambua kwamba kweli umoja wa Afrika unawezekana. Kwa hiyo watafanya kila jitihada kutufanya tushindwe. Ni wajibu wetu kujihadhari. Ni wajibu wetu kuulinda umoja huu.

“Tumwombe Mwenyezi Mungu atusaidie sisi na ndugu zetu wa Unguja na Pemba kutimiza wajibu huu,” alisema Mwalimu Nyerere.
Bunge lilikubali kupiga muhuri ombi hilo na Serikali hizo zikaungana kesho yake, Aprili 26.

Hotuba hiyo ya Mwalimu Nyerere iliwashawishi wabunge kuridhia mkataba wa Muungano na kuruhusu nchi mbili kuungana kuwa nchi moja yenye Serikali mbili.
Kisha, Jumapili ya Aprili 26, 1964, kikaja kile ambacho Mwalimu Julius Nyerere (na baadhi ya wengine) alikuwa akikitafuta kwa kipindi chote cha siku 100—Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao baadaye ulikuja kujulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya sherehe fupi za kihistoria, ndipo Sheikh Abeid Amani Karume alipokaririwa na gazeti The Nationalist akizungumza akiwa Zanzibar kwenye lile lililokuwa Kasri la Sultani akitangaza kuwa “Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatufaidisha sisi sote … hautakuwa kikwazo kwa watu wa Zanzibar.”

Jumatatu, Aprili 27, Mwalimu Nyerere alitangaza baraza jipya la mawaziri. Serikali ya Muungano ilitoa viti vitano kwenda Zanzibar kati ya 23 katika Baraza la Mawaziri.

Said Msawanya aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Misitu na Wanyamapori; Jeremia Kasambala (Biashara na Ushirika), Paul Bomani ( Waziri wa Fedha), Oscar Kambona (Waziri wa Mambo ya Nje), Rashidi Kawawa, (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Tewa Said Tewa (Ardhi, Makazi na Maji).

Wengine ni Job Lusinde (Waziri wa Mambo ya Ndani), Kassim Hanga (Viwanda, Madini na Nishati), Solomoni Eliufoo (Waziri wa Elimu), Dereck Bryceson (Waziri wa Afya), Michael Kamaliza (Waziri wa Kazi), Sheikh Amri Abeid (Jamii na Maendeleo ya Utamaduni), Austin Shaba (Serikali za Mitaa na Nyumba), Hassan Moyo (Waziri wa Sheria) na Abdul Idris Wakil (Waziri wa Habari na Utalii).

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama inavyojulikana leo.

Kabla ya tarehe hiyo, kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo yaliingia mkataba wa muungano na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.

Kwa hiyo baadaye ukathibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi. Siku moja baada ya Muungano, Aprili 27, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam na kubadilishana hati za Muungano.

Baada ya Muungano, Mwalimu Nyerere akawa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri.

Shabaha ya Muungano ilikuwa ni kuwaleta pamoja watu wa Tanganyika na Zanzibar kwa lengo la kujenga taifa moja lenye nguvu, ushirikiano na mshikamano kati ya pande hizo.

Utulivu wa kisiasa ulianza kuonekana. Awali, Zanzibar ilikuwa imekumbwa na machafuko na mvutano wa kisiasa, lakini kupitia muungano huo, amani ilirejeshwa na watu wa Zanzibar walihisi kuwa salama na imara.

Hata hivyo, pamoja na nia iliyokuwapo, Muungano ulikabiliwa na changamoto nyingi kuanzia siku ileile ya kwanza na changamoto nyingine zilijitokeza kadiri siku zilivyokuwa zinasogea.

Jumatatu tutaanza kuangazia faida na changamoto za Muungano kutoka kwenye mahojiano na viongozi mbalimbali. Uiskose