Prime
Nyuma ya pazia utapeli mtandaoni
Muktasari:
- Utapeli mtandaoni umepewa majina mbalimbali ya mtaani kulingana na maeneo, yakiwamo mjombamjomba, makeya, gangaley na baba mwenye nyumba.
Dar es Salaam. Wakati operesheni zikiendelea kufanyika kudhibiti utapeli wa mtandaoni, uchunguzi wa Mwananchi umebaini baadhi ya mawakala wa usajili wa laini za simu wanachangia kuwapo kwa mtandao wa uhalifu huo.
Imebainika katika uchunguzi huo kuwapo kwa mtandao wa utapeli wa simu unaojulikana ‘halohalo’, ambao hauhusishi wahalifu pekee, bali pia mawakala wa usajili wa laini za simu wasio waaminifu.
Yaliyobainika yanashabihiana na taarifa ya Polisi Mkoa wa Morogoro iliyotolewa Machi 5, 2026, ikieleza kuhusu kukamatwa kwa laini za simu 198 zinazodaiwa kutumika katika utapeli.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya laini hizo, 88 zilikutwa kwa wakala mmoja wa usajili wa laini za simu, zikiwa zimesajiliwa kwa majina tofauti.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, operesheni iliyofanyika Wilaya ya Kilombero, mbali na kunasa laini hizo, pia iliwanasa watuhumiwa 10 wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa ulaghai uliodaiwa kuwaibia wananchi zaidi ya Sh12 milioni, zikiwamo fedha zilizotapeliwa Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi umebaini wahalifu hao hubadilisha mbinu mara kwa mara kulingana na mazingira na mahitaji ya wananchi.
Baadhi ya ujumbe wanaoutumia unahusisha matangazo ya nafasi za kazi, madai ya kodi za nyumba, taarifa za wanafunzi wanaodaiwa kuwa na dharura shuleni, pamoja na ahadi za tiba au huduma za kiroho.
Utapeli huo umepewa majina mbalimbali ya mtaani kulingana na maeneo, yakiwamo mjombamjomba, makeya, gangaley na baba mwenye nyumba. Majina hayo hutofautisha mbinu zinazotumiwa na wahalifu.
Kwa mfano, makeya unahusisha mhalifu kujitambulisha kama mfanyakazi wa kampuni ya simu na kudai kuna fedha au huduma inayomhusu mtu aliyelengwa.
Kwa upande wa mjombamjomba, wahalifu hujifanya maofisa wa taasisi za Serikali au vyombo vya ulinzi na usalama, wakidai kuna nafasi za ajira zinazohitaji malipo fulani ili mhusika aunganishwe au apatiwe nafasi.
Mbinu zinazotumiwa
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, mawakala wasio waadilifu husajili laini kwa kutumia taarifa za wateja wanaofika kwa ajili ya usajili halali wa namba za simu, kisha huongeza nyingine bila ridhaa au ufahamu wa wahusika.
Laini hizo za nyongeza baadaye huuzwa kwa wahalifu wanaozitumia kupiga simu na kutuma ujumbe wa kitapeli, ukiwamo wenye maudhui kama "tuma kwa namba hii," "mpigie mzee fulani kwa ndagu," "kusafisha nyota," na aina nyingine za ulaghai zinazolenga kuwarubuni wananchi kutuma fedha au kutoa taarifa zao binafsi.
Uchunguzi umebaini laini hizo awali zilikuwa zikiuzwa kwa Sh25,000 kila moja, lakini kwa sasa huuzwa kati ya Sh10,000 na Sh15,000, ikidaiwa hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa upatikanaji wake katika soko hilo haramu.
Inaelezwa kuwa biashara ya laini hizo hufanyika kwa siri, hususan katika maeneo yanayotajwa kuwa na historia ya matukio mengi ya utapeli kwa kutumia mitandao ya simu.
Wauzaji na wanunuzi hutumia njia zisizo rasmi ili kuficha utambulisho wa wahusika na asili ya laini hizo.
Vilevile, imebainika baadhi ya mawakala wa simu huwasajili wananchi wasiokuwa na uelewa wa kutosha wa mifumo ya kidijitali na kutumia taarifa zao kwa malengo mengine tofauti na yale yaliyokusudiwa.
Wataalamu wa masuala ya usalama wa mtandao wanaeleza kuwa matumizi ya laini zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine huwapa wahalifu kinga dhidi ya ufuatiliaji wa vyombo vya dola, kwa kuwa taarifa za usajili huonesha watu wasiohusika na vitendo vya uhalifu vinavyofanyika.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, anayefanya kazi kwenye kibanda cha kusajili laini za simu na kuuza vocha (jina limehifadhiwa), anataja mbinu wanazotumia ili kumfanya mteja asajili laini zaidi ya moja bila yeye kujua.
“Mteja anaweza kuambiwa ameweka vibaya kidole, mashine haijasoma, kwa hiyo arudie kuweka kidole. Pale ndipo huwa tunasajili laini ya pili ambayo tunakuja kuuza kwa wateja wetu wa mtandao wa halohalo,” anasema.
Anasema vitendo hivyo havifanyiki mara nyingi katika maeneo ambayo mawakala wanafahamika, bali vijijini na maeneo ya pembezoni wanapokwenda kutoa huduma za usajili wa laini kwa wananchi.
“Ni vigumu kuwafahamu wanaohusika kwa sababu biashara hiyo hufanyika kwa siri. Mara nyingi laini hizo huuzwa kwa watu tunaofahamiana nao,” anasema.
Ifakara ni miongoni mwa maeneo ambayo shughuli kuu za wananchi ni kilimo cha mazao ya biashara, yakiwamo mpunga, mahindi na ufuta. Kipindi cha mavuno kuanzia Juni hadi Agosti huwa na mzunguko mkubwa wa fedha, hali ambayo wadau wa usalama wanaeleza huwafanya baadhi ya wananchi kuwa walengwa wa matapeli.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Asha Ramadhan, anasema baadhi ya mawakala wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu hujenga uhusiano wa karibu na wahalifu kwa kile alichokiita kulindana pale operesheni za vyombo vya dola zinapofanyika.
Anasema wakala mmoja anaweza kumuuzia mhalifu laini kadhaa ambazo zimesajiliwa kwa majina ya watu tofauti bila ridhaa wala ufahamu wao, jambo linalofanya ufuatiliaji wa wahusika halisi kuwa mgumu.
Uchunguzi umebaini baadhi ya wahalifu hutumia simu zisizo na uwezo mkubwa wa kiteknolojia, maarufu kama viswaswadu, wakiamini ni vigumu kufuatiliwa.
Katika hatua nyingine, wengine huendesha shughuli zao katika maeneo ya vichaka, mashamba au vijiweni, ambako hutuma ujumbe wa kitapeli au kupiga simu kwa namba walizobuni kwa kubahatisha.
“Wanakaa maeneo yaliyotengwa na kuanza kutuma ujumbe au kupiga simu kwa namba wanazobuni. Wakimpata mtu anayejibu kwa namna wanayotaka, ndipo mchakato wa utapeli unaanza,” anasema mmoja wa wakazi wa Ifakara.
Michael Joseph, mkazi wa eneo hilo, anasema baadhi yao huondoka nyumbani asubuhi kama wafanyakazi wengine wa kawaida, lakini huenda katika maeneo maalumu kwa ajili ya kutekeleza shughuli za ulaghai.
“Unaweza kumwona mtu akitoka nyumbani kama anaenda kazini, lakini anakwenda kuungana na wenzake kufanya utapeli wa simu. Mara nyingi hutumia simu za kawaida wanazoamini ni vigumu kufuatiliwa,” anasema na kuongeza kuwa baadhi yao hutuma ujumbe wa simu kwa namba walizobuni kwa kubahatisha.
Ushuhuda wa waathirika
Emil Yohana, mkazi wa Morogoro, anasema aliwahi kupoteza Sh25,000 baada ya kupokea ujumbe uliomtaka atume fedha kwenye namba tofauti na aliyokuwa amekusudia kuitumia.
“Nilikuwa naelekea kwa wakala kutuma fedha kwa mtu niliyemkusudia. Kabla sijafanya hivyo, ukaingia ujumbe ulioelekeza fedha zitumwe kwenye namba nyingine. Nilifuata maelekezo hayo, baadaye nikagundua nilikuwa nimetapeliwa,” anasema.
Kwa upande wake, Mariam Khamis, mkazi wa Dodoma, anasema baba yake aliwahi kutapeliwa Sh350,000 ambazo zilikusudiwa kulipia ada yake ya chuo.
Anasema siku ya tukio alimjulisha baba yake kuwa simu yake ilikuwa inakaribia kuzima kutokana na kukosa chaji, hivyo amtumie fedha kama walivyokuwa wamepanga.
“Baada ya mazungumzo yetu, baba alipokea ujumbe uliokuwa ukionesha fedha zitumwe kwenye namba nyingine iliyodaiwa kuwa yangu. Bila kushuku chochote, akatuma fedha hizo. Baadaye tuligundua zilikuwa zimeenda kwa matapeli,” anasimulia.
Takwimu za TCRA
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha mikoa ya Rukwa na Morogoro inaongoza kwa matukio ya majaribio ya utapeli wa simu kwa miaka kadhaa mfululizo.
Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA ya mwaka 2024, Ifakara, mkoani Morogoro, ilirekodi matukio 3,922 ya utapeli wa simu na ujumbe mfupi, huku Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiongoza kwa matukio 5,198.
Ripoti ya tathmini ya mawasiliano ya Tanzania ya kipindi cha Juni hadi Septemba 2024 ilionesha Rukwa na Morogoro ni miongoni mwa maeneo yaliyoongoza kwa majaribio ya utapeli, licha ya matukio hayo kupungua kwa asilimia 28 katika baadhi ya maeneo ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia.
Hali hiyo iliendelea kujitokeza katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2025, ambapo takwimu za TCRA zilionesha Rukwa ikiongoza kwa majaribio 4,394 ya ulaghai, ikifuatiwa na Morogoro yenye majaribio 3,586. Kwa ujumla, majaribio ya ulaghai nchini yalipungua kwa wastani wa asilimia 10 katika kipindi hicho.
Awali, ripoti ya TCRA ya mwaka 2023 iliitaja Rukwa kuwa kinara wa matukio ya utapeli yanayohusisha kadi za simu, ikiwa na matukio 5,422, huku Morogoro ikifuatia ikiwa na matukio 2,137.
Kwa mujibu wa takwimu za TCRA, majaribio ya ulaghai yalipungua kutoka 12,275 hadi 9,468 katika robo mwaka iliyoishia Desemba 2025. Hata hivyo, changamoto hiyo bado inaendelea kuwapo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ripoti za mamlaka hiyo zinaonesha kuwa katika robo mwaka iliyoishia Juni 2025 kulikuwa na majaribio 13,837 ya ulaghai nchini.
Athari za utapeli
Wakati matukio hayo yakiendelea, takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha Tanzania ilipoteza zaidi ya Sh5 bilioni kutokana na matukio ya udanganyifu mwaka 2024.
Kati ya fedha hizo, Sh288.7 milioni pekee zilirejeshwa kwa waathirika, sawa na asilimia 5.6 ya fedha zote zilizopotea.
Matukio mengi yanahusisha uhamishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi, akaunti za benki na miamala mingine ya kidijitali.
Wataalamu wanaonya kuwa, pamoja na hasara za kifedha, utapeli wa mtandaoni una athari kubwa kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali kwa kupunguza imani ya wananchi katika matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.
Usiku kesho, tutaangazia vitu vinavyokwamisha mapambano dhidi ya utapeli wa mtandaoni