Odinga ajitokeza kanisani, aahidi neema

Mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga

Muktasari:

  • Mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kwenye kanisa la ACK Mtakatifu Francis tangu apige kura Agosti 9, 2022 huku akiwaahidi Wakenya kuwapa maisha bora akiwa Rais.

Nairobi. Mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kwenye kanisa la ACK Mtakatifu Francis tangu apige kura Agosti 9, 2022 huku akiwaahidi Wakenya kuwapa maisha bora akiwa Rais.

Odinga amejitokeza kipindi ambacho Wakenya wamekuwa na shauku ya kutaka kujua matokeo ya kura za urais ambayo yanaendelea kuhakikiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya katika ukumbi wa Bomas

“Sisi kama Azimio la Umoja tunataka kuwapeleka wananchi wa Kenya Kanani kupitia mto Jordani ili wakafurahie maisha mazuri,” amesema Odinga huku akitolea mfano wa vifungu vya biblia.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo mstaafu amesema kuwa anaomba kwa Mungu Amani ambayo imekuwepo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi iendelee hata baada ya matokeo kutangazwa.

“Nataka kumshukuru Mungu kwa hapa alipotufikisha hadi sasa tumepitia kipindi chenye changamoto kama nchi kwenye kampeni na uchaguzi lakini tunamshukuru kwasababu kulikuwa na amani na tunaomba amani hiyo iendelee muda wote hata baada ya uchaguzi kuisha kwa ajiri ya Kenya imara,”amesema.

Akinukuu maneno ya mtakatifu Fransisco wa Asizi akiwa kanisani hapo, Odinga amesema kuwa amemuomba mungu amfanye kuwa chombo cha Amani miongoni mwa Wakenya wote.

 “Bwana nifanye kuwa chombo chako cha Amani, kwenye chuki niuone upendo, kwenye maumivu niponye, kwenye hofu nipe imani, kwenye giza nionyeshe mwanga na kwenye huzuni nipe furaha. Hayo ni maneno ya mtakatifu Fransico aliyoyasema lakini pia natamani kuona bwana akinifanya kama chombo cha Amani kwa ajili ya umoja na mshikamano wa nchi yetu,” amesema.