Waihiga akubali kushindwa urais Kenya

Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Agano nchini Kenya, David Waihiga

Muktasari:

  • Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Agano nchini Kenya, David Waihiga amesema kuwa amekubali kushindwa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na mwenendo wa matokeo kura unaoendelea.

Nairobi. Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Agano nchini Kenya, David Waihiga amesema kuwa amekubali kushindwa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na mwenendo wa matokeo kura unaoendelea.

Kauli hiyo ya Waihiga imekuja huku Wakenya wakiwa na shauku kubwa ya kujua matokeo ya kura za urais ambazo zinaendelea kuhakikiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya ambayo inatarajiwa kutangaza matokeo hayo leo au kesho.

“Wapendwa Wakenya tunakubali kwamba tumeshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 kwenye nafasi ya urais. Tumefikia kusema kauli hiyo kutokana na mwenendo wa kiwango chetu hadi sasa (idadi ya kura),”amesema.

Waihiga ambaye pia ni askofu kutokana na matokeo ya uchaguzi yanayohakikiwa yameonyesha kuwa anaburuza mkia kati ya wagombea wanne akiwa na kura 31,278 ambazo ni sawa na asilimia 0.23.

Hata hivyo kwenye uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9,2022 ni wagombea wawili tu kati ya wanne wa nafasi ya urais hawakuwa kwenye muungano wowote ambao ni David Waihiga na Profesa George Wajackoyah.

Mpaka sasa mchuano ni mkali kati ya mgombea urais wa Kenya Kwanza, William Ruto wenye kura milioni 6.7 na mgombea wa Azimio Kwanza Raila Odinga mwenye kura milioni 6.6.