Ole Sendeka: Kama shida kuwatetea wananchi sitarudi nyuma

Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (kulia) akizungumza na mbunge wa Afrika Mashariki, James Ole Millya kwenye mkutano wa hadhara, alipokwenda kuzungumza na wananchi kuhusu gari lake kushambuliwa kwa risasi. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Machi 29 mwaka huu Ole Sendeka na dereva wake Hassan, gari lao lilishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana katika Wilaya ya Kiteto katikati ya vijiji vya Ndedo na Ngabolo.

Simanjiro. Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema ikiwa ameshambuliwa na risasi kwa sababu ya kuwatetea wafugaji, hatarudi nyuma kuwatetea.

Machi 29 mwaka huu gari walilokuwamo Ole Sendeka na dereva wake Hassan lilishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana kwenye Wilaya ya Kiteto katikati ya vijiji vya Ndedo na Ngabolo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara leo Jumatatu Aprili mosi, 2024 katika mji mdogo wa Orkesumet baada ya tukio hilo, Ole Sendeka amesema hatarudi nyuma katika kuwasemea wafugaji na wana Simanjiro kwa ujumla.

Amesema hata hivyo, hausishi tuko hilo na yeye kutetea ardhi kwa sababu wiki iliyopita alikaa na viongozi wa Serikali wakajadili suala la ardhi ya wafugaji kugeuzwa kuwa pori tengefu.

"Mimi na viongozi wakubwa tujadili suala la hilo na walihakikisha kuwa hatutakubali kubadilisha ardhi yenu ya wafugaji iwe hifadhi ya wanyama," amesema Ole Sendeka.

mesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hahusiki na kushambuliwa kwake kwa risasi.

Hata hivyo, amesema alishambuliwa akiwa na gari lake lililopigwa risasi 18 kwa kutumia silaha mbili tofauti kijeshi baina ya SMG au AK47 na kuwa risasi nne ziliingia kwenye gari

"Mimi nilipiga juu risasi mbili katika kujihami ila tukio hili lilichukuwa kama dakika mbili ila ilikuwa vita kubwa mno," amesema.

Amesema baada ya tukio alipigiwa simu ya kupewa pole na viongozi wakubwa wakiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu Mwenyeki wa CCM Abdulrahaman Kinana.

"Nilipigiwa simu ya kupewa pole na hadi Ikulu na marafiki wengine mbalimbali ambao hata siwajui," ameema mbunge huyo.

Amesema nchi 15 duniani zilimpigia simu kumpa pole kutokana na kushambuliwa kwake na kunusurika kuuawa na watu wasiojulikana.

"Nimepata pole kutoka mashirika mbalimbali ya haki za binadamu duniani na nchi mbalimbali za Afrika wakinipa pole kwa kurushiwa risasi nikanusurika kuuawa," amesema Ole Sendeka.

Hata hivyo, amesema hawezi kumtaja mtu yeyote kuhusiana na tukio hilo kwa sababu  hana uhakika na aliyemshambulia kwa risasi.

"Namuachia Mungu kwani atamuumbua na kumuweka hadharani aliyetaka kuchukua maisha yangu kwa kunipiga risasi," amesema Ole Sendeka.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, James Ole Millya aliyekuwa kwenye mkutano huo amesema tukio hilo ni la kinyama na linapaswa kulaaniwa.

Ole Millya amesema Tanzania ni nchi ya amani ila matukio ya viongozi kutaka kuuawa kwa risasi yanawapa hofu wananchi.

"Kama tukio hili limetokea kwa sababu Ole Sendeka anatetea ardhi ya wafugaji tutamuunga mkono kwani anajali masilahi ya watu wengi," amesema Ole Millya.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema wana Simanjiro wapo nyuma ya mbunge wao, hivyo asiogope kuwatetea.

"Huwezi kutaka kuchukua maisha ya kiongozi wa watu kwa sababu ya masilahi yako binafsi hili ni tukio baya mno katika maisha ya kisiasa," amesema Kanunga.

Diwani wa Langai, Jackson Sipitieck mesema Serikali ina mkono mrefu, ichukue hatua kwa kuwatia mbaroni wahusika wote.

"Hao wahuni waliosababisha tukio hilo wanapaswa kutiwa mbaroni kupitia mkono mrefu wa Serikali," amesema.

Diwani wa Ruvu Remit, Yohana Maitei amesema tukio hilo ni lenye ukatili mkubwa hivyo wahusika wachukuliwe hatua.

Wakati wasiasa hayo wakisema hayo, Kaimu Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu amesema mpaka sasa hawajamkamata mtu yeyote kuhusiana na shambulio hilo.

"Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na tunatarajia kuwakamata wote waliohusika na uhalifu huo," amesema Mwakatundu.