Gari la Ole Sendeka lashambuliwa kwa risasi

Kiteto. Gari la mbunge wa Simanjiro (CCM) mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, limeshambuliwa kwa risasi akiwamo ndani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu akizungumza na Mwananchi Digital amesema tukio hilo limetokea jioni ya leo Ijumaa Machi 29, 2024.

Amesema limetokea eneo la Ndaleta, wilayani Kiteto wakati Ole Sendeka akiwa na dereva wake akielekea jimboni kwake Simanjiro.

"Ole Sendeka akiwa na dereva wake, gari lao lilishambuliwa kwa risasi ila hawakudhurika ni wazima kabisa," amesema Kaimu Kamanda Mwakatundu.

Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi na hakuna anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.

Kaimu Kamanda amesema kwa sasa Ole Sendeka na dereva wake wapo Kituo cha Polisi Kiteto wakiendelea kuhojiwa kuhusu tukio hilo.

Mbali na ubunge, Ole Sendeka amewahi kuwa msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Desemba 7, 2016 aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli, alimteua Ole Sendeka wakati huo akiwa msemaji wa CCM kuwa mkuu wa mkoa huo.

Machi 2016, CCM kilimteua Ole Sendeka kuwa msemaji wake.

Uteuzi wake ulitangazwa Machi 20 mwaka huo na Abdulrahman Kinana, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Msemaji wa awali wa chama hicho, alikuwa Nape Nnauye ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.

Wakati wa uteuzi huo, Ole Sendeka alikuwa ameshahudumu kwa nafasi ya ubunge wa Simanjiro tangu mwaka 2010.

Ole Sendeka alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa alichukua nafasi iliyoachwa na Dk Rehema Nchimbi, ambaye Rais Magufuli alimuhamishia Mkoa wa Singida kujaza nafasi ya Mhandisi Mathew Mtigumwe aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo anayeshughulikia Kilimo.

Julai, 2020 Ole Sendeka alikabidhi ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe akaenda kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika jimbo la uchaguzi la Simanjiro, mkoani Manyara.